Demokrasia yetu
imefungwa pingu
Julian
Msacky
UCHAGUZI
nchini Chad umemalizika na Rais Idriss Deby aliyeingia madarakani tangu mwaka
1990 ameendelea kushikilia nafasi hiyo kwa mwendo mdundo.
Tume ya
Taifa ya Uchaguzi ya Chad (CEN) ilisema Rais Deby alipata asilimia 60 ya kura
na mpinzani wake, Saleh Kebzabo aliambulia asilimia 12 ya kura.
Kwa mujibu tume
hiyo idadi ya wapiga kura katika uchaguzi huo wa Aprili 10 ilikuwa milioni
sita.
Kama kawaida
ya chaguzi nyingi za Afrika, matokeo yaliyompa ushindi Rais Deby yalipingwa vikali
na wapinzani, akiwemo Kebzabo.
Miongoni mwa
malalamiko ya wapinzani ni kwamba kura zilichakachuliwa kwani mamia ya
masanduku ya kura yalipotea, hivyo uchaguzi haukuwa huru na haki.
Hiki ni
kilio cha muda mrefu kutoka wapinzani waliopo katika Bara la Afrika. Swali ni
je, ni kweli wanachezewa mchezo mchafu au wanaamua tu kudeka?
Hii ni mada
ya kujitegemea, hivyo leo tuendelee kujadili mada yetu ya viongozi kusigina
demokrasia.
Wakati
wapinzani wakilalamikia ushindi wa Rais Deby anayetokea Chama cha Patriotic
Salvation Movement (MPS), Umoja wa Afrika (AU) ulisema ulikuwa huru.
Ninachotaka
kusema hapa ni kuwa tangu Afrika ikumbatie mfumo wa vyama vingi, hakuna
uchaguzi uliofanyika bila malalamiko au vurugu.
Tumeona na
kushuhudia namna chaguzi zetu zinavyogubikwa na utata, zikiwemo vurugu,
umwagaji damu, raia kukimbia nchi na mengine mengi.
Hii ina
maana gani kwa Afrika? Maana yake ni kuwa tulikubali kupokea mfumo wa vyama
vingi kwa shingo upande ili kufurahisha wanaotupatia misaada.
Katika
mazingira hayo hakuna kiongozi anayeangalia ameingia madarakani kwa kura halali
au kwa kuua ili mradi tu aingie Ikulu kwa gharama yoyote.
Kwa lugha
nyingine ni kuwa demokrasia katika chaguzi zetu inakuwa haina mwenyewe na
badala yake mabavu na kejeli ndizo hutawala chaguzi zetu.
Ndiyo maana
demokrasia katika nchi za Afrika ni kana kwamba imefungwa pingu ili kuruhusu
wanasiasa uchwara na wababaishaji waendelee kutamba.
Tunadhani ni
muda muafaka sasa kuruhusu demokrasia ifanyekazi badala ya kushikilia viongozi madarakani
kwa silaha nzito nzito kana kwamba tupo vitani.
Viongozi
wetu ni lazima wafahamu kuwa wananchi wamechoshwa na tabia ya kuchezea
demokrasia kwani madhara yake yameonekana wazi wazi barani kwetu.
Badala ya
kutumia muda wetu kufanya shughuli za maendeleo tunapoteza nafasi kubwa
kujadili namna ya kurejesha amani iliyovurugwa na uchaguzi.
Katika bara
letu hakuna mwenye uhakika uchaguzi unapomaliza kama watu wataendelea kuwa na
amani au wataamshwa nyumbani na milipuko ya risasi.
Mathalan,
kumalizika kwa uchaguzi wa Chad hakuna mwenye kujua kama amani na utulivu
utakuwepo au la maana wapinzani bado wana kinyongo moyoni.
Aliyekuwa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Dk Koffi Annan aliwahi kusema chimbuko la
migogoro barani Afrika ni demokrasia duni.
Hii ikiwa na
maana kuwa Afrika imepanda demokrasia yake kwenye mwamba. Kwa msingi huo
haistawi zaidi ya kuendelea kudumaa miaka nenda rudi.
Demokrasia
duni inatokana na uongozi dhaifu (weak leadership) na mifumo legelege ambayo
imegharimu mengi katika Bara la Afrika.
Pengine ni
kutokana na udhaifu huo viongozi wa Afrika walikutana tena nchini Senegal ili
pamoja na mambo mengine kujadili namna ya kuimarisha demokrasia.
Akizungumza
kuhusu demokrasia, aliyewahi kuwa Rais wa Nigeria, Olusegun Obasanjo aliwataka
watawala kuandaa mazingira ya upatikanaji wa demokrasia.
Anachosema
Obasanjo ni kuwa watawala wa Afrika wamechezea mno demokrasia na sasa ni muda
muafaka wa kuhakikisha tunairejesha (to retrieve).
Obasanjo
anasema ni muhimu kufanya hivyo kwa ustawi wa vijana wa sasa na vizazi vijavyo,
ingawa alisema demokrasia ina hatua.
Bila
kumumunya maneno ni lazima tukiri kuwa viongozi wetu wanatakiwa kubadilika.
Kama kweli ni wafuasi wa demokrasia yanayotokea leo Afrika tusingeyaona.
Kwa mfano,
angalia namna ulafi wa madaraka unavyosababisha viongozi wetu wachezee katiba
za nchi wanavyotaka kana kwamba ni nguo zao.
Tuwaelewe
vipi wanapobadilisha katiba ili tu wasalie madarakani badala ya kuheshimu
zilizopo? Ni lipi jema la kuiga kutoka kwa viongozi wa aina hiyo?
Kinachosikitisha
ni kuwa kadiri siku zinavyosogea ndivyo viongozi wetu wa zama hizi za
utandawazi wanavyochezea katiba na kimsingi hawajali.
Tuseme
imetosha. Afrika inahitaji demokrasia ya kweli ili kuharakisha maendeleo ya
nchi zilizopo katika bara hilo na si vinginevyo kwani wamechoka na umaskini.
Wananchi wa
bara hilo wana kiu ya kuona haki za binadamu zinaheshimiwa. Nje na hapo viongozi
wanaotundika demokrasia msalabani hawatufai.
SHARE
No comments:
Post a Comment