Rais mstaafu wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt
Jakaya Mrisho Kikwete amevitaka vyama tawala barani Afrika
kutovichukulia vyama vya upinzani kama maadui wa serikali badala yake
vionekane kama moja ya nguzo muhimu katika kutimiza utawala wa sheria.
Aidha, Rais Kikwete amewataka wabunge wa vyama tawala pamoja na viongozi
wengine, kuvikosoa vyama vyao pale vinapokwenda mrama badala ya kuwa
waoga na kuunga mkono mambo yote.
Rais Kikwete ambaye ni maarufu Tanzania kwa jina la JK ameyasema hayo
alipokuwa katika mkutano wa masuala ya uongozi barani Afrika wa mwaka
2017 (African Leadership Forum 2017) ambao umefanyikia nchini Afrika
Kusini.
Viongozi wengine waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Rais mstaafu wa
Tanzania, Benjamin Mkapa, Rais mstsaafu wa Nigeria, Olusegun Obasanjo,
Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki na Rais mstaafu wa Malawi,
Bakili Muluzi.
Akizungumza katika kongamano hilo la siku mbili lililomalizika Agosti
25, 2017, JK alisema kuwa, kuvichukulia vyama vya upinzani au wanasiasa
wa upinzani kama maadui, ni kutengeneza uadui ambao hauna ulazima katika
nchi za Afrika.
Kikwete alisema kuwa vyama vya upinzani katika nchi nyingi za Afrika
vina kazi kubwa ya kuhakikisha vinanadi sera zao kwa wananchi ili viweze
kufahamika zaidi kwa vingi ni vichanga. Hii itasaidia wananchi kuwa na
uelewa wa sera pamoja na mipango yao inapofika wakati wa uchaguzi
wakiomba dhamana ya kuongoza nchi, alisema JK.
Mbali na wito huo kwa watawala, Rais Kikwete alivitaka vyama vya
upinzania pia kukubali matokeo ya uchaguzi endapo umefanyika katika
mazingira ya haki, uhuru na uwazi.
Kazi ya vyama vya upinzani ni kuhakikisha kuwa serikali inakuwa macho
muda wote kutekeleza majukumu yake, lakini na wao wasiwe watu wa kupinga
au kukataa kila jambo.
Kauli hii ya Rais Kikwete imekuja wakati ambao vyama vya upinzani nchini
vinalalamika kuhusu kuzuiwa kwa mikutanao ya kisiasa, maandamano,
pamoja na kukamatwa mara kwa mara kwa viongozi wa vyama vya upinzani.
Kwa upande wake Rais Mzee Mkapa, alivitaka vyombo vya habari na
waandishi wa habari kuwa wazalendo kwa nchi zao wanapofanya kazi na
waandike habari zitakazochochea maendeleo ya wananchi pamoja na
kuzikosoa serikali kwa nia ya kujenga.
SHARE









No comments:
Post a Comment