JPCC kati ya Tanzania na Malawi ni chachu ya kuimarisha mahusiano
Wajumbe
wanaoshiriki katika Kikao cha 4 cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya
Ushirikiano (JPCC) kati ya Tanzania na Malawi kilichofunguliwa leo
jijini Lilongwe, Malawi wamehimizwa katika majadiliano yao ya siku tatu
kubuni mkakati utakaowezesha kutatua changamoto zinazojitokeza kutokana
na muingiliano mkubwa wa ngazi mbalimbali za ushirikiano baina ya
wananchi wa mataifa hayo mawili.
Kauli
hiyo imetolewa na Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania katika ngazi ya
Wataalam, Balozi Ramadhan Mwinyi ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alipokuwa
anasoma hotuba ya ufunguzi.
"Kama
mnavyofahamu kunapokuwa na maingiliano makubwa ya wananchi wa nchi mbili
kama zilivyo nchi zetu, changamoto haziwezi kukosa kujitokeza. Hivyo ni
jukumu letu sisi wataalamu kubuni mkakati wa kuhakikisha kuwa
changamoto hizo zinashughulikiwa haraka iwezekanavyo".
Balozi
Mwinyi alieleza kuwa kikao hicho ni fursa nzuri kwa Serikali za
Tanzania na Malawi kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya
nchi zao katika maeneo tofauti ikiwemo uchumi, uwekezaji, biashara,
kutunza mazingira, elimu, Tehama, kilimo, uhamiaji, uchukuzi na masuala
ya ulinzi na usalama, Hivyo alihimiza wajumbe wa pande zote mbili kuwa
wabunifu katika majadiliano yao ili watoke na mipango inayotekelezeka
kwa kuwa wananchi wanachohitaji ni maendeleo na sio mikakati inayoishia
katika makabrasha.
Aidha,
Balozi Mwinyi aliekeza kuwa watu wengi walistaajabu kusikia ujumbe wa
Tanzania unakuja Malawi kushiriki kikao hiki kama walivyostaajabu kuona
Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipofanya mazungumzo hivi karibuni
na Rais wa Malawi, Mhe. Prof. Peter Mutharika pembezoni mwa Mkutano wa
Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa, Ethiopia. Alisema
hakuna cha kustaajabisha hapo, isipokuwa ifahamike lengo kuu la pande
zote mbili ni kuona uhusiano kati ya Tanzania na Malawi unaimarishwa na
kwamba mkutano huo ni ushahidi kuwa nchi hizi mbili zipo karibu zaidi
kuliko hapo awali.
Naibu
Katibu Mkuu aliihakikishia Serikali ya Malawi kuwa Serikali ya Tanzania
imedhamiria kushirikiana na nchi hiyo katika kuboresha mahusiano ya
kidiplomasia, uchumi na kijamii, hivyo alisisitiza umuhimu wa yale yote
yatakayoafikiwa katika mkutano huo yanatekelezwa katika muda uliopangwa.
Alishauri iundwe timu ya ngazi ya Makatibu Wakuu ambayo itakuwa
inakutana kila baada ya miezi sita kutathmini utekelezaji wa maazimio ya
kikao hicho.
Kwa
upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Malawi, Dkt.
Dalitso Kabambe alisisitiza umuhimu wa nchi hizi mbili kuweka mikakati
itakayorahisisha wananchi kufanya biashara bila vikwazo. "Bisahara ni
jambo muhimu lazima tuhakikishe kuwa Serikali zetu zinaweka mazingira
mazuri ili wananchi wafanye biashara kwa wepesi".
Kikao
hicho kinatarajiwa kufungwa rasmi na Mawaziri wa Mambo ya Nje siku ya
Jumapili tarehe 05 Februari 2017 ambapo Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anatarajiwa kuwasili
Malawi tarehe 04 Februari 2017. Mawaziri hao pia wataweka saini Mikataba
mitatu ya ushirikiano katika mashauriano ya kisiasa na kidiplomasia,
usafiri wa anga na utalii.
Wajumbe
wa Tanzania katika kikao hicho wanatoka katika sekta mbalimbali
wakiwemo wajumbe kutoka mikoa miwili ya Mbeya na Ruvuma inayopakana na
Malawi ambao wanaongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Amos Makalla.
Imetolewa na: Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Malawi na Mwenyekiti Mwenza wa Kikao
cha JPCC kati ya Tanzania na Malawi, Dkt. Kalitso Kabambe akisoma hotuba
ya iufunguzi na ukaribisho.
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi akisoma houtuba ya ufunguzi wa kikao
cha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPCC) kati ya Tanzania na Malawi.
Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Malawi, Dkt. Dalitso
Kabambe. Kikao hicho kinafanyika Lilongwe, Malawi kwa muda wa siku tatu
kuanzia tarehe 03 Februari 2017.
Wajumbe
wa Tanzania wakisikiliza hotuba za Makatibu Wakuu. Kutoka kushoto ni
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Amos Makalla, Mkurugenzi Msaidizi kutoka
Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Suleiman Salehe na Kaimu Mkurugenzi kutoka
Mamlka ya Viwanja vya Ndege.
Sehemu
nyingine ya ujumbe wa Tanzania. Kutoka kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga, Afisa kutoka Wizara
ya Mambo ya Nje, Bw. Ali Ubwa na mjumbe mwingine ambaye jina lake
halikupatikana.
Bw. Kalitso Kabambe akiwa na Balozi wa Malawi nchini Tanzania.
Sehemu ya ujumbe wa Malawi ukifuatilia hotuba za ufunguzi
Wajumbe wa pande zote mbili wakiwa katika kikao cha JPCC
Naibu Katibu Mkuu, Balozi Mwinyi akihojiwa na Mwandishi wa TBC, Bw. Hosea Cheo
Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Victoria Mwakasege akihojiwa na Mwandishi wa TBC
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Amos Makalla akifanya mahojiano na Mwandishi wa TBC
SHARE
No comments:
Post a Comment