Wakurugenzi watatu wa juu wamejiuzulu kutoka katika
baraza la uchumi na uzalishaji la Ikulu ya Marekani, wakati rais Donald
Trump akiendelea kukabiliwa na ukosoaji kwa kuchelewa kulaani makundi
yenye chuki.
Mkurugenzi wa kampuni ya teknolojia ya Intel Brian Krzanich na Kevin
Plank ambaye ni mkuu wa kampuni ya utengenezaji wa vifaa vya michezo
chini ya Armour wameungana na mkurugenzi mwingine wa Merck, Keneth
Frazier kujiuzulu katika baraza la uchumi na uzalishaji la rais Trump.
Kujiuzulu huko kunatokana na ghasia zilizojitokeza mjini Charlottesville
ambapo Bw. Krzanich amebainisha sababu iliyochangia akisema,
"nimejiuzulu kwa sababu nataka kusonga mbele, wakati wengi mjini
Washington wanaonekana kujali zaidi kumshambulia kila mmoja
asiyekubaliana nao."Awali, Frazier mmoja ya wakurugenzi wakubwa weusi wenye umaarufu nchini Marekani alitangaza kujiuzulu akisema "viongozi wa Marekani wanapaswa kuheshimu misingi muhimu kwa kukataa kwa uwazi chuki, wale wasioweza kuvumilia misimamo ya wengine na makundi yanayojiona bora zaidi ya wengine.
Trump, baadaye alimshambulia Frazier kupitia ukurasa wake wa Twitter akisema kwamba kwa kuwa Frazier amejiuzulu sasa atakuwa na muda mzuri wa kushusha bei za wizi.
Hapo awali Trump alivunja ukimya na kulaani makundi ya weupe wanaojiona bora baada ya kuzidi kukoselewa kwa kushindwa kutamka bayana ushiriki wa wazungu wenye itikadi kali na misimamo ya kibaguzi katika shambulio la mjini Virginia siku ya Jumamosi, badala yake alilaani vurugu hizo kuwa pande zote mbili zinahusika."Ubaguzi ni mbaya, Na wale wanaosababisha vurugu kupitia mgongo huo ni wahalifu na majambazi, ikiwemo KKK, Wanazi mambo leo, wazungu wanaojiona bora kuliko wengine pamoja na vikundi vingine vyenye chuki ambavyo vinakataa kila kitu ambacho sisi Wamarekani tunakishikili," alisema rais Trump.
Mkutano wa wazungu walio na itikadi kali mjini Charlottesvile uligeuka kuwa wa vurugu baada ya mzungu mmoja kudaiwa kulivurumusha gari katikati mwa kundi la waandamanaji waliokuwa wakipinga maandamano ya ubaguzi wa rangi, na kumuua mwanamke mmoja na kuwajeruhi wengine 19.
Trump ameongeza kwamba idara ya sheria imeanzisha uchunguzi wa haki za kiraia na wote waliohusika katika shambulio wataadhibiwa kisheria. Licha ya tamko lake la kulaani ubaguzi huo, wakosoaji waliendelea kuhoji kama maneno yake yaliyochelewa kutolewa yangebadili uharibifu uliokwishajitokeza kwa kushindwa kukemea kwa uwazi namna alivyomshambulia Frazier.
Trump amekutana mapema jana na mwanasheria mkuu Jeff Sessions na mkurugenzi wa shirika la upelelezi la Marekani FBI, Chris Wray kujadili juu ya uchunguzi huo.
Sessions alikiambia kituo cha utangazaji cha ABC kwamba tukio hilo linatoa taswira ya ugaidi wa ndani na kutoa hakikisho kwamba watawafungulia mashitaka wahusika na kwenda mbele zaidi na uchunguzi kwa sababu ni tukio baya lisilokubalika.
Mwanamume aliyeendesha gari katika umati wa waandamanaji James Alex Fields Jr wa Ohio ameshitakiwa kwa kosa la mauaji na uhalifu mwingine na alinyimwa dhamana wakati wa shauri hilo mahakamani jana Jumatatu.
CHANZO: DW
SHARE
No comments:
Post a Comment