Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Mawasiliano Prof. Faustin
Kamuzora alifanya ziara ya kutembelea Shirika la Posta Tanzania ili
kufahamu utendaji kazi na utekelezaji wa majukumu ya Shirika.
Katika ziara hiyo Prof. Kamuzora
aliambatana na Naibu Katibu Mkuu wake Dkt. Maria Sasabo na kufanya
mazungumzo na Menejimenti ya Shirika hilo. Katika ziara hiyo Prof.
Kamuzora alimuagiza Kaimu Posta Masta Kuu wa Shirika la Posta Tanzania
Ndugu Fortunatus Kapinga kuhakikisha kuwa ukusanyaji wa mapato yote ya
Shirika la Posta Tanzania (TPC) nchi nzima yanafanyika kwa kutumia njia
ya elektroniki ambapo alisema kuwa, “Shirika liboreshe mifumo yake ya
kielektroniki ili kupunguza mianya ya wizi na upotevu wa fedha za
Shirika na kufanikisha ongezeko la ukusanyaji wa mapato ya Serikali”.
Prof. Kamuzora aliongeza kuwa
Shirika la Posta Tanzania liendane na mabadiliko ili liende kuwahudumia
wananchi wa sasa na wa vizazi vijavyo. Shirika ni la kipekee na lina
nafasi nzuri ya kutoa huduma kwa wananchi kama ambavyo Shirika kama hili
linafanya kazi nzuri kwenye nchi ya China na Brazil.
Aidha, Prof. Kamuzora aliwaagiza
Viongozi wa wasimamizi wa Shirika la Posta Tanzania kutumia Sheria,
Kanuni na taratibu za kuwasimamia wafanyakazi na kuwachukulia hatua kali
na za kinidhamu watumishi wazembe; wasiotimiza majukumu yao; wasio
waaminifu na wabadhirifu. Aliongeza kuwa watendaji wafanye kazi na
kusimamia Shirika kwa kuwekeana malengo kama inavyojulikana kisheria kwa
kutumia Mfumo wa wa Wazi wa Upimaji Utendaji Kazi (OPRAS). Alisisitiza
kuwa, “Sheria zilizopo zinatosha kumsimamisha mtumishi kazi kwa makosa
na hatimaye kumfukuza kazi kwa kuwa watumishi wazembe na wasio waadilifu
wanawafanya wananchi wawe na mtazamo hasi na Serikali yao”.
Prof. Kamuzora alisema kuwa
wateja wanahitaji huduma nzuri; ya uhakika na kufikishiwa vifurushi,
barua, vipeto na bidhaa nyingine kwa wakati. Aliwaagiza viongozi wa
Shirika kuangalia uwezekano wa kupunguza gharama za uendeshaji ili
kuendesha Shirika kwa tija na faida. Prof. Kamuzora alisema, “Uchumi wa
nchi hauwezi kukua wala kwenda popote bila kufanya kazi kwa tija.
Alivitaka vyama vya wafanyakazi visiwatetee watumishi wazembe na
vishirikiane na Serikali kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Shirika
na watumie mtandao mpana wa Shirika uliopo nchi nzima na kuangalia fursa
zilizopo ili kufikisha huduma kwa wateja.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo
anayeshughulikia Mawasiliano ambaye aliambatana na Katibu Mkuu wake Dkt.
Maria Sasabo aliagiza kuwa, “Shirika lijipange haraka na kuongeza kasi
ya utendaji kazi ya kuwahudumia wateja wake na wananchi ili kuweza
kuendana na Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli”. Dkt. Maria Sasabo aliongeza
kuwa Shirika la Posta lipo nchi nyingi duniani na bado linahitajika
hivyo ni muhimu kujipanga kuendana na mahitaji ya sasa ya wateja na
Shirika libadilishe utaratibu wa utendaji kazi na kuondoa urasimu ili
kuweza kuwahudumia wateja. Dkt. Maria Sasabo aliwaagiza viongozi wa
Shirika wafanye tathmini na kuangalia namna bora ya kujiendesha ikiwemo
kupitia upya muundo na majukumu ya Shirika.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo
anayeshughulikia Mawasiliano Prof. Kamuzora aliuagiza uongozi wa Shirika
la Posta Tanzania kuongeza matumizi ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano kwa kuwa na huduma za ziada za kisasa zinazoendana na
mahitaji ya wateja kwa kutumia biashara mtandao kusafirisha na
kufanikisha usambazaji wa huduma na bidhaa za wateja kama vile uagizaji
wa magari; vitabu na bidhaa nyingine kwa kushirikiana na kampuni kubwa
duniani kama vile Alibaba, Amazon na eBay.
SHARE
No comments:
Post a Comment