Na Paschal Dotto- MAELEZO
Serikali kupitia Bodi ya Maziwa
Tanzania (TDB) inatarajia kujenga kituo cha kukusanya na kuuza maziwa
Jijini Dar es Salaam ili maziwa yanayozalishwa kutoka maeneo mbalimbali
ya jiji hilo yaweze kupatikana sehemu maalum ambapo wanunuaji watafika
kwa urahisi.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam
Meneja Masoko wa Bodi ya Maziwa Dkt. Mayasa Simba amesema lengo la
kujenga kituo hicho ni kudhibiti ubora na usalama wa maziwa kwa mlaji na
tayari Manispaa ya Ubungo imekubali kutoa eneo la kujenga kituo hicho
ambacho kitagharimu fedha za kitanzania shilingi bilioni 1.4.
“Kituo hicho kitajengwa Ubungo
kwa sababu zaidi ya lita 6,000 hadi 10,000 huuzwa katika eneo hilo
ambako wachuuzi wengi hufanya kazi zao, kwa hiyo tumeona kuna haja ya
kujenga kituo ili kuwe na sehamu nzuri ya upatikanaji wa maziwa bora na
salama kwa watumiaji” alisema Dkt. Mayasa.
Dkt. Mayasa alieleza kuwa
wachuuzi hao huuza maziwa katika maeneo ya kituo cha mafuta kilichopo
Ubungo Mataa, Riverside na Ubungo External Barabara ya Mabibo Hostel
hivyo si rahisi kwa wanunuzi wa bidhaa hiyo kuipata kwa muda lakini
kukiwa na eneo maalum kutawezesha biashara yao kuthaminika na kupata
faida kubwa.
Aliongeza kuwa wateja takribani
700 hadi 800 hufika kwenye maeneo hayo kila siku kununua maziwa ambapo
bei yake ni kuanzia shilingi 1,000 hadi 1,500 kwa lita.
Akiendelea kutaja faida za kituo
hicho Dkt. Mayasa alisema kuwa kitasaidia kudhibiti uuzaji holela wa
maziwa kwenye chupa za plastiki zilizokwishatumika ambazo si salama
kiafya.
Alibainisha kuwa kituo hiki pia
kitasaidia Bodi hiyo kuratibu Sheria na Kanuni za Maziwa kote nchini
ikiwemo kurahisisha ukusanyaji wa tozo za maziwa (Milk Cess) na
kuboresha sekta ya maziwa pamoja na kutoa ushindani kwa soko la maziwa
Afrika Mashariki.
Katika Mpango wa Miaka Mitano
ulioanza 2013/2014 mkakati wa Bodi ni kuhakikisha kwamba wadau wa tasnia
ya maziwa wanafuata Sheria ya Maziwa na kuhakikisaha kuwa bidhaa
zinazozalishwa zinakuwa na ubora.
“Zao lenyewe ni nyeti kwa hiyo
litahitaji umakini mkubwa sana kwani likiandaliwa vibaya linaweza kuleta
madhara makubwa sana kwa watumiaji”, alisisitiza Dkt. Mayasa.
Naye Meneja Idara ya Huduma ya
Maziwa Bw. Deogratius Mlay alisema kuwa katika takwimu zilizopo, mwaka
huu watumiaji wa bidhaa hiyo kwa maana ya walaji wameongezeka kutoka
asilimia 45 mwaka 2016 mpaka asilimia 47 mwaka 2017, huku asilimia 70 ni
maziwa ya ng’ombe wa kienyeji na 30 ni wa kisasa na asilimia 10 tu ya
maziwa yote ndio inaenda sokoni.
Kwa upande mwingine Bodi ya
Maziwa imetoa tahadhari kwa wananchi wote kuepuka kununua maziwa
yaliyohifadhiwa au kuuzwa kwenye chupa za maji za plastiki kwa kuwa
chupa hizo si salama kutokana na wauzaji kuziokota ovyo mitaani kisha
kuwekea maziwa.
Aidha Bodi hiyo imewaomba
wahisani na wadau mbalimbali wa maendeleo kujitokeza kusaidia ujenzi wa
kituo hicho kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya maziwa na uimarishaji wa
afya ya watanzania.
SHARE








No comments:
Post a Comment