Mkurugenzi
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani akizungumza na
waandishi wa Habari mjini Musoma kuwaeleza mkakati wa NEC wa kuwafikia
wananchi moja kwa moja kuwapatia elimu ya mpiga kura.
Mkurugenzi
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani akizungumza na
waandishi wa Habari mjini Musoma kuwaeleza mkakati wa NEC wa kuwafikia
wananchi moja kwa moja kuwapatia elimu ya mpiga kura.
Na. Aron Msigwa – NEC, Musoma
Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeanza kutekeleza programu endelevu za kutoa
elimu ya mpiga kura ili kuwaelimisha wananchi waliofikisha umri wa
kupiga kura kutekeleza wajibu na haki waliyonayo kikatiba ya kupiga
kura katika chaguzi zijazo.
Kauli
hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima
Ramadhani wakati akizungumza na waandishi wa Habari mjini Musoma kuhusu
mkakati wa NEC wa kuwafikia wananchi moja kwa moja kuwapatia elimu ya
mpiga kura.
Amesema
kuwa Tume hiyo imeanza kutoa elimu hiyo kwa kushiriki maonesho na
mikutano mbalimbali ukiwemo mkutano wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa
Tanzania (ALAT) unaofanyika mjini Musoma kuanzia Septemba 22 hadi 24
mwaka huu.
“Tumeamua
kushiriki kwenye mkutano huu kwa kuwa hawa ni watendaji wa Serikali
katika ngazi za mitaa, tumekuja kutoa elimu ya mpigakura kwani suala la
elimu tunalipa kipaumbele” Amesema Bw. Kailima.
Amesema
Tume imeandaa programu ya kuwafikia wapiga kura moja kwa moja kwa
kuweka mkakati wa kuhudhuria mikutano yote ambayo iko kihalali
ikijumuisha ile ya Mawaziri na Naibu Mawaziri , Makatibu Wakuu na Naibu
Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya.
Amebainisha
kuwa tayari NEC imewasiliana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili iweze kupata ratiba ya vikao vya kamati
za ushauri za mikoa na wilaya ili iweze kupata fursa ya kutoa elimu ya
mpiga kura ndani ya vikao hivyo.
Aidha,
amefafanua kuwa Tume imemwomba Katibu Mkuu TAMISEMI ratiba ya vikao vya
Mabaraza ya madiwani ya halmashauri zote nchini kwa lengo la kuwezesha
wataalam wa Tume hiyo kutoa elimu ya Mpiga kura.
“Tumemwomba
Katibu Mkuu TAMISEMI atusaidie kuweka ajenda ya kudumu kuhusu utaratibu
mzima wa uendeshaji wa uchaguzi na uelimishaji wa mpiga kura kwenye
vikao vya mabaraza ya Madiwani ambapo maafisa wa Tume walio katika ngazi
za halmashauri watapata fursa ya kutoa elimu ya mpiga kura katika vikao
hivyo” Amesisitiza.
Ameeleza
kuwa NEC imejipanga kupanua wigo wa utoaji wa habari kupitia vyombo vya
habari hasa Televisheni,Redio, Magazeti na Mitandao ya kijamii ili
kuwawezesha wananchi wengi kupata elimu ya mpiga kura na taarifa
sahihi kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi na majukumu yake.
“Tumejipanga
kutumia vyombo vya habari, kila wiki tutakuwa na taarifa na mada
fupifupi zinazohusu mchakato mzima wa uchaguzi kwa maana ya uandikishaji
na zoezi zima la upigaji kura kujenga uelewa kwa jamii nzima kuhusu
Tume ya Taifa ya Uchaguzi” Amefafanua.
Amesema
kuwa kifungu Na 4 (c) cha Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985 kinaelezea
wazi kuwa pamoja na mambo mengine Tume ya Taifa ya Uchaguzi ina jukumu
kutoa elimu ya Mpiga kura, kuratibu Taasisi na watu wenye uwezo wa
kutoa elimu ya mpiga kura ili kuongeza uelewa miongoni mwa jamii.
“Tunategemea
kuanzia mwanzoni mwa mwezi Oktoba tutatoa tangazo la kuzialika Asasi na
taasisi zinazotaka kutoa elimu ya mpiga kura ziwasilishe maombi yao
Tume ya Uchaguzi pamoja na zana zao za kutolea elimu ili tuweze
kuwapatia kibali cha miezi 6 na baadaye tutafanya tathmini juu ya
ufanisi wa kazi wanayoifanya” Amebainisha Bw. Kailima.
Amesema
lengo la kuzishirikisha taasisi na Asasi hizo ni kuondoa ombwe
lililokuwa linaonekana la utoaji wa elimu ya mpiga kura wakati wa
uchaguzi pekee kwa kuhakikisha elimu hiyo inatolewa kila wakati ili
kuongeza uelewa wa wananchi katika chaguzi zijazo.
Aidha,
amesema NEC imeandaa mpango mpya wa kuzifikia shule mbalimbali za
Sekondari hapa nchini utakaowawezesha wanafunzi wa shule
zitakazochaguliwa kuwa na Klabu za elimu ya mpiga kura.
Amesema
programu hiyo itaiwezesha Tume kuwaelimisha wanafunzi waliofikisha umri
wa kupiga kura na wale ambao bado hawajafikia umri huo ili kujenga
uelewa wao kuhusu elimu ya Mpiga kura.
“Tumeanza
program hii kwa kuzitembelea shule mbili za Sekondari za Isange
(wasichana) na Shule ya Ufundi Musoma zilizo katika Manispaa ya Musoma,
tutaongea na wanafunzi ambao wamefikia umri wa kupiga kura lakini bado
hawajajiandikisha kupiga kura na wale ambao bado hawajafikisha umri wa
kupiga kura, tumenalenga kuanzisha klabu ya Elimu ya mpiga kura kwenye
shule moja katika kila wilaya ya Tanzania” Amesema.
Amefafanua
kuwa kuanzishwa kwa klabu hizo kutawawezesha wanafunzi kujadiliana kwa
kina kuhusu mfumo wa uandikishaji wa wapiga kura kwa mujibu wa sheria
iliyopo ili kufikia lengo la kuwa na shule moja yenye Klabu ya elimu ya
mpiga kura katika kila wilaya ifikapo Januari 2020. (P.T)
SHARE
No comments:
Post a Comment