Waziri
wa Maliasili na Utalii Mhe. Prof. Jumanne Maghembe (wa pili kushoto)
akikabidhiwa taarifa ya makabidhiano ya ofisi na aliyekuwa Waziri wa
Wizara hiyo Mhe. Lazaro Nyalandu (wa pili kulia) leo tarehe 29 Desemba
2015 ofisini kwake Mpingo House. Wanaoshuhudia makabidhiano hayo ni
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Adelhelm Meru (kushoto) na Naibu Katibu
Mkuu Ndugu Selestine Gesimba (kulia).
Aliyekuwa
Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Singida
Kaskazini Mhe. Lazaro Nyalandu (kushoto) akizungumza na Waziri wa sasa
wa Wizara hiyo Mhe. Prof. Jumanne Maghembe na Katibu Mkuu Dkt. Adelhelm
Meru (kulia) wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi yaliyofanyika
leo tarehe 29 Desemba 2015 katika ofisi za Wizara hiyo Mpingo House.
Katika salamu zake Mhe. Nyalandu amepongeza uteuzi wa Prof. Maghembe
ambapo amesema Mhe. Rais amefanya chaguo sahihi kwani Prof. Maghembe
anao uwezo wa kufanya kazi nzuri katika Wizara hiyo.
Waziri
wa Maliasili na Utalii Mhe. Prof. Jumanne Maghembe akizingumza na
aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la
Singida Kaskazini Mhe. Lazaro Nyalandu (kulia) muda mfupi baada ya
makabidhiano ya ofisi yaliyofanyika ofisini kwake leo. Mhe. Prof.
Maghembe amempongeza Mhe. Nyalandu kwa kazi nzrui aliyoifanya akiwa
Waziri wa Wizara ya Malisili na kuahidi kuanzia alipoishia katika
kuhakikisha Maliasili za nchi zinatunzwa ipasavyo ikiwemo kupambana na
changamoto zilizopo za ujangili na uharibifu wa misitu na maliasili kwa
ujumla.
WAZIRI
wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe amekabidhiwa rasmi ofisi
na aliyekuwa Waziri kabla yake Mhe. Lazaro Nyalandu, Makabidhiano hayo
yamefanyika leo Makao Mkuu ya Wizara hiyo, Mpingo House jijini Dar es
Salaam.
Katika
makabidhiano hayo Mhe. Nyalandu amekabidhi taarifa rasmi ya
makabidhiano kwa Mhe. Waziri Prof. Jumanne Maghembe kama ishara ya
kukabidhi rasmi Ofisi ya Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Makabidhiano
hayo ambayo ni utaratibu wa kiserikali wa kukabidhi ofisi umeshuhudiwa
na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Adelhelm Meru, Naibu Katibu Mkuu, Bw.
Selestine Gesimba, baadhi ya watumishi wa Wizara hiyo na waandishi wa
habari.
Akizungumza baada ya makabidhiano hayo Mhe. Nyalandu amempongeza
Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumteua Prof. Maghembe kuwa
Waziri wa Wizara ya Maliasili kwa kuwa ana sifa stahiki za kuongoza
Wizara hiyo nyeti.
Aliongeza kwa kusema kuwa Prof. Maghembe ana sifa ya kuwa mhifadhi
kwa kusomea na pia ni mhifadhi kwa asili yake hivyo Wizara imepata mtu
makini kwenye masuala ya Uhifadhi.
“Natambua umahiri wako katika masuala ya uhifadhi nina imani
utapambana na ujangili pamoja na usafirishaji haramu wa magogo kwa kasi
inayotarajiwa na wananchi”. Alisema Mhe. Nyalandu.
Kwa upande wake, Waziri aliyechukua nafasi yake Prof. Jumanne
Maghembe amempongeza Mhe. Nyalandu kwa kazi nzuri na juhudi aliozoonesha
wakati akiwa Waziri wa Wizara hiyo katika kuhakikisha Maliasili
zilizopo zinaendelea kuwepo kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
Prof. Maghembe ameongeza kuwa kwa sasa vita kubwa iliyoko mbele
yake ni vita dhidi ya ujangili na uharibifu wa misitu ikiwa ni pamoja na
usafirishaji wa rasilimali za misitu kinyume cha sheria. Ameomba
ushirikiano kwa wadau wote wa Maliasili nchini kumpa ushirikiano wa
kutosha kuhakikisha anafanikiwa katika vita hiyo.
Pamoja na mambo mengine taarifa hiyo ya makabidhiano inaelezea
kazi zilizokwisha kufanyika katika kipindi cha utawala uliopita, kazi
zinazoendelea na zilizopo kwenye mpango wa utekelezaji pamoja na
changamoto mbali mbali zinazoikabili sekta ya Maliasili na Utalii
ikiwemo Ujangili na uvunaji pamoja na usafirishaji wa magogo.
(Na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Maliasili na Utalii)
SHARE
No comments:
Post a Comment