Mjamzito
akipoteza
maisha
nani anajali?
Julian Msacky
MJAMZITO mmoja akipoteza maisha au mtoto wake
wakati wa kujifungua ni watu wachache wanaonekana kujali au kuguswa na kilichotokea.
Watu wengi huona tukio hilo la kawaida.
Ndiyo maana huwezi kusikia serikali ikipiga kelele
linapotokea tukio la aina hiyo na hata ikifanya hivyo inakuwa ni mara chache.
Si hivyo tu, hata wauguzi hawaoneshi kusononeshwa. Ni business as usual!.
Hii ni hatua mbaya. Ni lazima viongozi waoneshe kuguswa
pale taifa linapopoteza raia wake kwa sababu zinazozuilika.
Ni lazima tujenge utamaduni huo kwani uhai wa mtu
una thamani kubwa. Uhai wa mtu haununuliwi, hivyo ni vizuri Serikali
kuhakikisha imeweka mfumo mzuri wa kumhudumia mjamzito.
Tuhakikishe hospitali, zahanati na vituo vya afya
vina wahudumu bora.Wahudumu wenye vitendea kazi vya kutosha.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu (katikati) akimfariji mtoto mchanga
Wahudumu wanaolipwa maslahi mazuri ili waweze
kuwahudumia wagonjwa na wajawazito.
Tuhakikishe hakuna mjamzito anayepoteza maisha.Tuhakikishe
mjamzito akifikishwa hospitalini anahudumiwa kwa ukaribu.
Anahudumiwa kwa lugha laini badala ya kutumia
kejeli na maneno mengine ya kuzidi kumtia uchungu mjamzito. Ndiyo.
Nchi zilizoendelea ni nadra mjamzito kupoteza
maisha wakati wa kujifungua. Ni nadra mtoto kupoteza maisha wakati wa kuzaliwa.
Kama nchi hizo zimeweza, kwa nini sisi kama nchi
tushindwe? Ni lazima tufanye kazi ya ziada ya kumlinda mama mjamzito.
Haiwezekani nchi kama yetu hadi leo tuendelee
kupoteza maisha ya mama na mtoto wakati wa kujifungua. Haiwezekani.
Kama tuna fedha za kujenga barabara, majumba
marefu yanayokaribia kugusa angani, ni kwa nini tushindwe kujenga hospitali
nzuri kila wilaya na zahanati bora kila kijiji au kata.
Kama tuna madini ya kila aina na yanachimbwa usiku
na mchana ni kwa nini tushindwe kumhudumia mama mjamzito ili aweze kuleta
kiumbe kipya dunia bila matatizo. Inawezekana. Tujipange.
Leo hii tunaambiwa nchi ina hazina kubwa ya gesi.
Ina hazina kubwa ya madini ya heliamu na mengine mengi. Ni kweli tumeshindwa
kutumia utajiri huo kuweka mazingira bora ya huduma za afya?
Kwa utajiri uliopo nchini tulitakiwa tuwe na
huduma nzuri za afya na wahudumu wenye weledi ili kuokoa maisha ya ndugu na
jamaa zetu ambao wanapoteza maisha kwa sababu zinazoepukika.
Mbali na huduma za afya hususan kwa wajawazito,
hatuoni sababu ya watoto wadogo kuendelea kuteseka kwa kukosa huduma muhimu
katika maisha yao hata kama wazazi wao hawapo.
Sisi kama nchi ni lazima tuweke mfumo mzuri wa kulinda
maisha ya watoto. Wale tunaoimba kila siku ni watoto wa mitaani tukiwawekea mazingira
rafiki wataondoka tu mitaani.
Ni suala la kujipanga. Kwa mfano, tukiwawekea
vituo pamoja na wasimamizi wa kuhakikisha wanawatunza na kuhakikisha wanapata
elimu, hivi hatutakuwa tumeondoa au kupunguza tatizo?
Kipi bora kuwaacha wanarandaranda mitaani au kuweka
mfumo wa kuondoa tatizo. Pamoja na mikakati ya aina hiyo kuna umuhimu wa kila mzazi
kutimiza jukumu lake.
Hii ikiwa na maana kuwa tusikwepe majukumu ambayo
tumeyataka wenyewe. Katika hili wanawake na wanaume wanaozurura na watoto wakiomba
huku wakiwa na nguvu za kufanya kazi, tusiwachekee.
Kama Rais John Magufuli anasema Hapa Kazi Tu ni
lazima watu wa aina hiyo wafanye kazi. Kama wenye ulemavu wanafanya kazi za
kujipatia riziki sembuse hao wenye nguvu zao!
Wakati tukitafakari hayo, tukumbuke pia kwamba
Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), limetoa ripoti ambayo viongozi
wetu ni lazima wakune vichwa na kuangalia namna ya kuwanusuru.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo watoto walio na umri
chini ya miaka mitano watafariki kutokana na sababu zinazozuilika kati ya sasa
na mwaka 2030.
Katika ripoti yake ya mwaka UNICEF imesema kwamba
kulingana na mwenendo wa hivi karibuni na makadirio ya ukuaji wa watu, watoto milioni
167 wataishi katika umaskini uliokithiri.
Si hivyo tu, bali watoto milioni 60 hawataweza
kuhudhuria elimu ya msingi na wanawake milioni 750 watakuwa katika ndoa kama
watoto ifikapo mwaka 2030.
Hii ina maana gani? Ina maana kuwa suala la usawa
lisiposhughulikiwa na nchi kuboresha afya na elimu kuna hatari ya kupoteza
viumbe hao.
Ripoti hiyo ilisema asilimia 80 ya vifo vinavyozuilika
vinatokea katika maeneo ya kusini mwa Asia na Jangwa la Sahara ambako ndiko
iliko Tanzania.
SHARE









No comments:
Post a Comment