Watoto wasitumiwe vitani
Julian Msacky
RIPOTI iliyotolewa hivi karibuni na Shirika la Watoto la Umoja
wa Mataifa (UNICEF), inasikitisha.
Inaonesha namna watoto wanavyoishi maisha ya mateso barani
Afrika na kujiingiza katika vitendo visivyofaa.
Shirika hilo limesema vurugu zimesababisha mamilioni ya watoto
kukimbia makazi yao huku wengi wao wakiishi katika mazingira magumu.
Ripoti hiyo inalaani ukosefu wa upatikanaji wa huduma muhimu
kwa watoto ambapo takriban watoto milioni 50 duniani kote wanaishi katika mazingira
hayo.
Tatizo hili linasababisha watoto wajione wapweke na
kutofurahia maisha ya utoto kama walivyo wengine.
Ni wakati muafaka sasa kwa nchi za Afrika kuweka mazingira
bora ya watoto ili waweze kuishi salama na kupata haki zao za msingi.
Haki hizo ni pamoja kutunzwa, kupatiwa elimu, chakula, malazi
na huduma nyingi muhimu ambazo kimsingi anastahili kila mtoto.
Ili kufikia hatua hiyo lazima viongozi wa kisiasa waache kugeuza
nchi zao uwanja wa vita na ngome za mapambano.
Viongozi wetu wafahamu kuwa kwa namna moja ama nyingine
wamechangia kwa kiwango kikubwa mateso ya baadhi ya watoto.
Baadhi yao wameweka madaraka mbele kuliko utu. Wanaangalia
namna wanavyopoteza maisha kwa kukosa chakula au dawa.
Lakini wao wenyewe hawapo tayari kukosa fedha za uchaguzi au
kuendesha maisha yao. Kwa mfumo huo uko wapi upendo tunaohubiri?
Wapo tayari kuwapatia watoto wao tiba nzuri wanapokohoa au
kupiga chafya, lakini wengine wanakufa kwa matatizo hayo hayo. Kweli?
Hapa tena, usawa uko wapi? Kama hiyo haitoshi viongozi hao
hao wapo tayari kuingiza nchi zao kwenye vita bila kujali watu
watakavyoathirika, wakiwemo watoto.
Katika hili nchi mmoja inapokuwa haina vita haina maana hakuna
watoto wanaoteseka, wapo wanaotaabika kwa namna nyingine.
Kwa msingi huo chimbuko la mateso kwa watoto linatakiwa
kuangaliwa kwa undani badala ya kuangalia juu juu.
Kutokana na vita watoto wamekuwa waathirika wa kukimbia huku
na kule kunusuru maisha yao huku hatima yao ikiwa haijulikani.
Inasikitisha pia kuona kwamba madaraka yanapewa kipaumbele
zaidi kuliko uhai wa watu, zikiwemo haki zao za msingi.
Hebu tujiulize ni kiongozi gani leo hii ana habari na watoto
ambao wanakimbia huku na kule ili kuepuka vita katika nchi zao?
Ni kweli tumefikia hatua ya kutoona thamani ya watoto ambao
tuliwatafuta kwa jasho tena tukiomba Mungu usiku na mchana?
Kama kweli hivyo ndivyo ni kwa nini tunawaacha watoto
wateseke na kufanya kazi za kutumishwa na wengine kuwa watumwa wa kingono?
Tukiwa kama wazazi, walezi na viongozi ni lazima tubadilike.
Pili ni lazima tuhakikishe tunawaandaa watoto wetu vizuri na kuhakikisha haki
zao za msingi zinaheshimiwa.
Kama ni migogoro ya kisiasa ndiyo inasababisha wazazi
washindwe kutunza watoto wao hatuna budi kuachana nayo.
Kama ni ndoa kuvunjika ni lazima wazzai wabadilike na
kuhakikisha wanalinda ndoa kwa ustawi wa watoto.
Tukumbuke kuwa migogoro ya ndoa inachangia pia matatizo kwa
watoto, hivyo ni vizuri tuheshimu ndoa zetu kwa ustawi wa watoto wetu.
Kwa kufanya hivyo watoto watalelewa katika mazingira mazuri
na kutoa fursa kwao kupata huduma muhimu za kijamii ambazo kwa leo hii
hawazipati.
Ndiyo maana tunasikia watoto wakikimbilia migodini ambako
wanafanya kazi za kutumishwa huku wakiathiriwa na kemikali ambazo ni hatarishi
kwa maisha yao.
Kama tunawapenda watoto wetu ni lazima tuwakinge na kila
lililo baya. Ni lazima tuhakikishe wanapata elimu nzuri.
Ni lazima tuhakikishe wanapata chakula bora ili kulinda afya
zao na kukuza miili yao inavyotakiwa.
Tuna kila sababu ya kuhakikisha wanapata elimu ambayo ndiyo
msingi muhimu wa maisha.
Tukiwanyima elimu tunawaharibu.
Bila elimu watashindwa kutoa mchango unaostahili katika
kuharakisha maendeleo yao pamoja na nchi kwa ujumla.
Watoto wakikosa elimu madhara yake ni mengi maana watashindwa
kupanga aina ya maisha wanayotaka na hii ni hatari kubwa.
Sisi kama Waafrika na Watanzania tusikubali watoto wetu waishi
maisha ambayo yatakuwa mateso kwa siku zao za usoni.
Tunasema hivi kwa sababu tunazo mali za kutosha kuwaondoa watoto
wetu katika matatizo wanayokumbana nayo leo hii.
SHARE
No comments:
Post a Comment