NA OWM, UYUI
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema Serikali italipa madeni yote ya watumishi ambayo
yamehakikiwa na kukutwa kuwa ni halali.
“Mheshimiwa
Rais, Dk. John Pombe Magufuli alisitisha malipo sababu ya zoezi la kubaini
watumishi hewa, sasa kazi hiyo imeshakamilika, yale yaliyobainika kuwa ni
halali yatalipwa. Tunataka watumishi mfanye kazi ya kuwahudumia wananchi kwa
bidii,” alisema.
Ametoa kauli
hiyo jana (Jumamosi, Agosti 12, 2017) wakati akizungumza na watumishi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Uyui kwenye mkutano uliofanyika kata ya Goweko,
wilayani Uyui mkoani Tabora.
Akiwa katika
wilaya za Sikonge, Urambo, Kaliua na Uyui, Waziri Mkuu alielezwa na baadhi ya
wabunge wa mkoa huo kwamba kuna watumishi ambao walihamishwa kutoka manispaa
kwenda wilaya za jirani lakini hawajalipwa fedha zao kwa zaidi ya miaka mitano
sasa.
Kwa nyakati
tofauti, Waziri Mkuu ambaye ameweka utaratibu wa kukutana na watumishi wa umma
kila anapofanya ziara za kikazi mikoani, aliwaeleza watumishi wa wilaya hizo
kwamba Serikali imeanzisha mfumo wa kielektroniki wa malipo ya mishahara kwa
watumishi wa umma ambao unalenga kuondoa tatizo la madai ya malimbikizo ya
stahili zao.
“Hivi sasa
tunadhibiti uzalishaji wa madeni mapya ya watumishi, hakuna madeni ya matibabu,
ya likizo au ya masomo. Kila mtumishi anaruhusiwa kujiendeleza, lakini ni
lazima kwanza aandike barua kwa Mkurugenzi wa Halmashauri kuelezea nia yake na
akikubaliwa, ndipo aanze kutuma maombi kwenye vyuo. Mtumishi akiamua kuomba
chuoni moja kwa moja ndipo alete madai yale, hatapewa chochote kwa sababu ni
nje ya utaratibu,” alisema.
Akifafanua utendaji kazi wa mfumo huo, Waziri Mkuu alisema mfumo huo ujulikanao kama LAWSON, unatumika kwenye ajira za watumishi wote nchini, wa Serikali Kuu na wale wa Serikali za Mitaa na kwamba unasaidia kutunza, kutuma na kuhuisha taarifa za watumishi kwa wakati na kwa ufanisi tangu mtu anapoajiriwa hadi inapofikia wakati wa kupandishwa madaraja ama kustaafu.
Akifafanua utendaji kazi wa mfumo huo, Waziri Mkuu alisema mfumo huo ujulikanao kama LAWSON, unatumika kwenye ajira za watumishi wote nchini, wa Serikali Kuu na wale wa Serikali za Mitaa na kwamba unasaidia kutunza, kutuma na kuhuisha taarifa za watumishi kwa wakati na kwa ufanisi tangu mtu anapoajiriwa hadi inapofikia wakati wa kupandishwa madaraja ama kustaafu.
Akifafanua kuhusu
upandishaji madaraja ya watumishi, Waziri Mkuu alisema Serikali imeondoa
utaratibu wa mtumishi kulazimika kuandika barua ya kukiri kupandishwa
daraja/cheo ndipo aanze kupata stahili zake mpya.
“Hii
imeondoa ucheleweshaji wa kufanyika marekebisho ya mshahara na pili
imeondoa tofauti za mishahara kwa watumishi wenye ngazi moja (sifa sawa za
kitaaluma, tarehe moja ya kuajiriwa) ambao walikuwa wakilipwa tofauti kwa
sababu mmoja aliwahi kuandika barua ya kukiri na mwingine alichelewa kuandika
barua kama hiyo hiyo,” alisema.
“Mimi
nimekuwa kwenye utumishi wa umma kwa muda mrefu, sijawahi kuona mtu anaandikiwa
barua ya kupandishwa daraja halafu anakataa. Kikubwa ni kwa maafisa utumishi
kuona kama kuna watumishi wanastahili kupandishwa madaraja, watume taarifa zao
mapema (kabla ya tarehe 10 ya kila mwezi ili waingizwe kwenye mfumo huu, kisha
wawaandikie barua za kuwajulisha wahusika. Hata barua ikichelewa kumfikia
mtumishi, mshahara wake hautachelewa na kwa njia hii tutaepuka kuweka madeni
yasiyo na tija,” alisema.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwakumbusha watumishi
hao wajibu wao wa kuwahudumia Watanzania bila kujali hali zao na akasisitiza
kuwa Serikali haitamuonea mtumishi yeyote ambaye anatimiza wajibu wake.
“Napenda
kusisitiza kuwa malengo ya Serikali ni kuimarisha utendaji wa watumishi lakini
pia Serikali hii haitamvumilia mtu mdanganyifu, mzembe, asiye mwadilifu na mla
rushwa. Tukikukamata hatuundi tume kwa sababu tume nazo zinamaliza fedha tu.
Tukiwa na ushahidi wa kutosha, tunamalizana hapohapo,” aliongeza.
SHARE
No comments:
Post a Comment