Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akifafanua
jambo kuhusu ukusanyaji madeni ambayo Wakala wa Majengo nchini (TBA)
inadai wapangaji wake.
Muonekano
wa barabara ya Sakina-Tengeru Km 14.1 inayojengwa kwa njia nne kwa
kiwango cha lami ili kupunguza msongamano wa magari kuingia na kutoka
katikati ya jiji la Arusha.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akijadiliana
jambo na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Fadhili Nkurlu jijini Arusha.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (kulia)
akikagua ripoti ya biashara inayofanywa na Kampuni ya Simu nchini
(TTCL), jijini Arusha. Wa tatu kulia ni Meneja Kanda ya Kaskazini TTCL
Bw. Peter Lusama.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (katikati)
akiimba wimbo wa mshikamano daima na wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wa
Wakala wa Barabara nchini TANROADS kabla ya kufungua rasmi mkutano wa
sita wa Baraza hilo. Kulia ni Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng. Patrick
Mfugale na kushoto ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Fadhili Nkurlu.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akisisitiza
kufanya kazi kwa malengo yanayopimika katika kikao chake na wafanyakazi
wa taasisi zilizo chini ya wizara yake, jijini Arusha.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akitoa
maelekezo kwa mkandarasi M/S Hanil Jiangsu J/V anayejenga barabara ya
Sakina-Tengeru Km 14.1 na barabara ya mchepuo wa kusini Arusha bypass Km
42.4 jijini Arusha.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa
ametoa mwezi mmoja kwa makandarasi wote nchini kuhakikisha wanasaini
mikataba ya ajira na wafanyakazi katika miradi ya ujenzi wa barabara
inayoendelea nchini kote.
Akizungumza jijini Arusha mara baada ya kufanya ukaguzi wa mradi
wa ujenzi wa barabara ya Sakina-Tengeru yenye urefu wa Km 14.1 na
barabara ya mchepuo ya kusini (Arusha bypass) yenye urefu wa Km 42.4,
Prof. Mbarawa amesema mkandarasi atakayeshindwa kutoa mikataba kwa
mujibu wa sheria za Tanzania, atanyang’anywa kazi ya ujenzi kwa kuvunja
sheria.
“Barabara zinajengwa kwa kodi za wananchi hivyo wajenzi wa
barabara nao ni lazima wafuate sheria za nchi ili kuhakikisha Serikali
inapata kodi stahili na wafanyakazi wazawa nao wanapata haki stahili kwa
mujibu wa ajira zao", amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Amezitaka taasisi za TRA, NSSF na nyingine zinazosimamia ajira za
wafanyakazi kufuatilia miradi ya ujenzi ili kuona fursa za mapato ambazo
serikali inaweza kupata na kusajili wafanyakazi katika hifadhi ya
mifuko ya jamii.
Waziri Prof. Mbarawa amewataka mameneja wa tanroads na maafisa
kazi kukagua mikataba ya ajira za ujenzi katika maeneo yao ili kuona
haki inatendeka kwa makandarasi na kwa wafanyakazi ili ujenzi wa
barabara ukamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amefungua mkutano wa Sita wa
Baraza la Wafanyakazi la Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) na
kuwataka kuweka mikakati itakayowezesha kulinda hifadhi ya barabara,
kudhibiti magari yanayozidisha uzito na kusimamia kasi katika miradi ya
ujenzi wa barabara.
“Mmekua mkifanya kazi nzuri, endeleeni kufanya kazi kwa uadilifu,
uwazi, weledi na kujiwekea malengo ya kujipima mwaka hadi mwaka ili
muendelee kuwa tassisi ambayo watu watakuja kujifunza kwenu”,
amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Naye Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng. Patrick Mfugale amemhakikishia
Waziri Mbarawa kuwa TANROADS imejipanga kuhakikisha miradi ipatayo 90
ya ujenzi wa barabara inayoendelea nchini kote inakamilika katika ubora
unaotakiwa na unao uwiana na thamani ya fedha.
Aidha, Waziri Prof. Mbarawa amemuagiza Meneja wa Wakala wa Majengo
nchini (TBA), mkoa wa Arusha, Bw. Victor Baltazar kukusanya madeni yote
kwa haraka ili kukamilisha miradi ya ujenzi wa nyumba za wafanyakazi na
za biashara inayosimamiwa na Wakala huo mjini Arusha kukamilika kwa
wakati.
Prof. Mbarawa ambaye yuko katika ziara ya mikoa ya kanda ya
kaskazini amezitaka taasisi zilizo chini wa wizara hiyo kuhakikisha
zinafanya kazi kibiashara ili kuboresha mapato ya Serikali na hivyo
kuiwezesha Serikali kutoa huduma bora kwa wananchi.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
SHARE
No comments:
Post a Comment