Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Mhandisi Stella Manyanya (kulia) ambaye alikuwa mgeni rasmi akimwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akimkabidhi cheti mmoja wa Wahitimu wa Kidato cha Nne wakati wa Sherehe ya Mahafali ya Nne ya Kidato cha Nne Shule ya Sekondari Wama Nakayama iliyopo Wilayani Rufiji Mkoani Pwani 26 Novemba, 2016.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Mhandisi Stella Manyanya (katikati) ambaye alikuwa mgeni rasmi akimwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi wa Shule, wageni waalikwa pamoja na Wahitimu wa Kidato cha Nne baada ya kumalizika Sherehe ya Mahafali ya Nne ya Kidato cha Nne Shule ya Sekondari Wama Nakayama iliyopo Wilayani Rufiji Mkoani Pwani 26 Novemba, 2016.
Mwenyekiti wa Shule ya Sekondari ya Wama Nakayama ambaye pia ni mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Salma Kikwete (kushoto) akimkabidhi zawadi mgenoi rasmi Mhe. Mhandisi Stella Manyanya wakati wa Sherehe ya Mahafali ya Nne ya Kidato cha Nne Shule ya Sekondari Wama Nakayama iliyopo Wilayani Rufiji Mkoani Pwani 26 Novemba, 2016.
PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM
Na Benedict Liwenga-WHUSM.
WANAFUNZI wa kike wametakiwa kuongeza bidii katika masomo ya sayansi ili waweze kulisaidia Taifa katika kukabiliana na baadhi ya changamoto hususani katika sekta ya afya.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Mhandisi Stella Manyanya wakati wa Mahafali ya Nne ya Shule ya Sekondari ya Wama Nakayama iliyopo Wilayani Rufiji Mkoani Pwani.
Katika Mahafali hayo, Mhe. Mhandisi Manyanya amewapongeza wahitimu wote na kuwaeleza kuwa, masomo yote yana umuhimu sawa lakini pale wapatapo fursa wasome kwa bidii masomo ya Sayansi kwani kwa sasa kuna changamoto mbalimbali zinazozikabili Taifa hususani katika sekta ya afya ambapo endapo mkazo ukitiliwa basi utasaidia kutatua baadhi ya changamoto hizo kama vile upungufu wa Wataalam wa masuala ya afya na hivyo kuweza kukabiliana na magonjwa mbalimbali.
Alisema kuwa, Serikali kwa sasa inajitahidi kuangalia maeneo yenye upungufu wa Wataalam mbalimbali ili iweze kutatua changamoto mbalimbali ambapo elimu bora inahitajika katika kuwapata wataalam watakaoweza kutatua mapungufu hayo ndiyo maana inajitahidi kutoa elimu bure kwa sasa na kuendelea kuhimiza wanafunzi kusoma kwa bidii hasa wasichana ili elimu itolewayo iwe sawa kwa wote pasipo ubaguzi na kuweza kumkomboa msichana.
“Pale mpatapo nafasi ya kusoma, jitahidini musome masomo ya sayansi kwasababu kwa sasa masomo hayo yana nafasi kubwa na ajira yake ni ya uhakika na hata katika upatikanaji wa Vyuo Vikuu wakati wa kuomba unakuwa ni rahisi lakini pia mkiyapenda masomo haya mtakuwa wataalam ambao mtalisaidia Taifa letu katika kutatua baadhi ya changamoto mbalimbali kama vile vifo vya akina mama na watoto, msife moyo kwa kuona kuwa ni magumu, someni kwa bidi siku zote”, alisema Mhandisi Manyanya.
Kwa upande wake Spika Mstaafu wa Bunge la 10 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Spika Anne Makinda amewataka wahitimu hao kutobabaishwa na wanaume ambao wanaweza kuwadanganya kwa kuwarubuni kwa pesa na vitu mbalimbali na kuwataka kutokubali kwa namna yoyote ile.
“Mkombozi wa Mwanamke ni elimu, mkisoma kwa bidii hata hakuna mwanaume atakayewachezea ama kuwababaisha kwa pesa au vitu alivyonavyo, hivyo msikubali kudanganyika”, alisema Mhe. Makinda.
Naye Mwenyekiti wa Shule hiyo ambaye ni Mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Salma Kikwete alisema kwamba, anajivunia maendeleo makubwa yaliyopigwa na yanayoendelea kupigwa katika shule hiyo na ni kwa mara ya nne kwa wanafunzi wa kidato cha nne kuhitimu katika shule hiyo huku akiwataka wahitimu kuyafanyia kazi yale yote mazuri waliyojifunza wakati wa masomo yao.
Ameipongeza Serikali kwa ushirikiano mkubwa iliyoutoa kwa wanafunzi na pia wadau mbalimbali waliojitoa kwa moyo katika kusaidia uwepo wa shule hiyo lakini pia amewapongeza Walimu na wafanyakazi na wanafunzi wote kwa ujumla kwa kazi nzuri iliyofanikisha kung’ara kwa shule hiyo katika taaluma hususani katika Wilaya ya Rufiji.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Mwl. Mwajuma Buguji alisema kwamba shule hiyo inapokea wanafunzi wa kike toka Wilaya na Mikoa yote ya Tanzania Bara pamoja na Visiwani ambapo wanafunzi wamegawanyika katika makundi mawili, wenye wazazi wote wawili ambao maisha yao duni, wenye wazazi mmoja na maisha yao ni duni na wengine ni yatima ambao maisha yao ni hatarishi.
Aidha, alisema kwamba wanafunzi hao kwa sasa wanapata ufadhili mkubwa toka Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) ambapo hapo awali katika miaka ya nyuma baadhi ya wanafunzi waliojiunga na shule hiyo walichangia kiasi kidogo.
“Kwa sasa shule yetu ina jumla ya wanafunzi 378 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita na leo wanahitimu wanafunzi 79, tunao wafanyakazi Walimu 26 na wasiokuwa walimu 13 na shule yetu inapiga hatua nzuri kimasomo kwa kuongoza Kiwilaya na kuchukua nafasi nzuri Kitaifa, alisema Mwl. Mwajuma.
Shule ya Wama Nakayama ilianzishwa mwaka 2010 na shule hiyo imetokana na majina mawili yaani WAMA pamoja na NAKAYAMA ambapo neno WAMA linasimama kama Taasisi ya Wanawake na Maendeleo na NAKAYAMA linasimama kama jina la mdau wa kwanza kuisaidia shule hiyo kwa kutoa msaada wa ujenzi ambaye ni Mfanyabiashara mkubwa toka nchi ya Japan.
SHARE
No comments:
Post a Comment