Miongoni mwa majengo yake mengi
yakiwa yamejengwa mnamo karne ya 18 na 19, Mji Mkongwe wa Zanzibar bado
haujapoteza taswira yake halisi mpaka hivi leo. Na kutokana na muonekano
huo, kutembea na kuvinjari mitaa na majengo mbalimbali kunakufanya
ujihisi kama kweli ulikuwepo kipindi cha nyuma pindi inajengwa.
Kati ya
majengo maarufu ambayo Jumia Travel inakuhakikishia utayaona pindi
utakapoingia kwenye mji huu ni pamoja na Ngome Kongwe iliyojengwa kwenye
eneo la mwanzo la Kanisa la Wareno; nyumba ya maajabu; kasri kubwa
iliyojengwa na Sultan Barghash; zahanati ya kale; Kanisa Kuu Katoliki la
Mtakatifu Joseph; Kanisa Kuu la Kristu la Waanglikana likiwa limejengwa
kukumbuka kazi ya David Livingstone katika kukomesha biashara ya utumwa
na kujengwa eneo lilipo kuwepo soko la watumwa; makazi ya aliyekuwa
mfanyabiashara maarufu wa watumwa Tippu Tip; Msikiti wa Malindi Bamnara;
jengo la Jamat Khan lililojengwa kwa ajili ya dhehebu la Ismailia; eneo
la makaburi ya Kifalme; na mabafu ya Kiajemi.
Kwa
pamoja, mitaa na barabara nyembamba zikiwa na kona nyingi, na majengo
makubwa yanayotazamana na bahari ndyo yanaufanya mji huu kuwa wa kipekee
ukiakisi shughuli za muda mrefu za kibiashara kati ya Waafrika na
Waarabu. Kwa ujumla, Mji Mkongwe unatambulika kama sehemu ambayo
hatimaye biashara ya utumwa ilikomeshwa.
Kutokana
na upekee na umaarufu wake mamia ya maelfu ya watalii kutoka kona
mbalimbali za dunia husafiri kuja kujionea vivutio vya kila aina
vinavyopatikana kwenye mji huu mkongwe wa Zanzibar.
Kwa ufupi
takribani kila kitu ndani ya Mji Mkongwe kina historia ya kuvutia na
kusisimua. Kuanzia mila na tamaduni za watu wake, shughuli
wanazozifanya, vyakula vyao na majengo ni utalii tosha ambao hauwezi
kupatikana sehemu yoyote duniani.
Huchukua
muda wa saa moja na nusu kusafiri kwa kutumia boti kutoka Dar es Salaam
mpaka kufika Zanzibar na usafiri huanzia saa moja asubuhi mpaka saa 12
za jioni. Hivyo basi kumbe inawezekana kwa mtu kutokea jijini Dar es
Salaam akaenda kule, akatalii na kurudi siku hiyo hiyo.
Na kama una
mpango wa kuufaidi zaidi mji huo pia inawezekana kwani vyakula na malazi
vya gharama nafuu kabisa ambayo kila mtu anaweza akamudu.
Uzuri wa
Mji Mkongwe ni kwamba ni rahisi kuuzunguka kwani mitaa yote inapitika
kwa urahisi kabisa aidha kwa kutumia ramani ya karatasi au simu (google
map) au muongozaji wa kitalii utayempata. Ni vizuri kuwa na muongozaji
mzuri kama ni mara yako kwanza kufika kule ili iwe rahisi na pia
kutembelea sehemu nyingi zaidi ambazo hauzifahamu.
Kikubwa
cha kushangaza zaidi ni namna majengo yalivyojengwa kwa ustadi mkubwa
kwa kutumia vifaa mbalimbali kama vile chokaa, matumbawe na miti. Na cha
kuvutia zaidi ni umri wa majengo hayo ambayo yamekuwepo karne na karne
bila ya kupoteza uhalisia wake. Pongezi kubwa ziende kwa serikali na
shirika la Umoja wa Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO)
kwa kuweka jitihada kubwa na sheria za kuulinda mjii huu. Kutokana na
jitihada hizo mnamo mwaka 2000 UNESCO liliutangaza Mji Mkongwe wa
Zanzibar kama eneo la urithi wa dunia.
Utakuwa
haujaufaidi Mji Mkongwe endapo hautopata fursa ya kula vyakula
mbalimbali (vya baharini) vinavyopatikana katika migahawa tofauti. Eneo
maarufu ambalo unaweza kuvipata vyakula vya aina hiyo kwa pamoja ni
kwenye bustani ya Forodhani. Litakuwa jambo la ajabu kama umefika
Zanzibar na hukuenda kutembelea eneo hili. Umaarufu wa bustani ya
Forodhani umetokana na mkusanyiko wake wa aina lukuki za vyakula vya
baharini vinavyopatikana pale kila siku kuanzia jioni. Na ni eneo ambalo
huwakutanisha watu kutokea sehemu mbalimbali za visiwa vya Zanzibar,
hivyo inawezekana kukutana na watu ambao mlikuwa mkipishana mchana
kutwa.
Kutembelea,
kuogelea na kutazama jua likizama kwenye fukwe ya bahari ya Hindi ukiwa
Zanzibar nazo ni miongoni mwa shughuli ambazo watalii wengi hufurahia.
Baadhi ya hoteli ambazo ukiwa kwenye Mji Mkongwe unaweza kuyafanya hayo
ni kama vile Mizingani Seafront Hotel, Africa House Hotel na Seyyida
Hotel & Spa.![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjkE8IVaSmYyuwER3yd54caToNNQKYytVhjqctAVAYr8XPWo3FI22qeRazVrVnw9cxUjkJpcel9twEJVEI3QgPdnx_VKsVuhAZptE8CtAGF4Hfl31SIW5d40CcasxN3a9-F9E9xZDTKZFfr/s640/005.jpg)
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjkE8IVaSmYyuwER3yd54caToNNQKYytVhjqctAVAYr8XPWo3FI22qeRazVrVnw9cxUjkJpcel9twEJVEI3QgPdnx_VKsVuhAZptE8CtAGF4Hfl31SIW5d40CcasxN3a9-F9E9xZDTKZFfr/s640/005.jpg)
Kwa
kumbukumbu zako itakuwa ni vema zaidi ukibeba kamera kwa ajili ya kupiga
picha matukio mbalimbali unayoyaona njiani. Kwa majengo inakuwa ni
rahisi zaidi ila kwa watu itakuwa ni busara ukaomba ruhusa ili kuepuka
matatizo kwani sio wote watakuwa tayari kufanya hivyo. Zanzibar ni kubwa
na ina maeneo mengi ya kutembelea ila kwa leo Jumia Travel inaamini
angalau utakuwa umeipata picha ya Mji Mkongwe wa Zanzibar na shughuli za
kufanya na kufurahia ukiwa kule.
SHARE
No comments:
Post a Comment