Julian Msacky
SWALI linaloulizwa sasa na wafuatiliaji wa siasa za Tanzania
kwa sasa ni je, nani ananufaika na mgogoro wa CUF?
Hili ni swali muhimu kwa sababu chama hicho kipo kwenye
mpasuko mkubwa wa kiuongozi na madaraka.
Mwenyekiti wa chama, Profesa Ibrahim Lipumba ana kundi lake
na Katibu mkuu, Maalim Seif Shariff Hamad vivyo hivyo.
Maalim Seif Sharif Hamad
Viongozi hao wawili kwa sasa ni sawa na mbingu na ardhi. Kila
mmoja anasema lake na kuacha wanachama njia panda.
Watu wanajiuliza kulikoni? Wengine wanasema viongozi hao
wamewekwa mfukoni ili waiue CUF kimya kimya.
Si hivyo tu bali wengine wanaeleza kuwa ruzuku ‘iliyozuiwa’
ndiyo inasababisha viongozi hao waparanganyike.
Kama hiyo haitoshi wadadisi wengine wa siasa wanadai Lipumba
amekuwa msaliti hivyo hawezi tena kuiongoza CUF.
Mambo hayo ndiyo yaliyosababisha chama kufikia hapo kilipo na
kusema kweli hivi sasa kinapitia kipindi kigumu.
Pamoja na hayo utashi wa kisiasa na kuvumiliana ukiendelea
kukosekana ipo hatari hali chama ikawa mbaya zaidi.
Hii ni kwa sababu tayari vurugu zimetokea na kusababisha
baadhi ya watu kujeruhiwa, wakiwemo waandishi.
Kimsingi hii si habari njema na wala haifurahishi wapenzi wa
mfumo wa vyama vingi vya siasa na demokrasia kwa ujumla.
Kwa msingi huo Prof Lipumba na Maalim Seif wanahitaji
kuonesha ukomavu wa kisiasa badala ya kuivuruga CUF.
Hii ina maana kuwa kama kuna dosari ya kiuongozi ni vizuri
wakae mezani na kuweka mambo yao sawa.
Tunasema hivi kwa sababu viongozi hao si muhimu kuliko chama.
Wao watapita na kuacha chama hapo kilipo.
Kwa sababu hiyo tofauti zao hazitakiwi kuendelea kupewa
nafasi kwani zitakuwa hazijengi zaidi ya kubomoa.
Mgogoro wa aina hiyo uliwahi kutokea kwenye vyama hivyo vya
siasa, kikiwemo Tanzania Labour Party (TLP).
Wote tunafahamu kilikofikia chama hicho achilia mbali vyama
vingine kama NCCR-Mageuzi ambacho kilikuwa tishio nchini.
Historia inaonesha adui mkubwa wa vyama vya upinzani ni
viongozi wenyewe kwani hunyukana wanachama wakiangalia.
Leo hii wanachama wa CUF wanaangalia Lipumba na Maalim Seif
wanavyoparuana, lakini athari zake ni nyingi.
Mojawapo ni kwamba viongozi hawana muda wa kujenga chama
zaidi ya kujadili migogoro isiyokwisha.
Leo utasikia mahakamani na kesho kwa Msajili wa vyama lakini
hutasikia ni lini wanakaa kujenga chama kiwe imara.
Mambo hayo na mengine yamefanya vyama vya siasa kuwa vya
msimu hivyo mchango wake kwa nchi kuwa mdogo.
Ndiyo maana wengine wanaviona kama maficho ya baadhi ya watu
kusukuma siku ziende na si kwa maslahi ya walio wengi.
Ni kwa sababu kama hizo ninashauri kuwa Lipumba na Maalim
Seif wakae meza moja ili kuleta utengamano ndani ya CUF.
Bila kufanya hivyo mbele kuna giza tororo. Wanachama waoneshe
mshikamano wa kweli badala kuburuzwa huku na kule.
Tunavyofahamu wanachama ndiyo uhai au mtaji wa chama. Wakiwa
imara chama kitapiga hatua. Wakilegea kitalegea.
Kwa mfano, maneno kama “mimi ndiye mwenyekiti” au “mimi ndiye
katibu” yana afya kwa chama au ni kutafuta ukuu?
Tulidhani kuwa Lipumba na Maalim Seif wangekuwa mwanga kwa
CUF kwani ni viongozi wa muda mrefu.
Hata hivyo, yanayoendelea ndani ya chama ile dhana kuwa “uzee
dawa” inaashiria kukosa mwenyewe.
Kwa hiyo kinachoendelea sasa ni viongozi kuoneshana umwamba
kwa gharama za wanachama na Watanzania kwa ujumla.
Njia hii mara nyingi haina tija zaidi ya kuvuruga mambo na
ushauri ni viongozi kujirekebisha ili kulinda hadhi yao.
Haitawapunguzia kitu kama watasuluhisha mgororo uliopo kwa
majadiliano kama anavyoshauri Msajili wa vyama nchini.
Ndivyo alivyosema Msajili wa Vyama Msaidizi, Sisty Nyahoza
kwa kukumbusha viongozi umuhimu wa kuheshimu maadili.
Alishauri viongozi hao kuacha kuendeleza mivutano isiyo na
tija kwani inawafanya wanachama kuingia kwenye mgongano.
Hilo lisipofanyika kambi ya Maalim Seif na Prof Lipumba
haitaacha CUF ikiwa salama zaidi ya kubaki vipande vipande.
Ni matarajio ya Watanzania wengi kwamba busara na hekima
itatumika zaidi ili CUF iendelee kuwa yenye mshikamano.
SHARE
No comments:
Post a Comment