Watumishi
wa afya 22 katika hospitali ya Kolandoto manispaa ya Shinyanga
wamerudishwa kazini na mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro mara
baada ya kutumbuliwa na uongozi wa hospitali hiyo kutokana na kutoa
malalamiko yao mbele Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana Athony
Mavunde alipofanya ziara yake Februari 27,2018.
Watumishi
hao walifukuzwa kazi siku moja baada ya ziara ya Naibu Waziri huyo
kwenye hospitali hiyo ambayo aliifanya Februari 27 mwaka huu mara baada
ya kutoa malalamiko yao juu ya kunyanyaswa na hospitali hiyo ambapo
kesho yake wale waliojifanya wazungumzaji 'kiherehere' wakatimuliwa kazi
na kutolipwa stahiki zao zote.
Akiongea
Machi 1, 2018 na uongozi wa hospitalini hapo mkuu wa wilaya ya
Shinyanga Josephine Matiro alisema mara baada ya kupewa taarifa hizo juu
ya watumishi hao kuwa wametimuliwa kazi baada ya kusema ukweli kwenye
ziara ya Naibu Waziri huyo, jambo hilo limemkera na kuamua kufika kwenye
hospitali hiyo kuwarudisha kazini.
“Kuanzia sasa watumishi wote mliowafukuza kazi wanarudi kazini na
ninatoa siku 14 wawe wameshalipwa haki zao zote wanazodai, ikiwamo
malimbikizo ya mishahara, makato ya NSSF,TUGHE, pamoja na kulipwa
mishahara kiwango cha serikali, na msipofanya hivyo ndani ya siku hizo
tutawachukulia hatua,”alisema.
"Kwanza hospitali hii mmeidharau serikali kwa sababu haiwezekani
kiongozi mkubwa kama yule Naibu waziri anafanya ziara ya kusikiliza na
kutatua kero za watumishi, halafu ninyi kesho yake mnawafukuza kazi, huo
ni utovu wa nidhamu”,alisema Matiro.
Naye mmoja wa watumishi hao walifukuzwa kazi Elizabeth Zabron alisema
baada ya kutoa malalamiko yao juu ya kunyanyaswa kwenye mishahara na
madai mbalimbali, muda mfupi tu baada ya kuondoka Naibu Waziri huyo
wakaona majina ya watu 22 yakiwa yamebandikwa kwenye ubao wa matangazo
wakiitwa kesho kuonana na uongozi wa hospitali hiyo.
Alisema baada ya kwenda kuonana na uongozi huo wakajua tayari kilio chao
kimesikika cha kulipwa mishahara na madai yao, ambapo wakashangaa
wanaambiwa kuwa wamefukuzwa kazi na wanatakiwa kusaini barua hizo bila
ya kuzisoma, ndipo wakagoma na kuamua kwenda kushitaki kwa mkuu huyo wa
wilaya ili wapate haki zao.
Barua hizo kwa ndani zilikuwa zimeandikwa kuwa "unafukuzwa kazi na
hutakiwa kulipwa haki yako yoyote na kutakiwa kuondoka eneo la kazi mara
moja".
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt .Maganga Dohoi
alikiri kuwafukuza kazi watumishi hao na kudai kuwa bodi ya hospitali
hiyo ilikaa na kuagiza watumishi wote wasio na sifa ya kuwa na vyeti vya
kidato cha nne lakini wana taaluma ya uuguzi wafukuzwe kazi, ndipo naye
akafuata maagizo hayo.
Hata hivyo mmoja wa wajumbe wa Bodi ya hospitali hiyo Magezi Magedi
ambaye pia ni ofisa utumishi wa halmashauri ya manispaa ya Shinyanga,
alikana kukifahamu kikao cha kufukuza watumishi hao , na kudai kama
suala la kufukuza kazi kuna taratibu zake zinatakiwa kufuatwa na siyo
kuwafukuza hovyo hovyo.
Alisema hospitali hiyo isitumie kivuli cha serikali kufukuza watumishi
hao ikiwa suala la vyeti vya darasa la Saba lilikuwa la watumishi tu wa
serikali.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza na watumishi wa
afya katika hospitali ya Kolandoto waliotimuliwa kazi.-Picha na Marco
Maduhu - Shinyanga News blog & Malunde1 blog
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akionyesha masikitiko namna
walivyotendewa ndivyo sivyo watumishi hao wa afya katika hospitali ya
Kolandoto kwa kutimuliwa kazi kisa wametoa malalamiko yao mbele ya Naibu
waziri wa Kazi,Ajira na Vijana Anthony Mavunde.
Mmoja wa watumishi waliofukuzwa kazi Elizabeth Zabroni akielezea kisa cha kufukuzwa kazi
Emmanuel Makungu naye alidai wamekuwa wakilipwa mishahara lakini
hawapewi Salary Slip wala kusaini popote na kutokujua umeingia mshahara
wa mwezi gani na pia michango ya NSSF wamekuwa wakiambiwa imeingizwa
lakini wakifuatilia hakuna pesa yoyote iliyowekwa pamoja na fedha za
likizo kutopewa, na kubainisha kuwa walipotoa malalamiko yao mbele ya
Naibu Waziri wa Kazi,Ajira na Vijana Antony Mavunde iliwapate haki zao
wakaonekana kuwa kikwazo na kutimuliwa kazi.
Sara Mkem akionyesha kusikitishwa na uongozi wa hospitali hiyo kwa
kuwafukuza kazi kisa wametoa matatizo yao mbele ya Naibu Waziri huyo ili
yapate ufumbuzi, na kuonekana kuwa kero na kutimuliwa kazi, bila hata
ya kujali utu wao pamoja na kulazimishwa kusaini barua bila ya kuzisoma
na kudai uongozi huo una roho ya kinyama kwani huenda ina dhamira ya
kutaka arudi uraiani akauawe na watu wabaya kwa kumkata viungo vyake.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt Maganga Dohoi akijitetea kwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro
Baadhi ya watumishi waliofukuzwa kazi na uongozi wa hospitali ya
Kolandoto wakiwa kwenye kikao na mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine
Matiro na uongozi wa hospitali hiyo kutatua suala lao la kufukuzwa kazi
mara baada ya kutoa kilio chao kwa Naibu Waziri wa Kazi,Ajira na Vijana
Antony Mavunde juu ya manyanyaso wanaoyapata .
Watumishi wa afya waliofukuzwa kazi katika hospitali ya Kolandoto wakiwa
kwenye kikao cha kutatuliwa matatizo yao na mkuu wa wilaya ya Shinyanga
Josephine Matiro mara baada ya kumpelekea matatizo yaliyowakumba ya
kutimuliwa kazi kinyemela bila ya kufuata sheria za kazi.
Kikao kikiendelea.
Watumishi wa afya katika hospitali ya kolandoto waliofukuzwa kazi kenyemela wakiwa wameshika bango la kutaka haki yao
Ofisa utumishi wa halmashauri ya manispaa ya Shinyanga,Magezi Magedi
ambaye pia ni mjumbe wa bodi ya hospitali hiyo ya Kolandoto akikana
kukifahamu kikao cha kufukuza kazi watumishi hao na wala tangu
achaguliwe kuwa mjumbe wa bodi hiyo hajawahi kuitwa hata kikao kimoja
na kudai kama suala la kufukuza kazi watumishi hao kuna taratibu zake
zinatakiwa kufuatwa, na siyo kuwafukuza hovyo hovyo na kuwalazimisha
kusaini barua bila ya kuzisoma.
Ofisa kazi mkoa wa Shinyanga Revocatus Mabula alisema taratibu za
kuwafukuza kazi watumishi hao zilikiukwa ambapo hawakupewa notes na
walistahili kupewa haki zao zote ndani ya siku 14,kulipwa kiinua
mgongo,malimbikizo ya likizo zao zote pamoja na kusafirishwa mahali
walipotoka makwao na siyo kuambiwa tu wamefukuzwa kazi na hawatolipwa
pesa yoyote.
Katibu
wa Chama Cha Wafanyakazi TUGHE, Tabu Mambo alisema hawajahi kuona
mchango wowote wa watumishi hao waliofukuzwa kazi licha ya kuambiwa kuwa
wanalipiwa na kubainisha kuwa walipokuwa wakifika kuzungumza na
watumishi hao walikuwa wakikosa ushirikiano kutoka kwa viongozi wao, na
wale watumishi ambao walioonekana kuwa wanajua kuongea ndiyo kidogo
walikuwa wakitolewa michango hiyo.
Picha na Marco Maduhu - Shinyanga News blog & Malunde1 blog
SHARE
No comments:
Post a Comment