Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 31
Januari, 2018 amezindua mfumo wa uhamiaji mtandao (e-Immigration) ambao utasaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa
mipaka ya nchi, kudhibiti ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali na kuimarisha
utoaji wa huduma za kiuhamiaji kwa raia wa Tanzania na wageni wanaoingia na
kuishi hapa nchini kwa madhumuni mbalimbali.
Uzinduzi
wa mfumo huo umefanyika katika ofisi kuu ya uhamiaji Jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na
Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan,
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Mhe. Seif Ali Iddi, na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Wengine
ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Omar Othman Makungu, Spika
wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Zubeir
Ali Maulid, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson
Mwansasu, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mhe. Dkt. Ali Hassan Mwinyi na Rais
Mstaafu wa Zanzibar Mhe. Amani Abeid Karume.
Kabla
ya kuzindua mfumo wa uhamiaji mtandao Mhe. Rais Magufuli amekagua teknolojia
iliyotumika katika mfumo huo ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa alama za vidole na
baadaye kupatiwa pasipoti mpya ya kielektronikia (e-Passport) ambayo pia imeanza kutolewa leo.
Pasipoti
mpya za kielektronikia pia zimetolewa kwa viongozi wengine wakuu wa Serikali, Bunge na Mahakama wa
Tanzania Bara na Zanzibar, waliohudhuria uzinduzi huo.
Mhe.
Rais Magufuli amempongeza Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba
na Idara ya Uhamiaji kwa kufanikisha mradi wa kuweka mfumo wa uhamiaji mtandao
na kuanza kutoa pasipoti mpya ya kielektronikia kwa gharama
nafuu ya Shilingi Bilioni 127.2 ikilinganishwa na makadirio yaliyowekwa awali ya Shilingi
Bilioni 400.
“Hapa
tumeokoa fedha nyingi za Watanzania, kuna watu walikuwa wamejiandaa kutupiga na
kuchukua hizo Shilingi Bilioni 400, lakini tukatumia vyombo vyetu mbalimbali,
tukafanya uchunguzi na
tumefanikiwa kutekeleza mradi huu kwa gharama nafuu”
amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha,
kwa kutambua kazi nzuri inayofanywa na idara ya uhamiaji baada ya kupokea maelekezo yake ya
kutakiwa kufanya mabadiliko makubwa, Mhe. Rais Magufuli ameahidi kutoa Shilingi
Bilioni 10 kwa ajili ya kujenga ofisi ya makao makuu ya idara hiyo Mjini
Dodoma.
“Kamishna
Jenerali Dkt. Anna Makakala na timu yako mnafanya kazi nzuri, ndio maana nimewanunulia
nyumba 103 kwa ajili ya wafanyakazi kule Dodoma na leo nitawapa fedha nyingine
Shilingi Bilioni 10 mkajenge ofisi nzuri ya makao makuu, nyinyi endeleeni
kuchapa kazi, endeleeni kukamata wahamiaji haramu na endeleeni kukusanya mapato
vizuri” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mapema
akitoa taarifa ya mfumo wa uhamiaji mtandao, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt.
Anna Peter Makakala amesema mfumo huo ni muunganiko wa mifumo mbalimbali ambayo
imesanifiwa kufanya kazi kwa pamoja, kutoa taarifa kwa watumiaji na wadau wa
huduma za kiuhamiaji na kwamba kupitia mfumo huo idara ya uhamiaji inatarajia
kutoa pasipoti za kielektronikia (e-Passport),
viza za kielektronikia (e-Visa), vibali vya ukaazi vya
kielektronikia (e-Permit) na udhibiti
wa mipaka wa kielektronikia (e-Border
Management) kwa awamu nne hadi ifikapo mwisho wa mwaka huu 2018, pamoja na
kutoa pasipoti ya kielektronikia ya Afrika Mashariki ya Tanzania.
Balozi
wa Ireland hapa nchini Mhe. Paul Sherlock ameipongeza Tanzania kwa kufanikisha
mradi huu na kueleza kuwa mfumo huu wa uhamiaji mtandao ni alama muhimu ya
Taifa.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar
es Salaam
31
Januari, 2018
SHARE
No comments:
Post a Comment