Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Sylvia Lupembe (kulia) akiongea na
Waandishi wa Habari jana jijini Dar es Salaam kuhusiana na kukamilika kwa
ukarabati wa shule kongwe 10 za Serikali. Kushoto ni Meneja Ufadhili
Miradi ya Elimu, Anne Mlimuka.
Meneja Ufadhili Miradi ya Elimu wa
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Anne Mlimuka akiongea na Waandishi wa
Habari leo jijini Dar es Salaam kuhusiana na malengo ya mradi wa
ukarabati wa shule kongwe 10 za Serikali. Kulia ni Meneja Uhusiano na
Mawasiliano wa TEA, Sylvia Lupembe.
Picha na Fatma Salum-MAELEZO
…………………………
Na. Neema Mathias-MAELEZO
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA)
imekamilisha awamu ya kwanza ya ukarabati wa shule 10 kongwe za Serikali
ili kusaidia kuwepo kwa miundombinu bora ya kujifunzia na kufundishia
pamoja na kuongeza nafasi za wanafunzi kupata elimu.
Hayo yameelezwa jana Jijini Dar es
Salaam na Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa mamlaka hiyo Bi. Sylvia
Lupembe wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na
maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ukarabati wa Shule Kongwe za
Sekondari, ambao unatekelezwa na Serikali kupitia TEA na Wizara ya
Elimu kwa kushirikiana na wadau wengine.
“TEA inakarabati takriban shule
kongwe 17 kati ya 87 na tumeanza ukarabati wa shule 10 katika awamu ya
kwanza unaogharimu shilingi bilioni 10, mpaka sasa ukarabati huo
umefikia asilimia 80 na ifikapo mwezi Oktoba utakuwa umekamilika. Shule
nyingine 7 zitakarabatiwa katika awamu ya pili,” alifafanua Bi. Lupembe.
Alizitaja shule zinazokarabatiwa
kuwa ni Mzumbe na Kilakala – Morogoro, Shule ya Sekondari ya wasichana
Msalato-Dodoma, Shule ya Sekondari Mwenge – Singida, Shule ya Sekondari
Pugu – Dar es Salaam, Shule ya Sekondari Ilboru –Arusha, Shule ya
Sekondari Same-Kilimanjaro, Shule ya Sekondari Tabora Wavulana na Tabora
Wasichana na Shule ya Sekondari ya Wasichana Nganza iliyopo Mwanza.
Aidha Bi. Lupembe aliongeza kuwa
awamu ya kwanza ya ukarabati umehusisha miundombinu ya majengo ikiwemo
mabweni, madarasa, majengo ya utawala, kuboresha mifumo ya maji safi na
maji taka, mifumo ya umeme pamoja na mifumo ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano.
“Tayari makabidhiano ya awali
yamefanyika kwa baadhi ya majengo hususan mabweni na madarasa katika
shule za Msalato, Mwenge na Mzumbe,” alieleza Bi. Lupembe.
Bi. Lupembe alibainisha kuwa
mafanikio kutokana na mradi huo yameanza kuonekana kwani ari ya
wanafunzi kusoma imeongezeka na idadi ya usajili wa wanafunzi
imeongezeka katika shule ya Mwenge na nyingine zilizokarabatiwa.
Kwa upande wake Meneja Ufadhili
Miradi ya Elimu Bi. Anne Mlimuka alieleza malengo mbalimbali ya mradi
huo ikiwa ni pamoja na kuhifadhi ubora wa miundombinu ili kuhakikisha
wanafunzi wanapata elimu bora katika mazingira bora, kuongeza idadi ya
udahili wa wanafunzi katika shule za Serikali na kuboresha miundombinu
ya maabara kwaajili ya wanafunzi wa masomo ya Sayansi ili kuendana na
Sera ya Viwanda inayohitaji wataalam wengi wa Sayansi.
“Mradi huu wa kukarabati shule
kongwe utakapokamilika utaendelea kwenye shule za Kata ili kuirudisha
elimu katika hadhi yake na kuzifanya shule zote za serikali nchini zitoe
elimu bora, wataalam bora katika mazingira bora kama ilivyokuwa hapo
awali,” alisema Bi. Mlimuka.
Mamlaka ya Elimu Tanzania kupitia
mradi wake wa kukarabati shule kongwe za Sekondari za Serikali unalenga
kuimarisha Sekta ya Elimu nchini hasa kwa Shule za Serikali ambazo
zilipoteza hadhi yake iliyokuwa hapo awali pamoja na kufadhili miradi
mbalimbali ya elimu katika ngazi za Sekondari na Elimu ya Msingi.
SHARE
No comments:
Post a Comment