Benny Mwaipaja, WFM
Serikali imesema inaendelea
kupitia sheria, kanuni na taratibu za misamaha ya kodi mwaka hadi mwaka
ili kuhakikisha kuwa misamaha yote isiyokuwa na tija inafutwa na hivyo
kuiwezesha Serikali kuongeza mapato kwa ajili ya kupeleka huduma za
maendeleo kwa wananchi wake.
Kauli hiyo imetolewa Bungeni Mjini
Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji
(Mb), alipokuwa akijibu swali la Msingi la Mbunge wa Masasi, Mhe. Rashid
Mohamed Chuachua (CCM), aliyetaka kujua namna Serikali inavyodhibiti
misamaha ya kodi tangu irekodiwe kwa viwango vya juu Mwaka wa Fedha
2011/2012.
Mhe. Chuwachuwa alihoji mwenendo
wa utoaji wa misamaha ya kodi kwa wawekezaji kwa maelezo kuwa Tanzania
imekuwa miongoni mwa nchi zilizopoteza fedha nyingi kwa ajili ya
misamaha ya kodi ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki
kwa kigezo cha kuvutia Wawekezaji.
Alisema kuwa kwa mujibu taarifa ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2009-2010,
Tanzania ilipoteza asilimia 15 ya Pato la Taifa lililotarajiwa
kukusanywa kutokana na misamaha ya kodi, mwaka 2010-2011 asilimia 8, kwa
mwaka 2011-2012 asilimia 27 ya mapato ya Serikali yalipotea.
“Je hali ya misamaha ya kodi kuanzia 2013-2014 hadi sasa ikoje’’. Alihoji Mhe. Chuachua.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa
Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), misamaha ya kodi kama
sehemu ya asilimia ya Pato la Taifa katika kipindi cha kuanzia mwaka
2013/14 hadi sasa imekuwa ikipungua mwaka hadi mwaka.
“Misamaha hiyo ilikuwa asilimia
2.2 ya Pato la Taifa mwaka 2013/14, asilimia 1.9 ya Pato la Taifa katika
mwaka 2014/15 na asilimia 1.1 ya Pato la Taifa katika mwaka 2015/16”
Alifafanua Dkt. Kijaji.
Aidha aliongeza kuwa misamaha ya
kodi ikilinganishwa na mapato ya kodi imekuwa ikipungua kutoka asilimia
18 ya mwaka 2013-2014 hadi kufikia asilimia 8.6 ya mapato yote ya kodi
katika mwaka 2015-2016.
Dkt. Kijaji alifafanua kuwa
misamaha ya kodi inatolewa na Serikali kwa mujibu wa sheria, kanuni na
taratibu za kodi zilizopo, huku kukiwa na baadhi ya huduma zinazotolewa
katika jamii ambazo hazistahili kulipiwa kodi kwa sababu hazina manufaa
ya kibiashara.
‘’Pamoja na hatua nzuri
zinazochukuliwa na Serikali za kupunguza misamaha ya kodi ni vema
ikafahamika kwamba si kila msamaha wa kodi una madhara hasi katika jamii
na uchumi kwa ujumla’’. Alisema Dkt. Kijaji.
Alitolea mfano wa mashirika ya
dini yanayopata misamaha ya kodi kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT) (2014), kwa sababu huduma zinazotolewa na
taasisi hizo hazina faida ya kibiashara kama ilivyo kwa kampuni za
kibiashara.
Katika swali la nyongeza Mbunge huyo, alitaka kujua mpango wa Serikali kuhusu misamaha ya kodi kwa mwaka wa fedha 2017-2018.
Akijibu swali hilo la nyongeza
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Kijaji, alimuomba Mhe.
Chuachua awe na subira hadi tarehe 8 mwezi huu ambapo Serikali itapeleka
mapendekezo yote katika Bunge, ili mapendekezo hayo yaweze kujadiliwa
na kupitishwa na Bunge.
SHARE
No comments:
Post a Comment