Mh mkuu
wa mkoa wa Arusha Mrisho Mashaka Gambo amefanya ziara katika chuo kikuu
cha Arusha. Katika ziara hiyo Mkuu wa mkoa amezungumza na uongozi wa
chuo,watumishi pamoja na wanafunzi.
Pia alipata fursa ya kutembelea miundo mbinu mbali mbali ya chuo hicho ambacho kinamilikiwa na kanisa la Waadventista Wasabato.
Alipata
muda wa kuzungumza na wanafunzi na kusikiliza kero zao na changamoto
zinazowakabili ikiwemo kutokuridhishwa na huduma zinazotolewa na mfuko
wa Bima ya Afya katika utoaji wa kadi za Bima ya Afya hivyo kusababisha
usumbufu mkubwa wakati wa utoaji wa huduma hiyo chuoni hapo.
Masuala
mengine ni kama tatizo la kukatika umeme mara kwa mara, tatizo la maji,
ulinzi na usalama chuoni hapo, sehemu kubwa ya wenye sifa ya kukopeshwa
na bodi ya mikopo kutokuipata mikopo hiyo, pia wamemweleza hofu yao ya
kumaliza masomo na kukosa ajira.
Katika
kujibu changamoto hizo mkuu wa mkoa ameuagiza uongozi wa NHIF (bima ya
Afya) mkoa wa Arusha kufika chuoni hapo mara moja ili kuweza kulitatua
tatizo hilo ndani ya wiki moja toka leo.
Mkuu wa
mkoa ametoa maagizo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru, mkuu wa
wilaya ya Arumeru Ndg. Alexander Mnyeti na Mhandisi wa maji wilaya ya
Arumeru kufika chuoni hapo siku ya Jumatano tarehe 01/02/2017 na kukaa
na uongozi wa chuo kuona namna wanaitatua kero hiyo ya maji ya muda
mrefu.
Kuhusiana
na suala la ulinzi chuoni hapo na maeneo ya jirani Mh. Mkuu wa mkoa
ameihamasisha jamii nzima ya Arumeru bila kuwasahau wanachuo wenyewe
kuona namna gani wanaweza kujenga kituo cha polisi ili kuimarisha
usalama chuoni hapo na maeneo ya jirani, kwa kuanzia Mh. Gambo ametoa
mabati 100 ili kuamsha ari ya wananchi na jamii nzima ya Arusha
University kuanza ujenzi huo mara moja.
Mh. Gambo
ameichukua hoja ya wanafunzi walio na sifa za kukosa mkopo na kuagiza
uongozi wa chuo kumpa majina ya wanafunzi husika na ofisi yake
kuyawasilisha bodi ya mikopo ili yashughulikiwe, pia ametoa changamoto
kwa vyuo kutoa kozi kulingana na mahitaji ya serikali kwa wakati husika
ili kuepusha mgogoro wa kuwa na wahitimu wengi wasio na ajira.
Vile vile
katika kujibu baadhi ya changamoto Mh Gambo aliwapongeza wanafunzi kwa
ujasiri wa kutoa kero zao bila woga na ameahidi ataweka utaratibu wa
kutembelea vyuo vikuu vilivyopo mkoani Arusha ili kujua mazingira halisi
na matatizo yanayokabili vyuo husika.(P.T)
SHARE
No comments:
Post a Comment