Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias
Kwandikwa, akitoa maelekezo kwa Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo (TBA),
mkoa wa Mtwara Edward Mwangasa, wakati alipokuwa akikagua nyumba
zinazomilikiwa na Wakala huo, mkoani humo.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo
(TBA), mkoa wa Mtwara Edward Mwangasa, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri
wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, katika ukaguzi wa nyumba zinazomilikwa na
Wakala huo ambao unamiliki jumla ya nyumba 76 mkoani humo.
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Evod
Mmanda, akisisitiza jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa,
wakati alipokuwa akikagua nyumba zinazomilikiwa na Wakala wa Majengo
(TBA), mkoani humo.
……………………
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias
Kwandikwa, ametoa agizo kwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA),
kuhakikisha wanazitambua na kuzisajili nyumba zote na viwanja vya
Serikali zinazomilikiwa na Wakala huo katika maeneo mbalimbali nchini.
Agizo hilo amelitoa mkoani Mtwara,
mara baada ya kukagua nyumba na viwanja vinavyomilikiwa na Wakala huo
na kusisitiza kwa Mameneja wa mikoa wa Wakala huo kuhakikisha wanafanya
matengenezo na ukarabati wa majengo hayo ili kuvutia wapangaji wao.
“Wasimamizi wa nyumba hizi
hakikisheni nyumba hizi mnazitambua na mnazifanyia matengenezo ya mara
kwa mara, nimetembelea Halmashauri mbalimbali na kuona baadhi ya nyumba
za Serikali haziridhishi baada ya kuwa zimetelekezwa muda mrefu”,
amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Aidha, Naibu Waziri huyo amemtaka
Kaimu Meneja wa TBA mkoani Mtwara, kuhakikisha nyumba na viwanja vyote
anavyosimamia vinakuwa na hati ili kidhibiti changamoto ya wananchi
kuvamia viwanja vya Serikali.
Amekemea tabia ya baadhi ya wapangaji wa nyumba za Serikali
kutozitunza wala kuzijali nyumba hizo hali inayoipelekea Serikali
kuingia gharama kubwa katika kufanya marekebisho ya nyumba hizo.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa
TBA mkoani hapo, Edward Mwangasa, amekiri kutokuwa na hati kwa baadhi ya
nyumba na viwanja wanavyovimiliki na hivyo amemuahidi Naibu Waziri
huyo kuhakikisha anasimamia suala la utafutaji wa hati kwa nyumba hizo
na viwanja vyote 128 walivyonavyo sasa.
“Mheshimiwa Naibu Waziri nakuhakikishia kulifanyia kazi suala
la ufuatiliaji wa hati za nyumba na viwanja ili kuweza kuepuka migogoro
na wananchi wanaovamia viwanja vyetu”, amesitiza Kaimu Meneja.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara,
Evod Mmanda, amewataka wananchi kufuata sheria na kwamba hairuhusiwi
kuvamia maeneo ya Serikali kwani maeneo hayo huwa yanatengwa kwa ajili
ya shughuli za Serikali.
Wakala wa Majengo Mkoani Mtwara una jumla ya nyumba 76 ambapo
Manispaa ya mji wa Mtwara ina nyumba 64, Masasi 4, Nanyumbu 5 na
Tandahimba 3 ambapo baadhi ya nyumba hizo zina hati na nyingine hazina.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
SHARE
No comments:
Post a Comment