Mkurugenzi
Msaidizi, Ukaguzi, Maadili na Malalamiko, Mhe. Happiness Ndesamburo
akionesha Mkataba wa kazi aliokabidhiwa kwa ajili ya utekelezaji.
Katikati ni Mtendaji Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Hussein Kattanga, na
kulia ni Msajili Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revokati.
Mtendaji
Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Hussein Kattanga akitoa taarifa kuhusu
utendaji kazi wa Mahakaam ya Tanzania kwa Waziri wa Katiba na Sheria
Prof. Palamagamba Kabudi (aliyekaa mbele kushoto) alipotembelea Mhimili
huo hivi karibuni.
Mtendaji
Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Hussein Kattanga (katikati)
akimkabidhi Mkataba wa kazi Msajili-Mahakama ya Rufani, Mhe. John
Kahyoza (kushoto), anayeshuhudia ni Msajili Mkuu, Mahakama ya Tanzania,
Mhe. Katarina Revokati.
NA LYDIA CHURI- MAHAKAMA
Mahakama
ya Tanzania imepanga kutoa huduma bora ili kuhakikisha wananchi
wanapata haki zao za msingi kwa wakati. Mpango huo wa kutoa huduma bora
kwa wananchi unatekelezwa kupitia Mpango Mkakati wake wa miaka mitano
unaotekelezwa katika kipindi cha 2015/16-2019/20.
Mpango
Mkakati huu ni dira na mwelekeo wa Mahakama katika kufikia lengo lake
la kuwa Mahakama iliyo karibu na inayofikiwa na wananchi katika kutoa
huduma bora za utoaji wa haki. Aidha, Mpango Mkakati huu unalenga
kufikia malengo ya dira ya maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2025 ya
kuifikisha nchi kwenye uchumi wa kati.
Mpango
huu umejikita katika nguzo tatu ambazo ni Utawala bora, uwajibikaji na
usimamizi wa rasilimali, Upatikanaji wa Haki kwa wakati pamoja na
uimarishaji wa Imani ya wananchi kwa Mahakama pamoja na ushirikishwaji
wa wadau katika shughuli za Mahakama.
Katika
nguzo ya kwanza ya Mpango Mkakati huu, Mahakama imeanzisha vikao maalum
vya kutathmini kazi ya uendeshaji wa mashauri na kazi za mahakama kwa
ngazi za Mahakama ya Rufani, Majaji wafawidhi wa kanda za Mahakama Kuu
pamoja na kamati tano za kumshauri jaji Mkuu za kanuni, Mafunzo, Tehama,
ufuatiliaji na Maboresho. Aidha Mahakama pia inasimamia suala zima la
utendaji kazi kwa malengo kwa kada zote ndani ya Mhimili huo.
Matumizi ya TEHAMA ndani ya Mahakama
Akiwasilisha
Taarifa ya utendaji kazi wa Mahakama ya Tanzania kwa Waziri wa Katiba
na Sheria hivi karibuni, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Hussein
Kattanga alisema Mahakama imeanza matumizi ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA) ili kurahisisha utendaji kazi wake pamoja na
kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia. Mahakama tayari
imeanzisha mfumo wa ukusanyaji wa takwimu za mashauri kwa njia ya
kielekitroniki kuanzia ngazi ya Mahakama za wilaya, Mkoa, kanda na
Taifa. Mbali na mfumo huu, hadi kufikia mwisho wa mwaka huu wa fedha
2017/2018, Mahakama itakuwa imeanza kutumia mitandao kwenye uendeshaji
wa kesi. Aidha, Mahakama iko kwenye mpango wa kuweka kwenye mtandao na
kuingiza mkongo wa taifa kwa Mahakama zote za wilaya, Hakimu Mkazi/Mkoa,
Mahakama Kuu na Makao Makuu jijini Dar es salaam. Tayari majengo ya
Mahakama Kuu Mbeya na lile la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha
yameshawekewa.
Ili
kutekeleza nguzo ya pili ya Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama
ya Tanzania, mhimili wa Mahakama unapitia upya taratibu, kanuni na
sheria zinazokwamisha na kuchelewesha kesi mahakamani na zile zilizopo
nje ya mahakama na kushauri ipasavyo. Mpango huu umesaidia kupunguza
kesi za madai kutoka 38 na kufikia mpaka 21.
Aidha,
Mtendaji Mkuu alisema Mahakama pia imeandaa program na mazoezi endelevu
katika ngazi zote za mahakama za kuondosha na kuzuia mashauri ya zamani
na kuimarisha menejimenti ya mashauri, kuyajua, na kuyachambua majalada
pamoja na kufanya vikao vya awali na wadau wote baada ya mazoezi na
usikilizaji wa mashauri. Mahakama pia itaimarisha upatikanaji wa nakala
za hukumu na mienendo ya kesi zikiwemo njia za kupeleka kwa wateja kwa
njia ya posta na njia nyingine za kielektroniki.
Mpango waMiaka Mitano wa Maendeleo ya Miundombinu ya Mahakama
Katika
kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi, Kattanga alisema Mahakama
inao mpango wa miaka mitano wa Maendeleo ya Miundombinu ya Mahakama
kuanzia mwaka 2015/2016 hadi 2019/2010 ambapo matarajio ya mpango huu ni
kujenga jengo moja la Mahakama ya Rufani, majengo 30 ya Mahakama Kuu,
majengo 24 ya Mahakama za Hakimu Mkazi, majengo 109 ya Mahakama za
Wilaya na majengo 150 ya Mahakama za Mwanzo.
Hata
hivyo, bado kutakuwa na upungufu mkubwa wa Mahakama za Mwanzo kwa kuwa
kuna kata zaidi ya 3000 na Mahakama za Mwanzo zilizopo ni 960. Lengo ni
kuwa na Mahakama ya Mwanzo kwenye kila kata. Aidha, kati ya mikoa 26 ya
Tanzania bara, ni mikoa 14 tu ndiyo yenye Mahakama Kuu. Baadhi ya mikoa,
wananchi wake wamekuwa wakilazimika kufuata huduma za Mahakama Kuu
kwenye mikoa mingine, kwa mfano, wananchi wa mkoa wa Singida hawana budi
kupata huduma hizo katika mkoa wa Dodoma ambapo ndipo yalipo makao
makuu ya kanda ya Dodoma. Wananchi wa Kigoma pia wamekuwa wakifuata
huduma hizo katika mkoa wa Tabora ambapo ndiyo makao makuu ya kanda ya
Mahakama Kuu Tabora.
Mikoa
yenye Mahakama Kuu ni Dar es salaam, Dodoma, Mwanza, Arusha, Moshi,
Tanga, na Bukoba (Kagera). Mikoa mingine ni pamoja na Iringa, na Songea
(Ruvuma). Mikoa mingine niTabora, Mbeya, Sumbawanga (Rukwa), Mtwara na
Shinyanga.
Hivi
sasa Mahakama ya Tanzania inajenga majengo sita ya mfano katika utafiti
wa Teknolojia ya gharama nafuu na ya muda mfupi iitwayo Moladi katika
maeneo ya Kigamboni, Mkuranga, Bagamoyo, Kinyerezi, Kawe pamoja na jengo
la Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Pwani na Mahakama ya wilaya ya
Kibaha ambalo limekamilika na kuzinduliwa rasmi mwaka jana na Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa na tayari
limeanza kutumika.
Mahakama yaboresha Huduma kwa Majaji wake
Pamoja
na kusogeza huduma kwa wananchi, Mahakama pia imekuwa ikiboresha
mazingira ya kazi kwa Majaji wote nchini. Majaji 65 waliopo Mahakama kuu
ya Tanzania wamepatiwa ofisi zenye nafasi ya kutosha ili kuwawezesha
kufanya kazi zao za utoaji wa haki kwa ufasaha ili kesi ziweze
kumalizika kwa wakati. Kuna jumla ya vyumba 91 vilivyotengwa na kutumika
kama ofisi za Majaji kwenye Mahakama kuu zote nchini.
Kutokana
na idadi ya Majaji waliopo nchini, mahitaji ya Majaji bado ni makubwa
ili kufanikisha azma ya Mahakama ya kutokuwa na mlundikano wa kesi
kwenye mahakama mbalimbali nchini. Tathmini ya Mahakama iliyofanyika
mwishoni mwaka 2016, Mahakama Kuu na Divisheni zake imekuwa na mzigo wa
Mashauri 35,878 kwa idadi ya wastani wa Majaji 75 waliokuwepo kipindi
cha mwaka 2016. Kwa mantiki hiyo, kila Jaji alikuwa na mzigo wa wastani
wa mashauri 478.Aidha, uwezo wa Jaji mmoja kusikiliza kesi unakomea
kwenye kesi 198 kwa mwaka, hivi.
Pamoja
na kufahamu idadi ya Majaji waliopo nchini, ni muhimu pia wananchi
wakafahamu mchakato mzima unaowezesha Majaji kupatikana. Majaji wa
Mahakama Kuu ya Tanzania huteuliwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kama ambavyo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inampa
Mamlaka hayo katika uteuzi wa watoa haki hao.
Uteuzi wa Majaji
Kwa
mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 109 (6)
mtu anaweza kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano waTanzania kuwa
Jaji kama atakuwa na sifa maalum ambazo zimeelezwa katika ibara ndogo ya
7 na awe amekuwa na sifa hizo kwa muda usiopungua miaka 10.
Sifa
hizo maalum ni kuwa na digrii ya kwanza ya Sheria kutoka katika chuo
kikuu kinachotambulika na mamlaka za utambuzi pamoja na;
- Kuwa hakimu;
- Ameshika nafasi katika ofisi yoyote ya Umma akiwa kama Mwanasheria au Wakili wa kujitegemea na
- Awe na sifa ya kuweza kusajiliwa kama Wakili kwa kipindi cha miaka isiyopungua kumi.
Kwa
mujibu wa Ibara hii, siyo Mahakimu peke yao wenye sifa ya kuteuliwa
kuwa jaji wa mahakama Kuu. Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayo
mamlaka ya kuteua mtu mwenye sifa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania
hata kama anatoka nje ya mhimili wa Mahakama.
yo basi Majaji waliopo ni wachache na kuna ofisi 24 zipo wazi hazina Majaji.
Mafanikio katika Usikilizwaji wa Mashauri ya Zamani (Backlog)
Kwa
Mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, hadi kufikia Desemba
mwaka 2016, mlundikano wa mashauri kwenye mahakama mbalimbali nchini
ulishuka kutoka wastani wa asilimia 46mwaka 2013 na kufikia wastani wa
asilimia 21 kwenye mahakama ya Rufani na kutoka wastani wa asilimia 33
mwaka 2013 na kufikia wastani wa asilimia 9 kwenye Mahakama Kuu ya
Tanzania. Katika Mahakama za Hakimu Mkazi/Mkoa, idadi ya mlundikano wa
mashauri ya zamani ilipungua na kufikia wastani wa asilimia 3 kutoka
wastani wa asilimia 9 mwaka 2013. Aidha kwenye Mahakama za wilaya
mlundikano wa mashauri ulishuka kutoka wastani wa asilimia 9 mwaka 2013
na kufikia wastani wa asilimia 3 mwaka 2016 wakati kwenye Mahakama za
Mwanzomlundikano ulishuka kutoka wastani wa asilimia 2 mwaka 2013 hadi
kufikia kesi 0 au kutokuwa na mashauri hayo kabisa hivi sasa.
Mahakama
ya Tanzania haina budi kujivunia mafanikio haya makubwa hasa kwa
Mahakama za chini ambako asilimia 80 ya kesi zinazofunguliwa na wananchi
zipo kwenye ngazi hizo. Mahakama pia imefanikiwa kupunguza mlundikano
wa mashauri yenye zaidi ya miaka miwili kutoka mashauri 10,832 yaani
sawa na asilimia 10 mwaka 2012 hadi kufikia mashauri 2,702 sawa na
asilimia (5%) tano mwaka 2016.
Watanzania
pamoja na wadau wengine wa Mahakama wakiwemo Jeshi la Polisi, Magereza,
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa-TAKUKURU, Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwendesha Mashitaka wa Serikali,pamoja na
Mkemia Mkuu wa Serikalihawana budi kushirikiana na Mahakama ya Tanzania
bega kwa bega ili kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati.
Mahakama
imekuwa ikilaumiwa kwa kuchelewesha upatikanaji wa haki pasipo
kuangalia mchango wa wadau wengine katika kufanikisha suala hili, hivyo
basi, Taasisi hizi zote hazina budi kuendeleza ushirikiano na chombo
hiki muhimu cha utoaji haki ili nchi iweze kukua kiuchumi. Upatikanaji
wa haki kwa wakati hutoa fursa kwa wananchi kushiriki katika shughuli za
uzalishaji na hivyo kukuza uchumi wa nchi.
SHARE
No comments:
Post a Comment