Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Ahmada Abdalla Khamis akisalimiana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya kula kiapo cha ahadi ya uadilifu Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa wa Jeshi la Polisi waliopandishwa vyeo vya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) na Naibu Kamishna wa Polisi DCP mara baada ya kula kiapo cha ahadi ya uadilifu Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa wa Jeshi la Polisi waliopandishwa cheo cha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) mara baada ya kula kiapo cha Maadili ya Watumishi wa umma Ikulu jijini Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwagaia vitafunwa wageni mbalimbali waliofika Ikulu kwa ajili ya kushuhudia Maafisa wa Polisi walipondishwa vyeo wakati wakila kiapo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwagaia vitafunwa baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria tukio hilo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza
viongozi wa Jeshi la Polisi Tanzania kuwaondoa watumishi wote wasiokuwa
askari polisi na ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya ukiukwaji
wa taratibu na ufujaji wa fedha za umma ili kulinda heshima, nidhamu na
uadilifu ndani ya jeshi hilo.
Rais
Magufuli ametoa maelekezo hayo leo tarehe 18 Julai, 2016 muda mfupi
baada ya Naibu Makamishna wa Polisi 25 na Makamishna Wasaidizi
Waandamizi wa Polisi 35 kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma,
Ikulu Jijini Dar es salaam.
Pamoja
na kutoa agizo la kutaka wasio askari polisi kuondolewa katika utumishi
wa jeshi la polisi, Rais Magufuli pia ameagiza jeshi hilo lichukue
hatua dhidi ya wote wanaokabiliwa na tuhuma za wizi wa fedha wakiwemo
wanaodaiwa kuiba mabilioni ya shilingi zilizotolewa kwa ajili ya ununuzi
wa sare za askari mwaka jana 2015.
"Mnajua kupeleleza, mna vyombo vyote, ofisi ya IGP (Inspekta Jenerali wa Polisi)ipo palepale, ofisi ya DCI (Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai) ipo palepale, Makamishna wote mnazunguka mnakwenda palepale, mwizi mnae palepale, mnashindwa kumshika.
"Kama
mnafikiri kuwa na raia katika jeshi la polisi wanawaharibia kazi zenu
hamisheni raia wote na wapelekeni utumishi, kwani hakuna mhasibu ambaye
ni askari polisi? hakuna mhandisi ambaye ni askari polisi? hakuna afisa
tawala ambaye ni askari polisi? Mimi nafikiri kama matatizo ya wizi na
wafanyakazi hewa yanaletwa na raia waliomo ndani ya jeshi la polisi na
majeshi yetu mengine, IGP kaorodheshe raia wote wanafanya kazi Jeshi la
Polisi ili waondolewe na tuwapangie kazi nyingine uraiani" Amesema Rais Magufuli.
Hata
hivyo Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri
linayofanya iliyoliwezesha kujenga imani kubwa kwa watanzania na ametaka
viongozi wa Jeshi hilo wawaongoze askari walio chini yao vizuri,
wawatie moyo na waache vitendo vya kuwakatisha tamaa kwa kuwaadhibu ama
kuwatisha pale wanapochukua hatua stahiki dhidi watu wanaovunja sheria.
"Sasa
mimi niwaombe nyinyi, wale wadogo mnaowaongoza mkawape mamlaka ya
kutimiza wajibu wao, hata kama ameshika gari la IGP liache lishikwe IGP
atakwenda kujieleza mwenyewe, hata akishika gari la RPC afanye
hivyohivyo, hata akishika gari la Waziri au gari la Rais mwacheni
atekeleze wajibu wake, sheria ni msumeno, tunawanyima nguvu hawa wa
chini wanapotimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria halafu unamwambia
liachie, ukifanya hivyo aliyeshikwa anatoka pale akiwa anatamba
kwelikweli na yule askari unamvunja nguvu ya kufanya kazi"Amesisitiza Rais Magufuli.
Rais
Magufuli pia amelitaka jeshi hilo kuungana na vyombo vingine vya
serikali katika kutekeleza shughuli zake zikiwemo kusimamia ukusanyaji
wa mapato ya serikali bandarini, katika sekta ya utalii na maeneo
mengine, kukabiliana na vitendo vya rushwa na kuondoa watumishi hewa.
Tukio
hili la Naibu Makamishna wa Polisi na Makamishna Wasaidizi Waandamizi
wa Polisi kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma limeongozwa na
Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Salome Kaganda na limehudhuriwa na
viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe.
Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala
Bora Mhe. Anjellah Kairuki, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe.
Hamad Yusuf Masauni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Mcheche
Masaju, Makatibu Wakuu na Viongozi wa vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
18 Julai, 2016
SHARE
No comments:
Post a Comment