MWITO umetolewa kwa jamii ya watanzania kuacha mila potofu inayopelekea tabia ya baadhi ya wazazi kuwaficha watoto wenye matatizo mbalimbali hasa tatizo la kichwa kikubwa na mgongo wazi bali wawapeleke hospitali mapema ili wapate matibabu kwani wanaweza kupona endapo wakiwahishwa hospitali.
Mwito ulitolewa na Ofisa Mawasiliano mwandamizi wa Hospitali ya Mifupa (MOI) Bi. Mary Ochieng, wakati akitoa maelezo kwa wafanyakazi wa kampuni ya simu ya Halotel walipotembelea wodi za watoto hao pamoja na kutoa misaada ya kijamii, akizungumza na wafanyakazi hao Ochieng, amesema kuwa licha ya Taasisi hiyo kufanya jitihada kubwa za kutoa elimu na kufanya upasuaji kwa watoto hao bure bado kuna baadhi ya wazazi wameendelea na tabia ya kuwaficha watoto wao.
Wafanyakazi wa kampuni ya simu ya Halotel wakiwa katika picha ya pamoja nje ya wodi ya watoto ya Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI) kabla ya kutoa zawadi ya Pasaka kwa watoto hao.
"Tangu Taasisi yetu ichukue jukumu hili imefanya kazi kubwa sana, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali tumeweza kutoa matibabu kwa watoto wengi, ila changamoto kubwa bado inabaki kwa baadhi ya wazazi ambao wanawaficha watoto wao pale inapotokea wakagundua watoto wao wana matatizo ya vichwa vikubwa au mgongo wazi” Alisema nakuongeza.
“Bado changamoto ziko nyingi sana ndani ya jamii ya Watanzania, Kwanza wanawaficha watoto hawa, lakini pia wanawake wanao jifungua watoto wenye matatizo wakati mwingine wananyanyaswa na wanaume wao au hata ndugu kutokana na mila potofu zilizo ndani ya jamii yetu, sio jambo jema, na sio sahihi kabisa ni lazima watoto wote wapewe haki sawa ya kuhudumiwa kwani tunayo mifano ya watoto wenye matatizo haya na wameweza kupata matibabu na sasa wanaendelea na masomo yao kama watoto wengine na pia wana ndoto kubwa” Alisema Ochieng.
Aidha ofisa huyo aliiomba, Kamnpuni hiyo kuangalia namna ambavyo wanaweza kushirikiana na taasisi hiyo katika kutoa elimu na kusaidia kuchangia gharama za matibabu kwa watoto na wazazi wenye matatizo hayo kwani wengine wanatoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam na inakuwa vigumu wao kumudu gharama za maisha wanapokuwa wanapokea matibabu.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Nguyen Van Son, alieambatana na wafanyakazi wa kampuni hiyo amesema licha ya wao kutoa msaada wa vitu mbalimbali katika sikuu ya pasaka, kwa Pamoja kampuni yake itakaa na wataalam wa taasisi hiyo ili kuangalia namna gani wanaweza kuwasaidia wagonjwa hao ikiwa ni pamoja na kufanya kampeni ya kitaifa kusaidia kukabiliana na tatizo hilo.
“Tumeguswa na tatizo hili hatutaishia kutoa misaada hii midogo ya kijamii, na kuishia hapo lazima tuangalie kwa upana namna ambavyo tunaweza kuisaidia serikali na jamii ya Kitanzania kupambana na tatizo hili kadri tutakavyo weza,” Alisema Son.
SHARE
No comments:
Post a Comment