TRA

TRA

Sunday, May 14, 2017

Wa-Baha’i Ulimwenguni Kote Washerehekea Siku ya Tangazo la Bab

Share On Facebook ! Tweet This ! Share On Google Plus ! Pin It ! Share On Tumblr ! Share On Reddit ! Share On Linkedin ! Share On StumbleUpon !

Jioni ya tarehe Mei 22, 1844, Bab, neno ambalo maana yake kwa lugha ya Kiarabu ni “Lango”, alitangaza kuwa Yeye ndiye Mjumbe mpya kutoka kwa Mungu.


Yeye alikuja kuwaandaa wanadamu kwa ajili ya ujio wa Ufunuo wa Mungu kwa ajili ya ulimwengu, ambao umesubiriwa kwa hamu sana, ambao ungeletwa na Mjumbe mwingine. 

Mjumbe huyo alikuwa Baha’u’llah, Mtume Mwanzilishi wa Imani ya Baha’i, Ambaye angeleta zama mpya za amani na haki kama ilivyokuwa imeahidiwa katika dini zote zilizotangulia. Wafuasi wa Baha’u’llah wanajulikana kama Wa-Baha’i.

Jumuiya ya Wa-Baha’i wa Dar es Salaam wataunganika na jumuiya nyingine za ulimwenguni kote kwa ajili ya kusherehekea Tangazo la Bab, siku ya Jumatatu  tarehe Mei 22, 2017. 

Siku hiyo Wa-Baha’i kote ulimwenguni pia watasherehekea  mwaka wa  174 tangu kuzaliwa kwa Imani ya Baha’i. 

Miezi michache baada ya kutangaza ujumbe Wake, mnamo tarehe Mei 22, 1844, Bab alikamatwa, kupigwa na kufungwa. 


Hatimaye, mnamo tarehe Julai 9, 1850, Yeye Aliuawa hadharani katika uwanja wa mji wa Tabriz, Persia. Wafuasi Wake takriban 20,000 waliuawa katika mlolongo wa mashambulizi kila mahali nchini Persia. Kaburi Lake liko juu ya Mlima Karmeli huko Haifa, Israel.

Bab Alimtaja Baha’u’llah kama “Yule Ambaye Mungu Atamdhihirisha” na Alisema, “Sina maneno ya kuweza kueleza kwa kutosheleza jinsi Alivyo Yeye… ama kuifanyia haki Hoja Yake.” 


Ujumbe mkuu wa Imani ya Baha’i, kama ilivyotangazwa na Baha’u’llah, ni umoja wa mbari wa wanadamu. Wa-Baha’i huamini kuwa Wadhihirishaji wote wa Mungu: Abraham, Krishna, Moses, Zoroasta, Buddha, Yesu, Muhammad, Bab na Baha'u'llah ni "Waelimishaji Watukufu".

Tangazo la Bab ni mojawapo ya siku Takatifu tisa ambamo Wa-Baha’i hawapaswi kwenda kazini ama shuleni.

Jumuiya ya Wa-Bahá’í wa Dar es Salaam wanawaalikeni nyote kwa moyo mkunjufu kuungana nao kusherehekea tukio hili lenye furaha. Ratiba itaanza na ibada fupi, usomaji wa maandiko matakatifu program na kufuatwa na burudani ya nyimbo, maongezi na maakuli. 


Sherehe itafanyika katika Bahá’í Senta Mtaa wa Mfaume, Upanga, saa 12:00 jioni siku ya Jumatatu tarehe, Mei 22, 2017.

Author:

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment

 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger