Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar
Dkt. Abdalla Juma Saadala ” Mabodi” akizungumza na Mkurugenzi wa
taasisi ya kimarekani inayoshughulikia masuala ya Demokrasia duniani
(NDI), Dkt. Keith Jenningspamoja na ujumbe wake
……………………………………………………………..
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM
Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Sadala amefanya mazungumzo na Mkurugenzi
wa Taasisi ya kimarekani inayoshughulikia masuala ya Demokrasia Duniani
(NDI), kanda ya mashariki na kusini mwa afrika, Dkt. Keith Jennings,
huko Afisi kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo Naibu
Katibu Mkuu huyo alieleza kwamba CCM imekuwa mdau mkubwa wa kutekeleza
dhana ya demokrasia kwa vitendo, sambamba na kutoa fursa za uongozi kwa
makundi yote ya kijamii.
Alisema ujio wa taasisi hiyo
Zanzibar utafungua fursa mbali mbali kwa vijana na wanawake kupata ujuzi
wa kukabiliana na changamoto za kisiasa na kiuchumi.
Pia Dkt. Mabodi aliishauri
Taasisi hiyo kufungua Ofisi hapa nchini kwa lengo la kuratibu masuala
mbali mbali yakiwemo kuwapatia Vijana fursa za kimasomo nchini marekani
ili waweze kujifunza na kupata ujuzi wa fani zinazokubalika katika soko
la ajira hapa nchini.
“Vijana na Wanawake wa Zanzibar
wanakabiliwa na changamoto ya upungufu wa ajira, hivyo taasisi yenu
ikitoa fursa za mafunzo ya ujasiria mali itasaidia kukabili tatizo
hilo.”, alisema Dkt. Mabodi.
Naye Mkurugenzi wa taasisi ya
kimarekani inayoshughulikia masuala ya Demokrasia duniani (NDI), kanda
ya mashariki na kusini mwa afrika, Dkt. Keith Jennings alieleza kuwa
taasisi hiyo inajishughulisha na masuala ya Demokrasia na kutoa mafunzo
ya ujasiria mali kwa vijana na wanawake duniani.
Dkt. Keith alisema kuwa lengo la
ziara hiyo ni taasisi hiyo kujitambulisha kwa CCM Zanzibar na
kubadilishana mawazo yatakayosaidia kufanya kazi za kisiasa kwa pamoja.
” Taasisi yetu imekuwa ikitoa
mafunzo ya ujasiriamali pamoja na mbinu za kutumia fursa zinazopatikana
katika mifumo ya Kidemokrasia kwa vijana na wanawake, hivyo tunatarajia
hata kwa Zanzibar makundi hayo yatanufaika na mpango huo.”, alieleza
Dkt. Keith.
Dkt. Keith alisema Zanzibar ina
historia kubwa ya kisiasa hivyo taasisi hiyo ina dhamira ya kuwajengea
uwezo vijana mbali mbali hapa nchini ili waweze kutumia vizuri fursa
zilizopo katika michakato ya kidemokrasia.
SHARE
No comments:
Post a Comment