
Chama
tawala nchini Uturuki Jumapili (22.05.2016)kimemthibitisha mshirika
anayeaminiwa na Rais Receyp Tayyip Erdogan kuwa mwenyekiti wake mpya na
kufunguwa njia ya kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo.
Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Binali Yildimir amepata kura 1,405 kati ya
1,470 za wajumbe wa chama tawala cha Haki na Maendeleo (AKP)
waliohudhuria mkutano wa dharura wa chama hicho.
Yildimir
mwenye umri wa miaka 60 ambaye ni mwanachama muasisi wa chama hicho sasa
atachukuwa nafasi ya Waziri Mkuu Ahmet Davutoglu ambaye mapema mwezi
huu alitangaza kujiuzulu kutokana na kutofautiana na Rais Erdogan.
Yildirim
ambaye amegombea uongozi wa chama hicho bila ya kuwa na mpinzani
anatagemewa kukubaliana zaidi na Erdogan ambaye anashinikiza mabadiliko
makubwa ya katiba ambayo yatampa madaraka makubwa ya utendaji rais cheo
ambacho ni cha heshima tu nchini Uturuki.
Kwa jadi
wadhifa wa waziri mkuu nchini uturuki unakwenda kwa kiongozi wa chama
kikubwa bungeni na Erdogan anatarajiwa kumtaka rasmi Yidrim aunde
serikali mpya.
Erdogan amwagiwa sifa
Katika
hotuba yake kabla ya kupigiwa kura Yildirim ametowa heshima zake kwa
Erdogan kwa kusema kwamba "siku zote tumekuwa na fahari kusema kwamba
sisi ni washirika wa Erdogan, hatima yetu ni moja na shauku yetu ni
moja.Ameongeza kusema kwamba "Bw. Rais tunakuahidi kwamba shauku yako ni
yetu, mapambano yako yatakuwa yetu na njia yako itakuwa yetu."
Pia
ameapa kutowa ushirikiano wake katika kuanzisha katiba mpya kwa kubadili
mfumo wa kisiasa nchini Uturuki kuwa ule wa urais kuifanya hali ambayo
ípo hivi sasa nchini humo kuwa ya kisheria.
Mapema
katika ujumbe uliosomwa wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Erdogan kwa
mara nyengine tena amesisitiza haja ya kuwepo kwa katiba mpya na mfumo
mpya wa serikali na kusema kwamba anataraji huko mbele kutafanyika
masahihisho ya mfumo wa sasa wa utawala wenye mkorogo. Wajumbe na
maafisa wa chama walisimama wakati hotuba yake ikisomwa.
Erdogan
amesema "Uhusiano wangu wa kisheria na chama cha AKP yumkini ukawa
umemalizika siku alipokula kiapo cha urais lakini uhusiano wake wa
mapenzi na chama hicho haukumalizika na katu hautomalizika"
Yidirim apongezwa na kukosolewa
Wafuasi
wa Yidirim wanampongeza kwa dhima yake ya kuendeleza miradi mikubwa ya
miundo mbinu ambayo imesaidia kuuchangamsha uchumi wa Uturuki na
kuongeza umashuhuri wa chama cha AKP.Lakini wakosoaji akiwemo kiongozi
wa chama kikuu cha upinzani wanamtuhumu kwa rushwa madai ambayo
yanakanushwa na Yidirim.
Mabadiliko
ya uongozi wa chama hicho yanakuja wakati nchi hiyo mwanachama wa
Jumuiya Kujihami ya NATO ikikabiliwa na vitisho mbali mbali vya usalama
ikiwa ni pamoja na kuanza upya kwa mzozo na waasi wa Kikurdi kusini
mashariki mwa nchi hiyo, wimbi la mashambulizi ya kujitowa muhanga ya
wanamgambo wa Kikurdi na Dola la Kiislamu halikadhalika kuongezeka kwa
taathira kutokana na vita katika nchi jirani ya Syria.
Davutoglu
ambaye aliwahi kuwa mshauri wa Erdogan na waziri wa zamani wa mambo ya
nje alitafautina na rais katika masuala mbali mbali ikiwa ni pamoja na
uwezekano wa kuwa na mazungumzo ya amani na waasi wa Kikurdi na kesi ya
waandishi wa habari wanaotuhumiwa kwa upelelezi na wanataaluma
wanaotuhumiwa kuunga mkono ugaidi.
Katika
hotuba yake ya kuaga Davutoglo amesema kujiuzulu halikuwa takwa lake
lakinin alikubali kufanya hivyo kudumisha umoja wa chama. DW(P.T)
SHARE
No comments:
Post a Comment