Jana
ilikuwa ni siku ya Kimataifa ya Wakimbizi, Umoja wa Mataifa umesema watu
waliopoteza makaazi ya kote duniani imefikia rekodi mpya. Ujerumani
iliyapokea maombi mengi ya hifadhi kuliko nchi nyingine yoyote
Shirika
la Umoja wa Mataifa la Kuwashughulikia Wakimbizi – UNHCR limesema kuwa
kiwango cha mateso na mizozo katika nchi kama vile Syria na Afghanistan
kimeongeza idadi ya wakimbizi na watu walioachwa bila makao nchini mwao
kote duniani kufikia watu milioni 65.3 hadi mwishoni mwa mwaka jana,
ikiwa ni kiwango cha juu zaidi kuwahi kushuhudiwa.
Mwaka
uliotangulia, wa 2014, ulikuwa tayari umeshuhudia idadi kubwa ya
wakimbizi kote duniani tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia, ambapo watu
milioni 60 waliachwa bila makaazi. Lakini mwaka jana – wakati Ulaya
iliyumba kutokana na mmiminiko wa wahamiaji – uliongeza idadi hiyo kwa
karibu asilimia 10 kwa mujibu wa takwimu za UNHCR.
Shirika
hilo lenye makao yake mjini Geneva limewaomba viongozi wa UIaya na
kwingineko kuchukua hatua zaidi ili kumaliza vita ambavyo vinasababisha
mmiminiko wa watu kutoka manyumbani mwao. Filippo Grandi ni kamishena
mkuu wa Umoja wa Mataifa "Kile wakimbizi na wahamiaji wanaovuka bahari
ya Mediterania na kuwasili katika fukwe za Ulaya, ujumbe ambao wanaubeba
ni kuwa iwapo hautayatatua matatizo, matatizo yatakukujia. Na huo ni
ujumbe mkali".
UNHCR
inasema kuwa kwa kiwango cha wastani, watu 24 walipoteza makaazi kila
dakika, kila siku mwaka jana – au watu 34,000 kwa siku – ikiwa ni kutoka
idadi ya watu sita kila dakika katika mwaka wa 2005. Idadi ya watu
waliopoteza makaazi kote duniani imeongezeka maradufu tangu mwaka wa
1997, na kuongezeka kwa asilimia 50 tangu mwaka wa 2011 pekee – wakati
vita vya Syria vilianza.
Zaidi ya
nusu ya wakimbizi wote walitokea nchi tatu: Syria, Afghanistan na
Somalia. Uturuki ndiyo nchi iliyoongoza kwa kutoa hifadhi kwa mwaka wa
pili mfululizo kwa kuwapa hifadhi karibu watu milioni 2.5 – karibu wote
kutoka nchi jirani Syria. Nchi jirani ya Afghanistan, Pakistan ilikuwa
na watu milioni 1.6, wakati Lebanon, Syria, iliwapa hifadhi watu milioni
1.1.
Watunga
sera na makundi ya uhamasishaji yanakiri kukabiliana na changamoto kubwa
za kuwasaidia watu wengi walioachwa bila makaazi: ambao ni karibu watu
milioni 40.8 wanaoishi katika kambi za ndani mwa nchi zenye migogoro.
Grandi
amesema zaidi ya watu milioni moja walikimbilia Ulaya mwaka jana, na
kusababisha mzozo wa kisiasa katika Umoja wa Ulaya. "Hakuna mpango
mbadala kwa Ulaya katika siku zijazo, hakuna mpango mbadala. Ulaya,
imekuwa, na itaendelea kuwapokea waomba hifadhi. Takwimu huenda
zikatofautiana. Natumai zitapungua, maana kuwa matatizo yatapungua.
Kwamba labda kutakuwa na msaada zaidi kwa nchi nyingine kuwapa hifadhi
watu hao, lakini haliepukiki".
UNHCR
imezitolea wito nchi kupambana na chuki dhidi ya wageni ambayo
imeandamana na ongezeko la idadi ya wakimbizi, na ukalalamikia vizuizi
vinavyowekwa kama vile nyua zinazojengwa na baadhi ya nchi za Ulaya –
pamoja na vya kisheria ambavyo vinawazuia wakimbizi kuingia katika nchi
tajiri na zenye utulivu zaidi.
Takwimu
zinazozusha hofu katika ripoti hiyo zinaonyesha kuwa watoto walijumuisha
asilimia 51 ya idadi ya wakimbizi kote ulimwenguni mwaka jana. Wengi
watoto hao walipoteleana na wazazi wao au walisafiri peke yao, ambapo
zaidi ya maombi ya hifadhi 98,400 yaliwasilishwa na watoto ambao
hawakuandamana na wazazi.
Shirika
la kuwashughulikia watoto nchini Ujerumani limetoa wito wa kupewa elimu
watoto wakimbizi zaidi ya 8,500 ambao wazazi wao hawajulikani waliko.
Mkuu wa shirika hilo Thomas Kruger ameliambia gazeti la “Neue
Osnabrücker Zeitung” kuwa watoto hao wanakabiliwa na kitisho cha kuingia
katika ukahaba, utumwa, au hata kuuzwa kwa ajili ya biashara haramu ya
viungo vya mwili. DW
SHARE








No comments:
Post a Comment