Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha sherehe za
kuadhimisha miaka 50 tangu Benki Kuu ya Tanzania ilipoanzishwa.
Sherehe
hizi zitafanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania
jijini Dar es Salaam tarehe 22/06/2016 ambapo mgeni rasmi atazindua
vitabu viwili na kufuatiwa na kongamano litakaloshirikisha wataalam
mbalimbali wa uchumi wakiwemo magavana 20 wa benki kuu kutoka nchi za
Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Mada
kuu katika Kongamano hilo itakuwa: “Beyond Aid and Concessional
Borrowing: New Ways of Financing Development in Africa and its
Implications”, (yaani namna ya kupata fedha za miradi ya maendeleo zaidi
ya misaada na mikopo nafuu na athari zake) itakayowasilishwa na Prof.
Justin Lin wa Chuo Kikuu cha Peiking, China. Mada hii imechaguliwa kwa
kuzingatia changamoto ambazo serikali za Afrika zinakumbana nazo katika
kugharamia miradi ya maendeleo wakati ambapo misaada na mikopo nafuu
imekuwa ikipungua kwa kiasi kikubwa.
Wachumi
waliobobea wa ndani na nje ya nchi, wakiwemo magavana 20 kutoka nchi za
Jumuiya ya Afrika mashariki (EAC) na wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za
Kusini mwa Afrika (SADC) watashiriki katika kongamano hilo.
Vitabu
vitakavyozinduliwa siku hiyo ni (i) “Tanzania: The Path to Prosperity”
kinachoelezea masuala yanayohusu sera za uchumi nchini Tanzania ambacho
kimeandikwa na wachumi waliobobea wa ndani na nje ya nchi, na
kimechapishwa na Oxford University Press. (ii) Kitabu cha pili ni cha
miaka 50 ya Benki Kuu ya Tanzania kiitwacho “50th Anniversary of the
Bank of Tanzania: Evolution of the Bank of Tanzania’s Role and
Functions”, ambacho kinaelezea historia, majukumu, mafanikio na
changamoto za Benki Kuu katika kipindi cha miaka 50 na matarajio ya
Taasisi hii ya Umma katika maendeleo ya taifa katika kipindi cha miaka
50 ijayo.
Aidha,
Tarehe 11/6/16 Mheshimiwa Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa atakuwa
Mgeni Rasmi kwenye matembezi ya hisani ya wafanyakazi wa Benki Kuu
kutoka makao makuu ya Benki hadi viwanja vya Mnazi Mmoja kuchangia
ununuzi wa madawati ya shule za msingi kama sehemu ya maadhimisho ya
miaka 50 ya Benki. Wafanyakazi wa Benki Kuu walioko matawini Mtwara,
Mwanza, Dodoma, Arusha, Mbeya, Zanzibar na Chuo cha Benki Mwanza nao pia
watafanya matembezi ya hisani kwenye mikoa yao.
Pamoja
na matembezi kutakuwa na maonesho yaliyoandaliwa na Benki Kuu katika
viwanja vya Mnazi Mmoja yenye lengo la kuwapa wananchi historia ya
taasisi hii, ilikotoka, ilipo na inakoelekea katika kutekeleza majukumu
yake.
Benki
Kuu ingependa kuwakaribisha wananchi kufika kwa wingi kwenye viwanja
vya Mnazi Mmoja siku hiyo ya tarehe 11/6/16 kujifunza mengi kuhusu
taasisi hii ya umma.
Aidha,
tunawaomba wananchi kufuatilia vipindi mbalimbali vya redio na makala
kwenye magazeti ambapo mengi kuhusu historia, changamoto, mafanikio na
matarajio ya Benki yataelezwa na viongozi mbalimbali wa Benki wa sasa na
waliopita.
Benki
Kuu ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 1965 na
kuanza kutoa huduma rasmi tarehe 14 mwezi Juni mwaka 1966. Katika
kipindi cha uhai wake, Benki Kuu ya Tanzania imetimiza majukumu yake kwa
mujibu wa sheria na kulingana na mahitaji ya taifa yalivyojitokeza
mwaka hadi mwaka.
Imetolewa na:
Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki
03/06/2016
Wanachuo wa Royal Diffence College watembelea Wizara ya Mambo ya Nje
Mkurugenzi
wa Idara ya Ulaya na Amerika, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Balozi Joseph Edward Sokoine, akitoa maelezo ya awali
wakati wa kuanza kwa mkutano na wanafunzi
wa chuo cha Ulinzi cha Royal College of Diffence Studies kilichopo
nchini Uingereza (hawapo pichani), ambao wapo kwenye ziara ya mafunzo
katika nchi za Tanzania, Ethiopia na Malawi kwa ajili ya kubadilishana mawazo namna masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa yanayoibuka hivi sasa yanavyoathiri utulivu, usalama na ustawi wa nchi, kanda na dunia kwa ujumla. Mwingine katika picha ni Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Balozi Samuel Shelukindo.
Baadhi ya wanachuo hao wakisikiliza maelezo kutoka kwa mzungumzaji meza kuu (hayupo pichani). Masuala
mbalimbali yalijadiliwa ikiwa ni pamoja na hali ya usalama katika eneo
la nchi za maziwa makuu, nafasi ya wakuu wa nchi za Afrika katika utatuzi wa migogoro, uhusiano wa Tanzania na nchi jirani na mikakati ya kukabiliana na ugaidi katika kanda na dunia kwa ujumla.
Baadhi
ya wanachuo pamoja na Askari wa JWTZ (waliovaa sare), wakisikiliza
maelezo kutoka kwa mzungumzaji meza kuu (hayupo pichani).
Mmoja wa wanachuo hao akiuliza swali.
Balozi Sokoine, akifafanua jambo.
Kikao kikiendelea.
======================
PICHA NA: REUBEN MCHOME.
SHARE









No comments:
Post a Comment