Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt John Magufuli na Rais
mstaafu wa Marekani, Barack Obama ni miongoni mwa viongozi wanaotarajiwa
kuhudhuria katika sherehe za uapisho wa Rais mteule wa Kenya, Uhuru
Kenyatta.
Kamati ya maandalizi ya sherehe hizo inayoongozwa na Katibu Kiongozi,
Joseph Kinyua imebainisha kuwa imeandaa orodha ya majina ya viongozi wa
kimataifa kwa ajili ya kushuhudia tukio hilo la kihistoria la uapisho wa
Kenyatta endapo ushindi wa Kenyatta hautopingwa mahakamani.
Kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo, sherehe za uapisho hufanyika siku 14,
baada ya mshindi wa uchaguzi kutangazwa ili kutoa fursa kwa chama
chochote kinachotaka kupinga matokeo kufanya hivyo.
Viongozi wengine wanaotarajiwa kualikwa katika sherehe hizo wakiwemo
wakuu wa nchi ni pamoja na Rais wa Rwanda Paul Kagame, Rais wa Uganda
Yoweri Museveni, Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma na Rais wa Nigeria
Muhammadu Buhari. Wengine ni Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May.
Aidha, katika orodha hiyo pia yupo Rais wa Liberia, Ellen Johnson
Sirleaf, mfanyabiashara tajiri namba moja Afrika Aliko Dangote, Kiongozi
wa Jumuiya ya Ismailia, Aga Khan, Waziri Mkuu mstaafu wa Italia, Matteo
Renzi na Rais Xi Jinping wa China.
“Tupo kwenye maandalizi ya sherehe za uapisho wa Rais wakati tukisubiria
hatua za kikatiba kukamilika. Orodha hii ni ya marafiki wa Kenyatta,
viongozi wa Afrika na viongozi wengine wa kimataifa, tunaotarajia
kuwaalika,” amesema mmoja wa wanakamati hiyo ya maandalizi.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi Kenya, Wafula Chebukati
mwishoni mwa wiki alimtangaza rasmi Rais Kenyatta na Naibu wake, William
Ruto kuwa washindi katika uchaguzi uliofanyika wiki iliyopita nchini
humo.
SHARE
No comments:
Post a Comment