TRA

TRA

Wednesday, May 31, 2017

DKT. NCHIMBI AAGIZA HALMASHAURI KUANZISHA BENKI ZA WANA MICHEZI NA KUTENGA VIWANJA VVYA MICHEZO MKOANI SINGIDA.

Share On Facebook ! Tweet This ! Share On Google Plus ! Pin It ! Share On Tumblr ! Share On Reddit ! Share On Linkedin ! Share On StumbleUpon !


Halmashauri zote saba za Mkoa wa Singida zimeagizwa kutenga maeneo yenye hadhi ya kuwa viwanja vya michezo pamoja na kuhakikisha zinakuwa na benki ya wanamichezo katika halmashauri zao.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi ametoa maagizo hayo leo asubuhi kabla ya kuzindua mashindano ya michezo kwa shule za Sekondari (UMISSETA) kwa ngazi ya mkoa ambapo wanamichezo hao wataunda timu za Mkoa kwa ajili ya mashindano ya kitaifa yatakayofanyika jijini Mwanza mwezi ujao.

Dkt. Nchimbi amesema halmashauri zimekuwa zikiwatelekeza wanamichezo mahiri hivyo wakianzisha benki ya wanamichezo kwa maana ya kuhifadhi kumbukumbu za wana michezo mahiri pamoja na kuwaendeleza hawatapata shida kipindi cha mashindano yoyote. 

Ameongeza kuwa halmashauri zimekuwa zikijisahau katika kuandaa maeneno ya michezo hadi inapofika kipindi cha UMISETA hali inayopelekea kukosekana kwa viwanja vya kufanyia mazoezi ili kuwa na timu bora.

Dkt. Nchimbi amewaasa wana michezo kuwa na nidhamu, utii, bidii na kuitumia michezo kuutangaza Mkoa wa Singida wenye fursa nyingi za uwekezaji pamoja na kujitangaza uwezo wao ili waweze kupata nafasi katika timu mbalimbali za kitaifa.

Aidha amewasisitiza waamuzi wa michezo kutenda haki kwakuwa matendo yao ni darasa la nidhamu na maadili kwa wanafunzi wao na kuwatahadharisha wanafunzi wasio tii kuwa hawatapata nafasi katika timu ya Mkoa.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt Angelina Mageni Lutambi amewapongeza wakurugenzi wa halmashauri kwa kufanikisha upatikanaji na ushiriki wa timu za michezo za kila halmashauri.

Dkt. Lutambi ameishukuru pia kampuni ya Coca cola kwa udhamini wa UMISSETA kwa kutoa vifaa kwa shule 118 ambavyo ni tisheti 3,776, mipira ya miguu 118 na mipira ya basketball 118 pamoja na ahadi ya kuendelea kugawa vifaa katika shule 45 zilizobaki.

Ameongeza kwa kuwasihi wana michezo wote kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu, kwa kuzingatia sheria na kanuni za michezo ili kutengeneza timu ya ushindi ya mkoa.

Akisoma taarifa ya Michezo ya Umiseta Afisa Michezo wa Mkoa Henry Kapella amesema jumla ya wana michezo 576 wameshiriki katika michezo hiyo ambapo wataunda timu ya mkoa ya michezo ya bao, riadha, mpira wa miguu na mpira wa pete. 

Kapella ameongeza kuwa kauli mbiu ya michezo ya Umisseta kwa mwaka 2017 ni ‘Wekeza katika michezo kwa ustawi wa elimu na Viwanda’. 

Kwa upande wao wanafunzi walioshiriki mashindano ya umisseta wamesema michezo inawajenga kiafya na kiakili kwa kuwa wanafunzi wanaoshiriki katika michezo huwa na ufaulu mzuri wa masomo yao.

Wameongeza kuwa michezo inawaongezea nidhamu na kuwajenga kimaadili hivyo kufaulu inakuwa ni rahisi, aidha wamesema michezo ina faida nyingi ikiwemo kuwatengenezea ajira mara baada ya kumaliza masomo yao.
 Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi (aliyenyanua ubao) akipiga ubao wa kuashiria uzinduzi wa michezo ya UMISSETA mkoa wa Singida, mbele yake ni wanariadha wakianza mashindano.
 Wanamichezo kutoka Shule za Sekondari za Halmashauri ya wilaya ya Itigi wakiimba wimbo wa taifa kabla ya kuanza mashindano ya UMISSETA ngazi ya Mkoa.
 Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi (katikati) akiimba wimbo wa taifa kabla ya kuanza mashindano ya UMISSETA ngazi ya Mkoa, kushoto kwake ni Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Mageni Lutambi na Kulia Kwake ni Afisa Elimu Mkoa wa Singida Florian Kimolo.
 Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akihutubia kabla ya kuzindua mashindano ya UMISSETA ngazi ya Mkoa wa Singida.
 Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Mageni Lutambi akizungumza katika uzinduzi wa mashindano ya UMISSETA Mkoa wa Singida.
Afisa Michezo wa Mkoa wa Singida Henry Kapella akisoma taarifa ya michezo ya Umisseta wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo ngazi ya Mkoa.

Author:

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment

 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger