Jovina Bujulu- MAELEZO
Serikali
imewataka wachapishaji wote nchini waliojiandikisha kwa Msajili wa
Makampuni ( BRELA) na Mamlaka ya Mapato (TRA), kufika katika ofisi ya
Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali ili wajiorodheshe na watambuliwe na
Serikali na wananchi kabla ya Machi 30 mwaka huu.
Hayo
yamesemwa jijini Dar es salaam na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali ndugu
Cassian Chibogoyo alipokuwa akizungumzia kuwepo kwa wimbi kubwa la
wachapishaji hewa nchini.
Chibogoyo
amesema kuwa hatua hiyo inafuatia uwepo wa utitiri wa wachapishaji
ambao hawatambuliki na Serikali, kwa sababu baada ya kujiandikisha kwa
mamlaka husika kama kampuni, utawakuta wana mitambo ya uchapishaji
ambayo mara nyingi wanaitumia kuchapisha nyaraka bandia za Serikali bila
kuwa na kibali kutoka katika mamlaka yenye dhamana ya uchapishaji.
“Kwa
sasa tumeanzisha utaratibu maalum wa kuwatambua wachapishaji ambapo
wanatakiwa kujiorodhesha kwa Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali, hii ni
kutokana na kuwepo kwa uchapaji holela na bandia wa nyaraka za Serikali”
alisema Chibogoyo.
Aliongeza
kuwa chini ya utaratibu uliowekwa sasa wachapishaji wanatakiwa
kuwasilisha nyaraka halali za kampuni, shughuli wanazofanya, historia ya
kampuni na mahali kampuni inapofanyia kazi zake.
Adha,
Chibogoyo alisema kuwa faida za wachapishaji kujiandikisha ni pamoja na
kutambuliwa kisheria na Serikali ili hata wanaposhutumiwa waweze
kulindwa na Serikali, kukumbushana majukumu yao , wigo wao wa kazi, na
pia wataelimishwa kuhusu nyaraka wanazopashwa kuchapisha maana si kila
nyaraka wanapashwa kuzichapisha.
Zaidi
ya hayo, Chibogoyo alitaja madhara ya kuchapisha nyaraka bandia kuwa ni
pamoja na kuikosesha Serikali mapato kutokana na uchapishaji wa
stakabadhi mbalimbali bandia, uvamizi wa mawasiliano ya Serikali
uchapishaji wa vyeti vya usajili wa makampuni, na uchapishaji bandia wa
vyeti vya elimu ambavyo hupelekea mtu kuajiriwa kwa kazi ambayo hana
ujuzi nayo.
Akizungumzia
hatua ambao zinaweza kuchukuliwa dhidi ya wachapishaji wa nyaraka
bandia, Chibogoyo alisema kuwa ni pamoja na kutaifisha mitambo ya
wahusika.
Akizungumza
suala hilo hivi karibuni katika kipindi cha “Tujikumbushe”, Chibogoyo
alisema kuwa makosa ya uhalifu wa nyaraka bandia yanaangukia katika
sheria za ushahidi, sheria ya makosa ya jinai, sheria ya usalama wa
Taifa ya mwaka 1970, pamoja na sheria ya nembo na alama za Taifa.
Mpiga
Chapa huyo Mkuu wa Serikali alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na
Serikali kupambana na vita hii kwa kutoa taarifa katika kituo chochote
cha polisi ili kutokomeza janga hilo.
“Tunawaomba
wananchi tuwe na mshikamano katika kufichua janga hili la uchapishaji
holela na bandia kwani ni janga la kitaifa, linagusa maslahi ya nchi na
wananchi, nalifananisha na ujambazi wa hali ya juu” alisisitiza
Chibogoyo.
Baadhi
ya nyaraka ambazo zimekuwa zikighushiwa mara kwa mara ni pamoja na
vyeti vya elimu katika ngazi mbalimbali, risiti za serikali, vyeti vya
kuzaliwa na ndoa, kadi za magari na pikipiki, mihuri na nembo ya Taifa.
SHARE
No comments:
Post a Comment