Na Benny Mwaipaja, WFM, Songwe.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda,
amewaonya mawakala wa forodha katika mpaka wa Tanzania na Zambia wa
Tunduma/Nakonde kuacha Mara moja tabia ya kuwachelewesha madereva wa
malori yaendayo masafa marefu kwa makusudi ili wapewe rushwa.
Prof.
Mkenda ametoa onyo hilo katika mpaka huo wa Tunduma na Nakonde, baada
ya kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya madereva wa malori waliodai
wamekuwa wakicheleweshwa kuvuka mpaka huo kwa zaidi ya siku tatu hadi
tano.
Wadereva
hao wameeleza kuwa mawakala wa forodha wamekuwa wakiwaambia kuwa
nyaraka zao zinazohusika na mizigo wanayosafirisha zimekuwa
zilicheleshwa na kituo cha Forodha upande wa Zambia.
Hata
hivyo Meneja wa Mamlaka ya Mapato Zambia (ZRA), Kituo cha Nakonde, Bw.
Nase Lungu, amekana kuhusika na ucheleweshaji huo na baada ya ukaguzi wa
moja ya nyaraka hizo ilibainika kuwa upande wa Zambia unatoa nyaraka
hizo kwa wakati lakini zimekuwa zikifichwa na Mawakala wa Forodha upande
wa Tanzania.
Wakitoa
ufafanuzi wa tuhuma hizo, madereva hao wamesema kuwa mawakala wa
forodha kwa muda mrefu wamekuwa wakiwaeleza kuwa mtandao wa intaneti wa
Upande wa Zambia unaotumika kuchakata nyaraka zao uko chini, hivyo
walitakiwa kutoa shilingi 10,000 kwa kila nyaraka ili “kurahisisha” kazi
hiyo kwa kuwapa kitu kidogo maafisa wa forodha wa Zambia.
“Mawakala
wengine wa forodha wana nyumba zao za kulala wageni hapa Tunduma kumbe
wanatulazimisha kukaa hapa ili tulale kwenye nyumba hizo hali inayotutia
hasara na wanatumia kutokujua kwetu kutudanganya kwamba mtandao uko
chini wakijua hatuna uwezo wa kufuatilia huko Zambia” alieleza kwa
masikitiko dereva mmoja
Baada
ya kubaini uwepo wa vitendo hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda,
Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda, ameagiza Mamlaka ya Mapato
Tanzania TRA upande wa Tunduma kuandika kibao chenye namba za simu za
Mkuu wa TRA mpakani hapo zitakazotumiwa na madereva wanaocheleweshwa kwa
makusudi kutoa malalamiko yao.
“Tunataka
madereva mtumie siku moja tu kukamilisha nyaraka zenu ili muendelee na
safari yenu vinginevyo tutadumaza biashara kati ya Zambia na Tanzania na
pia tutaifanya Bandari yetu ya Dar es salaam kushindwa kuleta tija”
aliongeza Prof. Mkenda
Alisema
kuwa wakala wa forodha atakayebainika kufanya mchezo huo mchafu wa
kuwarubuni madereva na kuwachelewesha kupeleka mizigo nchini Zambia,
watanyang’anywa leseni zao za biashara.
Meneja
Msaidizi wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, mikoa ya Songwe na
Mbeya, Bw. Jomimassa Nsindo, amesema kuwa ofisi yake itashirikiana na
madereva kukomesha vitendo hivyo ambavyo amesema vinaharibu uchumi na
biashara mpakani hapo.
Naye
Mkuu wa wilaya ya Momba, mkoani Songwe, Bw. Juma Irando, alisema kuwa
ataitisha kikao cha Madereva, Mawakala wa Forodha na Mamlaka ya Mapato
Tanzania TRA katika Mpaka huo wa Tunduma/Nakonde mapema, ili kuweka
msimamo wa serikali na kuwaeleza wahusika wanaokiuka taratibu hatua
watakazochukuliwa.
Prof.
Mkenda na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina
Khamis Shaaban, walikwenda katika mpaka huo wa Tunduma na Nakonde,
kuangalia maandalizi ya uanzishwaji wa Kituo cha Pamoja cha Mpakani kati
ya Tanzania na Zambia, unaotarajiwa kuanza Februari mosi, 2017, baada
ya kusainiwa kwa mikataba kati ya nchi hizo mbili, juzi.
SHARE
No comments:
Post a Comment