Msimamizi
mkuu wa Kampuni ya uchambuzi wa mbegu za pamba Quton Tanzania Limited,
Pradyumanshinh Chauhan(Kulia), akitoa maelezo kwa waandishi wa habari
waliotembelea kiwanda hicho kinachohusika na uchambuzi na usindikaji mbegu za
pamba kilichopo Kasoli wilayani Bariadi mkoani Simiyu.
|
Mbegu mpya
aina ya UKM 08 toka kampuni ya Quton, ikiwa kwenye sahani ya maonesho, mbegu
hii tayari imefanyiwa majaribio na kuwa na sifa ya kuota bila kubahatisha nayo
imekuja sokoni sasa kwaajili ya kuiondosha ile ya zamani iliyojulikana kama UKM
91 pamoja na ile ya manyoya.
|
Mwandishi Wetu, Mwanza
WAKULIMA wa Mkoa wa Simiyu
wameielezea mbegu mpya ya Pamba ya UKM 08 isiyo na manyoya, kuwa ni bora
kutokana na kuitumia na kuongeza uzalishaji wao hivyo kuiomba serikali
kuisimamia kikamilifu kuhakikisha inalitumia na wakulima wote.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti wakati ya ziara na wanahabari
kujionea uzalishaji wa mbegu bora Mkoani Simiyu, baadhi ya wakulima waliopanda
mbegu hiyo katika msimu wa 2016/17 walisema mbegu hiyo ina ubora wa hali ya juu
sana ukilinganisha na mbegu ya manyoya ya UK91 ambayo imekuwa ikitumika kwa
miaka 26.
Mbegu ya UK91 huzalisha wastani wa kilo 300 kwa ekari ukilinganisha na
mbegu mpya ya UKM08 iliyotolewa manyoya ambayo inazalisha mpaka kilo 1,200 kwa
ekari.
Akielezea mafanikio aliyoyapata
Christopher Nkhanda, mkulima wa Kata ya Mwabusalu Wilaya ya Meatu Mkoa wa
Simiyu, alisema mbegu ya UKM 08 ni bora na yenye mavuno mengi huku akibainisha
kuwa katika ekari 27 alizolima aliweza kupata tani 17 za pamba ambao ni wastani
wa kilo 600 kwa ekari pamoja na kwamba hali ya hewa ilikuwa mbaya kutokana na
ukame.
Awali mavuno yalikuwa hayazidi kilo 300 hata katika msimu ambao
hali ya hewa ni nzuri na kuna mvua ya kutosha.
“Mwanzoni niliziogopa sana mbegu
hizi kutokana na kusikia maneno ya watu kuwa hazioti, hata wakati naanza
kuzilima kwa majaribio mwaka juzi watu walinicheka lakini niliona zinamafanikio
makubwa ndipo nilipoamua kuzilima kwa wingi na kufanikiwa kupata mavuno mara
mbili ya yake ya siku zote,” alisema.
Alisema katika kutumia mbegu hizo
amejifunza kuwa kutokana na ubora wake hapaswi kupanda nyingi kama walivyokuwa
wamezowea mbegu ya zamani aina ya UK 91 ambayo kwa ekari moja walikuwa
wakipanda kati ya kilo 15 mpaka 20 lakini sasa anapanda kilo 6 tu kwa ekari na
kupata mavuno maradufu kwani mbegu hiyo ina kiwango kikubwa cha uotaji na
vilevile inapita vizuri kwenye mashine ya kupandia jambo ambalo litasaidia
katika kuongeza tija kwani mashine inapanda kwa kuacha nafasi kama
inavyoshauriwa kwenye kanuni bora za kilimo cha pamba.
Matondo Kitinya mkulima wa
Kijiji cha Ikugijo Wilaya ya Meatu, akizungumzia mbegu hiyo mpya ya UKM 08,
alisema alinunua kilo sita kwa ajili ya ekari moja kwa Sh 15,000 na kuzipanda
kwa majaribio ambapo aliweza kuvuna kiasi cha kilo 700 na kupata kipato cha
shilling 900,000 kutokana na mavuno hayo.
“Ekari moja niliyolima kwa msimu
uliopita nilitumia kiasi cha Sh 180,000 kulima, kupanda, palizi hadi kuvuna na
kufanikiwa kuvuna kiasi cha kilo 700 tofauti na kilo 200 ambazo nilikuwa
nikipata awali wakati nikitumia mbegu ya UK 91,” alieleza.
Alisema mbegu ya zamani walikuwa
wakipanda kiasi cha kilo 15 hadi 20 kwa ekari moja tofauti na hizi ambazo
wanapanda kilo sita tu lakini zikiota ndani ya siku tatu japo alisema ili upate
mafanikio yake ni lazima uzipande kwa kuzingatia vipimo na mstari kwa kuwa
hazihitaji kubanana na mche mmoja hutoa vitumba 80 au zaidi.
Kwa upande wake Minza Lukomanga
wa kijiji cha Ng’obhoko wilaya ya Meatu, alisema mbegu hizo licha ya kuwa na
mavuno makubwa lakini zimekuwa rahisi kwake kupandwa kutokana na kutumia
mashine ya kupandia hivyo kuiomba serikali kuendelea kuzalisha ikiwa ni pamoja
na kuwafikishia wakulima elimu na mbegu hii.
Akizungumzia mbegu hizo, Meneja
wa Kanda wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) Jones Bwahana, alisema imekuwa na
mafanikio makubwa kwa wakulima walioitumia na kwamba mkakati wa bodi ni
kuhakikisha mpaka kufikia 2019 mbegu hiyo ya UKM08 inalimwa katika eneo lote la
uzalishaji wa pamba hapa Tanzania.
Alisema tani zaidi ya 4,000 za mbegu ya
UKM08 zilizotolewa manyoya zitasambazwa katika msimu huu wa 2017/18 ikiwa ni
sehemu ya mango wa serikali kuhakikisha wakulima wote wa paamba nchini
wanatumia mbegu bora kufikia mwaka 2019.
Alisema Serikali kupitia Wizara
ya Kilimo, Chakula na Ushirika tangu mwaka 2010 ilitoa jukumu la uzalishaji
mbegu bora aina ya UKM 08 kwa Kampuni ya Quton (T) Ltd ambazo zimekuwa
zikithibitishwa na Taasisi ya Kupima Ubora wa Mbegu (TOSCI) kabla ya kusambazwa
kwa wakulima.
Mkuu wa Kampuni ya Quton (T) Ltd,
Pradyumansinh Chauhan alisema mbegu hiyo imethibitika kuweza kuhimili magonjwa
kutokana kuandaliwa katika mfumo ambao unaua vijidudu vyote vinavyosababisha
magonjwa.
Mbegu hiyo ambayo ilipatikana kutokana na utafiti wa Taasisi ya
Utafiti wa Kilimo ya Ukiriguru uondolewa manyoya kwa kutumia tindikali na
baadaye kuondoa tindikali hiyo katika mbegu kwa mfumo wa mtetemo (gravity
table) ambapo upimwa na kuthibitishwa na Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu
(TOSCI) kabla ya kumfikia mkulima.
Alisema kwa sasa wanazalisha tani
4,000 za mbegu wakati uwezo wao ni tani 10,000 kwa msimu na mbegu hizo kwa sasa
zimeanza kulimwa katika maeneo ya Wilaya ya Meatu, Bariadi mkoani Simiyu,
Wilaya ya Bunda mkoa wa Mara na Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.
SHARE
No comments:
Post a Comment