KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki
na Kati, Azam FC, jana imeendeleza kutoa dozi kwenye kambi yake
nchini Uganda baada kuichapa Onduparaka mabao 3-0.
Huo ulikuwa ni mchezo wa nne wa
kirafiki wa Azam FC nchini humo, baada ya awali kutoka sare mbili, na
Ijumaa iliyopita kuifunga URA mabao 2-0.
Mabao ya Azam FC katika mchezo huo
uliokuwa mkali na aina yake yamefungwa kiufundi na washambuliaji Yahaya
Mohammed dakika ya 40, Yahya Zayd, dakika ya 63 kabla ya beki wa kulia
Swaleh Abdallah, kupigilia msumari wa mwisho dakika ya 74, likiwa ni bao
lake la kwanza tokea arejee Azam FC akitokea Majimaji kwa usajili wa
miaka miwili.
Bao alilofunga leo Yahaya
limemfanya kufikisha mabao manne kwenye mechi tisa za Azam FC za
maandalizi ya msimu ujao walizocheza mpaka sasa, akifunga moja wakati
timu hiyo ilipofungwa na Rayon Sports mabao 4-2.
Akafunga tena mawili wakati Azam
FC ikiichapa URA 2-0 juzi kwenye Uwanja wa Phillip Omondi, kabla ya leo
kutupia jingine, huku kinda Yahya Zayd, naye akiwa ametupia mawili
katika mechi hizo za maandalizi.
Jambo la kuvutia zaidi kwenye
mechi zote za maandalizi za timu hiyo nchini Uganda, Azam FC imeendelea
kuonyesha kandanda safi la pasi na mpira wa kasi huku wachezaji wapya
wakionekana kuingia haraka kwenye mifumo.
Mara baada ya mchezo huo, Azam FC
itamalizia kambi yake ya maandalizi nchini Uganda kwa kucheza mtanange
wa mwisho kesho Jumatatu dhidi ya Vipers, utakaofanyika Uwanja wa St.
Marys unaotumiwa na timu hiyo, uliopo Kitende nchini humo.
Kikosi hicho kitaanza safari ya
kurejea jijini Dar es Salaam, keshokutwa Jumanne, tayari kabisa kwa
kumalizia maandalizi ya mwisho kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaoanza rasmi Agosti 26 mwaka huu, Azam
FC ikiwa imepangiwa kuanzia ugenini kwa kukipiga na Ndanda kwenye Uwanja
wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
Kikosi cha Azam FC leo:
Razak Abalora, Himid Mao/Idd
Kipagwile dk 89, Bruce Kangwa, Aggrey Morris, Yakubu Mohammed, Daniel
Amoah, Stephan Kingue/Masoud Abdallah, Frank Domayo/Salmin Hoza dk 87,
Salum Abubakar/Swaleh Abdallah dk 55, Yahya Zayd/Joseph Kimwaga dk 81,
Yahaya Mohammed/Braison Raphael dk 62
SHARE
No comments:
Post a Comment