Katibu
Ofisi ya Rais Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Nyakimura Muhoji akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu majukumu
mbalimbali yaliyotekelezwa na Tume hiyo katika mwaka wa fedha 2016/17
kwa ajili ya kuboresha utendaji katika utumishi wa umma. Kushoto ni
Katibu Msaidizi wa Tume hiyo Bw. Peleleja Masesa.
Katibu
Msaidizi Idara ya Afya kutoka Ofisi ya Rais Tume ya Utumishi wa Umma
Bw. Peleleja Masesa akifafanua kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es
Salaam kuhusu Sheria ya Utumishi wa Umma Na.8 inayoelezea majukumu ya
Tume hiyo. Kulia ni Katibu Msaidizi Idara ya Utumishi Serikalini kutoka
Tume hiyo Bw. John Mbisso.
Katibu
Msaidizi Idara ya Utumishi Serikalini kutoka Ofisi ya RaisTume ya
Utumishi wa Umma Bw. John Mbisso akizungumza na waandishi wa habari
kuhusu taratibu za kupokea na kushughulikia rufaa za watumishi wa umma
katika Tume hiyo. Kulia ni Katibu Msaidizi wa Tume hiyo Bw. Peleleja
Masesa.(PICHA ZOTE NA FATMA SALUM- MAELEZO)
Na Fatma Salum (MAELEZO)
Serikali
imewataka Waajiri na Mamlaka za Ajira na Nidhamu kote nchini kuzingatia
Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayosimamia Utumishi wa Umma ili
kuleta ufanisi katika usimamizi na uendeshaji wa masuala ya Rasilimali
Watu kwenye Utumishi wa Umma.
Kauli
hiyo imetolewa na Katibu Ofisi ya Rais Tume ya Utumishi wa Umma
Bw.Nyakimura Muhoji wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar
es Salaam leo.
Muhoji
alisema kuwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Tume hiyo imefanya ukaguzi wa
Rasilimali Watu katika Taasisi 41 na kubaini kwamba kuna baadhi ya
Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu hazitekelezi ipasavyo majukumu yao
hususan katika usimamizi wa masuala ya ajira na nidhamu hivyo kupunguza
ufanisi katika utendaji kazi.
“Ukaguzi
wa Rasilimali Watu umefanyika katika Taasisi 41 ambazo ni Sekretariet
za Mikoa mitano ikiwemo Morogoro, Iringa, Mbeya, Arusha na Mwanza,
Mamlaka za Serikali za Mitaa 30 zilizopo kwenye mikoa hiyo pamoja na
Wakala na Taasisi 6 kwa lengo la kuangalia ni kiasi gani Waajiri na
Mamlaka za Ajira na Nidhamu wanafanya kazi kwa kuzingatia Sheria,
Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma.” alieleza Muhoji.
Naye
Katibu Msaidizi Idara ya Afya kutoka Tume hiyo Bw. Peleleja Masesa
alisema kuwa hali ya uwasilishaji wa taarifa zinazohusu usimamizi wa
Rasilimali Watu hairidhishi kwa kuwa zipo baadhi ya Taasisi za Umma
hazitekelezi jukumu hilo la kisheria.
“Nasisitiza
kuwa uwasilishaji wa taarifa kwa Tume ni jukumu la kisheria hivyo
Waajiri na Mamlaka za Ajira na Nidhamu ambao hawajawasilisha taarifa
hizo wanakumbushwa kuziwasilisha kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa.”
alisisitiza Masesa.
Aidha
Masesa alieleza kuwa Tume hiyo pia ina jukumu la kupokea na
kushughulikia Rufaa na malalamiko yanayohusu masuala ya kiutumishi
kutoka kwa Watumishi wa Umma ambao hawakuridhika na jinsi masuala yao ya
kiutumishi yalivyoshughulikiwa na mamlaka zao.
Pia
alitoa wito kwa Watumishi wa Umma na Watendaji wote kutekeleza majukumu
yao kwa kuzingatia sheria, maadili ya Utumishi wa Umma na taaluma zao
ili Utumishi wa Umma ukidhi matarajio ya wananchi.
SHARE
No comments:
Post a Comment