NA MWANDISHI
WETU, RUKWA
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Kamishna wa Polisi (mstaafu)
Zelote Stephen ameialika mikoa yote nchini yenye upungufu wa chakula kwenda
mkoani kwake, kwani kipo cha kutosha.
Ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo
ya kilimo cha kisasa yaliyoshirikisha uongozi wa Mkoa, Wilaya na Halmashauri
zake katika shamba la Msipazi lenye ukubwa wa ekari 4,420 lililopo katika
Kijiji cha China, Kata ya Kate,Wilayani Nkasi linalomilikiwa na Bw.Salum
Summry.
Mkoa wa Rukwa umevuna tani milioni 1.1
za chakula, huku zao la mahindi pekee likiwa limeongoza kwa kuvunwa jumla ya
tani 710,652.
Pia amewaomba wakuu wa mikoa
kuwahamasisha wafanyabiashara kwenye mikoa yao wafike Mkoani Rukwa kununua
bidhaa hiyo ili kuwaondolea hofu wakulima wa mkoani kwake, ya kukosa wateja na
hivyo kuanza mikakati ya kuuza chakula nje ya nchi.
“Nichukue
nafasi hii kuthubutu kuiambia mikoa mingine ambayo haijapata bahati ya kuvuna
kama tulivyovuna sisi watumie fursa hii watuambie kupitia ngazi zilizopo kwamba
wanahitaji nini, hili ni kwa Tanzania bara na visiwani, tunawakaribisha kufanya
biashara na sisi,” Alisema Mkuu wa Mkoa.
Hata hivyo amewaasa wananchi wa mkoa
huo, kutouza chakula chote na kwamba waweke akiba kwani serikali haitatoa
chakula cha msada kutokana na njaa.
“Sisi siyo wachoyo, uchoyo wetu ni
kuhakikisha wananchi wetu wanakuwa na akiba ndani ya nyumba zao, na wale
wanaouza mazao wahakikishe wanatenga fedha zinazotokana na mauzo hayo kwaajili
ya kununua pembejeo za msimu wa kilimo unaofuata,” Amesema
Katika kuhakikisha wakulima wanaondokana
na adha ya mbegu feki na ubabaishwaji wa bei za pembejeo Mh. Zelote amewaagiza
wauzaji wa pembejeo hizo kuweka mabango ya bei nje ya maduka yao na kuwaagiza
wakuu wa wilaya kuwachukulia hatua wale wote watakaogundulika kuuza mbegu feki.
Mbali na hayo Mh. Zelote amesema kuwa
anataka kusikia mkoa wa Rukwa unakuwa wa kwanza nchini kwa uzalishaji wa
chakula baada ya kuwa wa tatu ukitanguliwa na Ruvuma na Mbeya, hivyo aliwataka
wale ambao hawalimi kuonja utamu wa kilimo kwa kulima japo ekari moja.
“Naambia Mkoa wa Mbeya umekuwa wa
Kwanza, tujiulize wametuzidi nini, mkoa wa Ruvuma umekuwa wa Pili, wametuzidi
nini, sasa mwaka huu nataka kusikia mkoa wa Rukwa umekuwa wa kwanza ama wote
watatu tushike namba moja,” alimalizia.
Awali alipokuwa akisoma taarifa ya
shammba hilo, Mkurugenzi wa Shamba la Msipazi Salum Summry amesema kuwa
miongoni mwa changamoto zinazorudisha nyuma juhudi za wakulima katika Mkoa wa
Rukwa ni uwepo wa mbegu zisizo na ubora “Fake” pamoja na wadudu waharibifu wa
mazao.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa suala la mbegu
feki limekuwa likirudisha nyuma juhudi zetu kama wakulima ambao tunaanza
kuchipukia, na pia msimu huu tulishambuliwa na wadudu jamii ya viwavi jeshi
lakini nichukue nafasi hii kukushukuru wewe binafsi, Mkuu wa Wilaya ya Nkasi
pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri kwa mlivyotusaidia kukabiliana na wadudu
hao kwa kuwezesha kupata ndege ya kunyunyizia madawa n ahata mafuta ya ndege
kwaajili ya kazi hiyo,” Salum Summry alisema.
Naye Mstahiki Meya wa manispaa ya
Sumbawanga Mh. Justin Malisawa alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuwahamasisha
wananchi wa Rukwa kulima na kuongeza thamani katika mazao yao.
Mfanyabiashara na mwekezaji katika
kilimo, Bw. Salum Sumry, (kushoto), akifafanua jambo mbele ya Mkuu wa
Mkoa, Mhe. Zelothe Steven, (mwenye miwani), na Katibu Tawala wa Mkoa
huo, Bw.Makali, wakati Mkuu wa Mkoa na ujumbe wake, walipotembelea shamba la Msipazi lenye ukubwa wa ekari 4,420 lililopo katika
Kijiji cha China, Kata ya Kate,Wilayani Nkasi
Mkuu wa Mkoa akifafanua jambo baada ya kutembelea shamba la Bw. Sumry.
SHARE














No comments:
Post a Comment