Katibu
Mkuu wa Wizara ya Biashara, Uwekezaji na Ushirikiano wa Kenya, Dkt. Chris
Kiptoo na Mwenjeji wake Prof. Adolf Mkenda wakionyesha Sera ya Taifa ya
Biashara ya Kenya wakati mkutano baina ya Watendaji Wakuu wa Serikali,
Wafanyabiashara na Wazalishaji wa bidhaa za kilimo katika Mataifa hayo
uliojadili changamoto na utatuzi wa vikwazo vya biashara na uwekezaji katika
Mataifa hayo. Mkutano huo ulifanyika jana Septemba 8 Jijini Dar es Salaam.
Balozi
wa Tanzania nchini Kenya, Dkt. Pindi Chana akitoa taarifa ya majadiliano ya
mkutano baina ya Watendaji Wakuu wa Serikali ya Tanzania na Kenya uliojadili
changamoto na utatuzi wa vikwazo vya biashara na uwekezaji katika Mataifa.
Mkutano huo ulifanyika jana Septemba 8 Jijini Dar es Salaam. Wengine katika
Picha ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara ya Tanzania, Prof. Adolf Mkenda na
Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara ya Kenya Dkt. Chris Kiptoo.
NA ISMAIL NGAYONGA, MAELEZO
SERIKALI za Tanzania na Kenya
zimekubaliana kwa pamoja kumaliza vikwazo vya kibiashara katika usafirishaji na
uingizaji wa bidhaa katika mipaka baina ya nchi hizo mbili hatua
inayokusudia kuimarisha ushirikiano wa biashara na uwekezaji katika
Mataifa hayo.
Hayo yamesemwa jana Jijini Dar es Salaam
na Katibu Mkuu wa Wizara ya Wizara, Biashara na Uwekezaji (Biashara na
Uwekezaji) Prof. Adolf Mkenda mara baaada ya kumalizika kwa mkutano
wa pamoja yao ulioshirikisha Viongozi Waandamizi
wa Serikali hizo, Wafanyabiashara na Wakulima kutoka Mataifa hayo.
Anasema katika mkutano huo Serikali ya
Tanzania iliwasilisha mapendekezo 15 kwa Serikali ya Kenya yanayopaswa kupatiwa
ufumbuzi, ambapo kwa upande wa Kenya waliwasilisha mapendekezo 16 ambapo kwa
kiasi kikubwa hoja hizo zimekubaliwa na kupatiwa majibu yake katika mkutano
huo.
Prof. Mkenda alisema kupatikana kwa
mwafaka wa majadiliano hayo ni maelekezo ya Viongozi Wakuu wa Mataifa
hayo, Rais Dkt. John Pombe Magufuli wa Tanzania na Uhurru Kenyatta
wa Kenya kwa kuwa Viongozi hao wametaka suala hilo lipatiwe mwafaka wa haraka
ili kuweza kuendeleza ushirikiano na uhusiano katika nyanja mbalimbali baina ya
nchi hizo.
Kwa mujibu wa Prof. Mkenda alisema mkutano
huo uliofanyika kwa muda wa siku tatu ulilenga kumaliza changamoto za biashara
zinazojitokeza kwa Wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya, ambapo Timu za
Wataalam wa Serikali hizo ambapo hoja hizo zimeweza kujadiliwa na kupatiwa
ufumbuzi wa pamoja, hatua inayolenga kufungua upya milango ya ushiriakiano
baina ya Wafanyabiashara na Wakulima wa Tanzania na Kenya.
“Katika majadiliano yetu tumekubaliana
kuwa sasa bidhaa ya gesi ya kupikia na ungano wa ngano ambazo zilizuliwa
kuingia Kenya sasa zitaruhusiwa kuingia nchini humo, na sisi kwa upande wetu
Tanzania tumeruhusu maziwa na sigara kutoka Kenya zianze kuingia nchini”
alisema Prof. Mkenda.
Akifafanua zaidi Mkenda anasema Mkutano
huo pia uliwashirikisha Wafanyabiashara na Kampuni za uzalishaji wa
bidhaa za ngano ikiwemo kampuni ya Azam Bakhressa ambayo huzalisha na kusambaza
ngano hapa nchini pamoja na nchi jirani ikiwemo Kenya pamoja na wakulima
wa zao hilo kutoka mikoa ya Sumbawanga, Iringa na Manyara.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa
Wizara ya Viwanda, Biashara na Ushirikiano ya Kenya, Dkt. Chris Kiptoo alisema
Serikali ya Kenya itayachulia kwa uzito unaostahili mwafaka wa majadiliano hayo,
kwa kuzingatia kuwa Serikali ya Tanzania na Kenya zina uhusiano na ushirikiano
wa muda mrefu katika masuala ya biashara na uwekezaji.
Alisema kuwa Serikali ya Kenya imewekeza
jumla Dola Bilioni 1.5 katika sekta ya viwanda, ambapo hadi sasa
vimeweza kuajiri jumla ya watu 50,000 na pia msingi wa biashara ya Kenya katika
Tanzania imeweza kuongeza kutoka Tsh. Bilioni 17 mwaka 2004 hadi kufikia Dola
Bilioni 34 mwaka 2015.
Dkt. Kiptoo anasema mara baada ya mkutano
huo, Viongozi wa Serikali hizo pamoja na Wafanyabiashara kutoka upande za
Tanzania na Kenya wanatarajia kukutana kwa mara ya mwisho Mombasa nchini Kenya
kwa ajili ya kuhitimisha makubaliano ya pamoja ya uingizaji na usafirishaji wa
bidhaa.
Akifafanua zaidi Dkt. Kiptoo anasema
katika majadiliano hayo Idara muhimu zinazohusika na masuala ya biashara na
uwekezaji kutoka Serikali za Tanzania na Kenya zilishiriki katika mkutano huo,
ikiwemo Maafisa wa Idara za forodha, kodi na ushuru.
Tarehe 3 Agosti mwaka huu, Viongozi
Waandamizi wa Serikali za Tanzania na Kenya walikutana katika Mpaka wa Namanga
kwa ajili ya kikao cha majadiliano ya pamoja kilicholenga kumaliza mzozo wa
kuzuiwa kwa Wafanyabiashara ya Ngano nchini kuingiza bidhaa hiyo nchini Kenya.
SHARE
No comments:
Post a Comment