Baraza
la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) ni chombo kilichoanzishwa kwa
sheria ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi, Sura 129, ili kusimamia na
kuratibu utoaji wa mafunzo ya elimu ya ufundi nchini. Sheria hii
inazitaka Taasisi zote zinazotoa elimu ya ufundi kusajiliwa kabla ya
kuanza kuendesha mafunzo yoyote. Baraza pia huidhinisha mitaala kabla
haijaanza kutumika. Hivyo
taasisi zote haziruhusiwi kuanza kutoa mafunzo yoyote bila kibali
maalumu kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).Baraza
linapenda kuwataarifu wadau wa sekta ya Mafunzo ya Ufundi na Umma kwa
ujumla kuwa udahili na uchaguzi wa wanafunzi kwa ajili ya masomo ya
Astashahada na Stashahada mbalimbali yanayotolewa na vyuo vyote hapa
nchini, utafanyika moja kwa moja vyuoni, isipokuwa kozi za afya na
ualimu zinazotolewa na vyuo vya Serikali tu. Hivyo maombi yote ya nafasi
za masomo yatumwe kwenye chuo husika.
Udahili
wa kozi za Afya na Ualimu katika vyuo vya Serikali utaratibiwa na
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto; na Wizara
ya Elimu, Sayansi na Tekinolojia kwa kushirikiana na Baraza (NACTE).
Hivyo maombi ya Udahili kwa kozi za Afya na Ualimu kwa vyuo vya serikali
tu yatumwe kwa njia ya mtandao kupitia tovuti ya NACTE (www.nacte.go.tz)
au kupitia vyuo husika vya Afya na Ualimu ambavyo vitashughulikia
maombi hayo na kufanya udahili kwa njia ya mtandao kupitia
‘Institutional Panel’ zao.
Aidha
vyuo vyote vitatangaza au kuwafahamisha moja kwa moja waombaji majina
ya watakaochaguliwa kujiunga na kozi mbalimbali; na wale wa kozi za Afya
na Ualimu watatangazwa na Wizara husika na kupitia tovuti ya NACTE.
Baraza
linapenda pia kuwafahamisha kuwa Vyuo vitaanza kupokea maombi ya
udahili wa wanafunzi kuanzia tarehe 15 Mei, 2017 hadi tarehe 20 Agosti,
2017. Majina ya waliochaguliwa yatatangazwa tarehe 14 Septemba, 2017.
Masomo kwa mwaka wa masomo 2017/2018 yanatarajiwa kuanza rasmi tarehe 25
Septemba, 2017.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA KATIBU MTENDAJI
BARAZA LA TAIFA LA ELIMU YA UFUNDI (NACTE)
TAREHE: 10/05/2017
SHARE
No comments:
Post a Comment