Mkurugenzi
wa Sheria kutoka Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi
ya Jamii (SSRA), Bw. Onorius Njole akizungumza na waandishi wa habari
leo jijini Dar es Salaam kuhusu Mpango Maalum wa kutoa huduma ya hifadhi
ya jamii kwa sekta isiyo rasmi maarufu kama Informal Sector Scheme
ambayo inajumuisha waendesha bodaboda, bajaji na mama lishe. Kulia ni
Mkuu wa Uhusiano na Uhamasishaji wa SSRA, Bi. Sarah Kibonde.
Mkuu wa
Kitengo cha Uhusiano na Uhamasishaji kutoka Mamlaka ya Usimamizi na
Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Bi. Sarah Kibonde
akiwaeleza waandishi wa habari juhudi za Serikali katika kuboresha na
kupanua wigo wa huduma za hifadhi ya jamii hasa kwa wananchi walio
kwenye sekta isiyo rasmi. Kushoto ni Mkurugenzi wa Sheria kutoka SSRA,
Bw. Onorius Njole.
Mkurugenzi
wa Sheria kutoka Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi
ya Jamii (SSRA), Bw. Onorius Njole akizungumza na waandishi wa habari
leo jijini Dar es Salaam kuhusu Program maalum ya kutoa elimu ya hifadhi
ya jamii kwa Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na Waratibu wa Mifuko
ya Bima ya Afya ya Jamii nchini kote. Zoezi hilo linaenda sambamba na
usajili wa mifuko hiyo. Kulia ni Mkuu wa Uhusiano na Uhamasishaji wa
SSRA, Bi. Sarah Kibonde na kushoto ni Afisa Uhusiano Ally Masaninga.
Baadhi ya
Waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano wa SSRA uliofanyika leo jijini
Dar es Salaam ambao ulilenga kuufahamisha umma maboresho mbalimbali
katika sekta ya hifadhi ya jamii nchini.
Na Fatma Salum (MAELEZO)
Serikali
kupitia Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii
(SSRA) imejizatiti kupanua wigo na kuboresha huduma za hifadhi ya jamii
hasa kwa kundi la watu walio kwenye sekta isiyo rasmi.
Hayo
yamebainishwa na Mkurugenzi wa Sheria kutoka Mamlaka ya Usimamizi na
Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Bw. Onorius Njole wakati
akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu
Mpango Maalum wa kutoa huduma ya hifadhi ya jamii kwa sekta isiyo rasmi
maarufu kama Informal Sector Scheme ambayo inajumuisha waendesha
bodaboda, bajaji na mama lishe.
Bw. Njole
alisema kuwa katika kuhakikisha watanzania wote wananufaika na huduma
za hifadhi ya jamii, SSRA inafanya tafiti mbalimbali na kuhamasisha
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kubuni mafao mbalimbali yanayolenga kuwafikia
wananchi wote walio kwenye sekta isiyo rasmi.
Ili
kufanikisha hilo, mwaka 2015 SSRA ilifanya utafiti katika sekta ya
usafirishaji na kubaini kuwa asilimia 83 ya waendesha vyombo vya usafiri
mijini wakiwemo waendesha bodaboda wako tayari kuchangia kwa hiari
katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
“Kutokana
na matokeo hayo mamlaka ilipendekeza kuanzishwa kwa Mpango Maalum
ujulikanao kama Informal Sector Scheme ambapo watu waliojiajiri kwenye
sekta isiyo rasmi watapata nafasi ya kunufaika na huduma ya hifadhi ya
jamii.” Alisema Njole.
Njole
aliongeza kuwa tayari baadhi ya mifuko imekwishaandaa mafao maalum
yanayowalenga waendesha bodaboda, bajaji, daladala na mama lishe ambao
watapata fursa ya kuchangia kiasi kidogo kila siku kulingana na kipato
chao ili kupata huduma za hifadhi ya jamii kama vile akiba ya uzeeni,
matibabu na mikopo.
Aidha,
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Uhamasishaji wa SSRA, Bi. Sarah Kibonde
alieleza kuwa mamlaka hiyo inaendelea na zoezi la kutambua na kusajili
Mifuko yote ya Bima ya Afya ya Jamii (CHFs) kwa lengo la kuboresha
huduma na kuimarisha mfumo wa utoaji huduma za afya kwa wananchi.
Pia Bi.
Sarah alisema kuwa SSRA imeandaa program maalum kwa ajili ya kutoa elimu
ya hifadhi ya jamii kwa Wakurugenzi wa Halmashauri na Waratibu wa
Mifuko ya Bima ya Afya ya Jamii nchini kote na zoezi hilo linaenda
sambamba na usajili wa mifuko hiyo kwa mujibu wa Sheria ya SSRA, Sura ya
135.
“Program
hii imeanzia Kanda ya Kati ambako ilihusisha Wilaya 27 na jumla ya CHF 5
zilisajiliwa na nyingine 22 zinakamilisha taratibu za usajili. Zoezi
hili linatarajiwa kuendelea Juni 22 kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini
ambako jumla ya CHF 25 zinatarajiwa kusajiliwa.”
Sambamba
na program hiyo Serikali kupitia Wizara ya Afya na Wizara yenye dhamana
ya masuala ya hifadhi ya jamii na SSRA inafanya mapitio ya mfumo wa
usimamizi wa Mifuko ya Bima ya Afya ya Jamii (CHF) ili kupata mfumo
utakaoweza kutoa huduma ya afya kwa watanzania wote. (P.T)
SHARE








No comments:
Post a Comment