Mkuu
wa Wilaya ya Ilala Bi. Sophia Mjema akizungumza hivi karibuni na Wadau
wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016/17.
Kwa Dar es Salaam, utafiti huu unatarajia kuanza mwishoni mwa mwezi Mei,
2017.
Na: Veronica Kazimoto.
Wito
umetolewa kwa Wananchi wote wa mkoa wa Dar es Salaam ambao kaya zao
zimechaguliwa kitaalam kwa ajili ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya
UKIMWI wa mwaka 2016/17 kutoa ushirikiano kwa wadadisi wataokusanya
taarifa za utafiti huo utakaofanyika mwishoni mwa mwezi Mei, mwaka huu.
Akizungumza
hivi karibuni katika Mkutano wa Wadau wa Utafiti huo jijini Dar es
Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Bi. Sophia Mjema amesema Utafiti huu ni
muhimu sana kwani husaidia kujua hali halisi ya ugonjwa wa UKIMWI na
hivyo kuongeza nguvu zaidi ya kuondokana na ugonjwa huo.
"Mimi
niwaeleze tu kwamba, utafiti huu ni muhimu sana katika mkoa wetu wa Dar
es Salaam kwa kuwa utatusaidia kujua hali halisi ya maambukizi ya VVU
na hatimaye kupata nguvu zaidi za kuondokana na ugonjwa huu, hivyo
nawaagiza kusimamia zoezi hili na kuwahimiza Wananchi wote ambao kaya
zao zimechaguliwa kutoa ushirikiano kwa wadadisi watakaofanya taarifa za
utafiti huu", amesema Mjema.
Mkurugenzi
Msahauri, Dkt. Cecilia Makafu kutoka Shirika la ICAP Tanzania
akiwasilisha mada kuhusu Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI wa
mwaka 2016/17 kwa wadau wa Utafiti huo wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Mjema
amefafanua kuwa, utafiti huu ni wa kwanza kukusanya taarifa
zinazohusiana na maambukizi mapya ya VVU, kiwango cha VVU mwilini kwa
watu wanaoishi na VVU na wastani wa maambukizi ya VVU kwa watu wa rika
zote pamoja na wingi wa chembechembe za kinga mwilini (CD4 T-cell
count).
Aidha,
utafiti huu utapima uwepo wa viashiria vya usugu wa dawa, kiwango cha
maambukizi ya kaswende pamoja na homa ya ini (Hepatitis B).
Akizungumzia
kiwango cha maambukizi ya VVU katika tafiti zilizopita, Mkuu wa Wilaya
huyo ameeleza kuwa, maambukizi yamepungua kutoka asilimia 7 mwaka 2003
mpaka asilimia 5.1 mwaka 2011 na kuifanya Tanzania kuwa ni miongoni mwa
nchi zenye kiwango cha chini cha maambukizi ya nchi za kusini mwa Jangwa
la Sahara ambapo nchi nyingi za ukanda huo zina kiwango cha zaidi ya
aslimia 10.
Baadhi
ya Washiriki waliohudhuria Mkutano wa Wadau wa Utafiti wa Viashiria na
Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016/17 uliofanyika hivi karibuni
jijini Dar es Salaam.
Nae
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Grace Magembe amesema kuwa,
kwa mkoa wa Dar es Salaam, utafiti huu utahusisha kaya zisizozidi 1,000
na Wananchi watakuwa na hiari ya kukubali kupima ambapo kwa wale
watakaogundulika kuwa na maambukizi, watapata rufaa ya kwenda kupatiwa
matibabu bure katika vituo vya kutolea huduma za afya.
"Utafiti
huu wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI hauhusishi watu wote bali ni kaya
chache tu ambazo zimechaguliwa kitaalam ili ziweze kuwakilisha kaya
nyingine na kwa hapa Dar es Salaam kaya zilizochaguliwa hazizidi 1000",
amesema Dkt. Magembe.
Utafiti
wa aina hii ni wa mara ya nne (4) kufanyika nchini Tanzania ambapo wa
kwanza ulifanyika mwaka 2003, wa pili mwaka 2007 na wa tatu mwaka 2011.
Utafiti
wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016 /17 unafanyika
nchini, chini ya usimamizi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa
kushirikiana na Wizara ya Afya kwa Tanzania Bara, Wizara ya Afya
Tanzania Zanzibar, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS),
Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) na Tume ya UKIMWI Zanzibar
(ZAC).
SHARE
No comments:
Post a Comment