Utawala bora, Anjela Kairuki
Said Mwishehe
KWA Ujinga Wangu nimekaaa na kujikuta nawaza mambo mengi yanayoendelea kwenye nchi yetu kwani yapo yanayofurahisha na yapo yanayochukiza.
Wakati naendelea kuwaza nikajikuta naijadili kimya kimya likizo ambayo amepewa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ambayo haieleweki itakwisha lini?
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphery Polepole amenukuliwa akisema Kinana yupo likizo ili kumpa nafasi ya kumpuzika baada ya kufanya kazi muda mrefu hivyo amechoka na wakati huo huo afya yake ilitetereka licha ya kwamba hivi sasa ipo sawa.
Wakati Polepole akielezea likizo hiyo ya Kinana yanayozungumzwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu Katibu Mkuu huyo yanatia hofu. Kama ni kweli yanayozungumzwa acha nikae kimya nisubiri tuone tunakoelekea.
Kwa Ujinga Wangu kuwaza kuhusu alipo Kinana yakaondoka ghafla nikaanza kuwaza mjadala unaohusu vyeti feki kwa watumishi wa umma ambao kwa sasa wametakiwa kuondoka kazini baada ya kubaini wamefoji vyeti vyao vya elimu.
Inatia huruma maana watumishi ambao wamekutwa na sakata hilo wengine wameitumikia nchi yetu kwa uadilifu wa hali ya juu na huenda miundombinu inayotumiwa sasa kwenye maeneo ya utumishi wa umma wameshiriki kuijenga.
Idadi ya watumishi wa umma ambao wamekutwa na tatizo la vyeti feki ni zaidi ya 9,000. Kimsingi ni watu wengi na wengine walibakisha muda mfupi kustaafu kazi ya utumishi. Leo hii wamepoteza mafao yao na haki nyingine za msingi.Inasikitisha.
Kwa Ujinga Wangu wiki iliyopita nilizungumzia hili hili la vyeti feki na kilichotokea kwa watumishi hao ambao leo hii wamebaki kama yatima maana hakuna wa kuwatetea, kisa tu sheria inasema anayefoji cheti cha elimu atafungwa jela miaka saba na kupoteza mafao yake.
Hata hivyo, lazima tukubali sheria hizo zilitungwa na Watanzania wenyewe, hivyo bado zinaweza kuangaliwa upya. Pia mbali ya kutumia sheria bado ipo nafasi ya kuamua mambo kwa kutanguliza busara, hekima na utu.
Kwa Ujinga Wangu upendo una nafasi yake kwa sababu sheria bila upendo wakati mwingine ni kazi bure.
Baadhi ya hao ambao wamekutwa na vyeti feki walikuwa ni wataalamu mahiri kwenye utumishi wao na hawajawahi kuleta athari kwenye utumishi wao.
Wengine ndiyo wamefanya kazi kubwa ya kupika watalaamu wa kada mbalimbali lakini leo hii wanaokosa haki zao kwa sababu tu cheti chake cha kidato cha nne hakikuwa cha kwake au alifoji cheti cha elimu yake.
Kwa Ujinga Wangu nilidhani utaalamu ni jambo la msingi zaidi kuliko cheti cha kidato cha nne. Tujiulize tu kwani cheti cha kidato cha nne kinatusaidia kwenye nini katika utendaji wetu wa kila siku.
Hivi mtumishi wa umma ambaye ni dereva wa mkurugenzi wa idara au taasisi ya umma kwake cheti cha kidato cha nne kina faida gani kwake?
Maana kazi yake ni kuendesha gari na anaifanya vema zaidi anachohitaji ni cheti cha mafunzo ya udereva na leseni ya kuendesha gari.
Wiki iliyopita nilisema tatizo la nchi yetu kuna wakati vilitangulizwa vyeti vya elimu zaidi ili kupata ajira serikalini.
Nakumbuka serikali iliwahi kutoa waraka uliokuwa unaelekeza kuwa watumishi wawe na elimu ya sekondari na hivyo iliamua kutoa muda kwa watumishi wasio na elimu hiyo kusoma na ndipo uliibuka utaratibu wa elimu ya sekondari kwa miaka miwili.
Hata hivyo, ni jambo la kujiuliza tu hivi dakatri ambaye ni mtalaamu wa magonjwa ya akina mama na kazi yake anaweza vizuri cheti cha elimu ya kidato cha nne ina faida gani zaidi ya utalaamu wake ambao ndiyo unatija kwetu?
Kwa Ujinga Wangu naomba ifahamike kuwa naamini kwenye kufanya kazi zaidi kuliko kuamini kwenye vyeti na huo ndio ukweli.Wale wenye elimu ndogo au wasio soma wamekuwa wafanyakazi wazuri kuliko wale ambao wanajivunia kwa kuwa na vyeti vyenye alama ya A darasani lakini kwenye utendaji kazi sifuri.
Nikiri binafsi naunga mkono jitihada ambazo Serikali inafanya katika kuweka misingi sahihi ya ufanyaji kazi katika utumishi wa umma. Lazima taratibu zilizopo kwa mujibu wa sheria na kanuni zifuatwe na kila mmoja wetu.
Kwa Ujinga Wangu najiuliza nini kilisababisha watumishi hao kufoji vyeti vya elimu? Naamini jibu ni kwamba serikalini walitanguliza cheti kuliko uwezo wa mtu kufanya kazi.
Yaani hata mwenye nguvu zake za kuchimba mashimo ya choo au kuchimba msingi kwa ajili ya kujenga majengo ya umma kwenye halmashauri fulani lazima awe na elimu ya kidato cha nne na si nguvu zake.
Wakati naendelea kutafakari kuhusu idadi kubwa ya watumishi kuondolewa kwenye utumishi kwasababu ya kufoji vyeti nikakumbuka Rais John Magufuli alikakariwa kwenye moja ya hotuba zake kuwa katika uongozi wake hataki kufukua makaburi na kwa Kwa Ujinga Wangu nadhani alikuwa anamaanisha hatahangaika na mambo yaliyofanywa na awamu zilizotangulia na badale yake hatakubali kuona mambo yakienda kombo kwenye utawala wake.
Kwa Ujinga Wangu kauli hiyo ilionesha anatembea kwenye nyayo za viongozi wengine ambao hawakuhangaika kufukua makaburi na nakumbuka Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili Alhaj Ali Hassan Mwinyi aliwahi kusema kila kitabu na zama zake.
Kwa hiyo kauli ya Rais Magufuli na mzee Mwinyi zina mafundisho mengi katika suala zima la uongozi ili kuhakikisha viongozi wanaongoza kwa kufuata taratibu za kisheria lakini zaidi zile ambazo zilizoasisiwa na Mwalimu Julius Nyerere kwani tunaamini mifumo mingi aliyoweka bado ni hai au inaishi na hakuna ambacho kimeharibika.
Kwa Ujinga Wangu kwenda tofauti na yale ambayo Mwalimu Nyerere aliyaamini kama ndio msingi wa nchi yetu kupiga hatua tunaweza kujikuta kwenye matatizo makubwa ambayo wakati mwingine si rahisi kuyaona sasa labda baadaye.
Mwalimu Nyerere aliamini kwenye utendaji zaidi na uwezo wa mtu katika kufanya kazi.
Ndiyo maana enzi za utawala baada ya kuona kuna tatizo la uhaba wa walimu aliamua kuanzisha utaratibu wa kuwa walimuwa UPE ambao kazi yao ilikuwa kufundisha wanafunzi.
Kwa mfano aliyeishia darasa la nne alipata nafasi ya kuwa mwalimu wa kufundisha wanafunzi wa dasara la kwanza au la pili.
Kwa ule aliangalia zaidi mahitaji na si cheti cha mtu anayedhani anaweza kufundisha wengine kwa kiwango cha elimu aliyonayo.Watanzania wengi wakajua kusoma na kuandika kupitia UPE.
Kwa Ujinga Wangu natambua kama nchi tumepita hatua tofauti na hatuwezi kuzibeza maana zilikuwa zinatuondoa kwenye hatua moja na kwenda nyingine.
Hata hivyo, lazima tuwe na mfumo rasmi kama nchi ambao utatuwezesha kusimama imara kwa siku zijazo bila kuharibu maisha ya wengine.
Fikiria mtumishi wa umma ambaye amefanya kazi tangu utawala wa awamu ya pili chini ya mzee Mwinyi hadi awamu ya tano halafu anaambiwa hawezi kupata mafao yake kwa sababu tu amebainika alifoji cheti cha elimu ya sekondari.
Inauma na inasikitisha. Tena wengine ambao wao wanaondolewa kwa sababu tu ya matatizo ya vyeti vyao lakini wakiwa kwenye utumishi walitumia fedha ndogo wanayopata kusomesha watoto wao hadi kufikia chuo kikuu.
Binafsi naamini pamoja na masuala ya sheria lakini watumishi hao bado wanastahili kulipwa mafao japo kidogo, wengi wao ni watu wenye uwezo mdogo kifedha na waliamini mafao yao baada ya kustaafu wanaweza kuandaa maisha yenye unafuu lakini mwisho wa siku wanaondoka patupu. Kweli?
Kwa Ujinga Wangu nilitamani watumishi hao baada ya kubaini vyeti vyao vya elimu vina matatizo wapewe nafasi ya kurudi shule huku wakiendelea na utumishi wa umma lakini njia nyingine ilikuwa ni kufanya uhakiki na kisha kutambua ukubwa wa tatizo na baada ya hapo unawekwa mfumo maalum ambao utahakikisha kuanzia sasa kila anayeingia kwenye ajira ya umma awe na vyeti vilivyotimia.
Kwa kufanya hivyo tusingeathiri maisha ya Watanzania wenzetu ambao wametumia muda wao mwingi kwa ajili ya kuijenga nchi yetu. Natambua dhamira njema ya Serikali yetu lakini ni vema ikaenda sambamba na huruma.
Nisengekuwa sina tatizo kama watumishi waliofukuzwa wangekuwa si raia wa Tanzania lakini waliamua kufoji vyeti vya elimu ili kupata ajira ndani ya serikali yetu. Chukua mfano mtumishi wa umma ambaye amekuwa kwenye utumishi wa umma kwa miaka 35.
Na amefanya kazi yake vizuri na wakati mwingine amepata tuzo za mfanyakazi bora leo anaambiwa hawezi kupata mafao yake, kisa tu alifoji cheti cha kidato cha nne au sita.
Ni kweli uamuzi umetolewa lakini bado nafasi ipo ya kuwaangalia upya namna ya kufanya angalau wanufaike na jasho lao ambalo walilitumia kwenye utumishi.
Najua kuna maeneo ambayo sheria lazima isimame ili mambo yaende sawa lakini kwenye hili la watumishi ipo haja ya kutafakari upya. Hata hivyo, huu ni Ujinga Wangu.
Tuwasiliane
0713 833822
SHARE
No comments:
Post a Comment