Wananchi wa Pemba wahimizwa kuchangamkia fursa za kiuchumi katika Soko la EAC
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt.
Augustine Mahiga amewataka wakazi wa Pemba na Tanzania kwa ujumla
kuchangamkia ipasavyo fursa za Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika
Mashariki kwa ajili ya kujiongezea kipato.
Mhe.
Waziri alieleza kuwa katika ulimwengu wa leo hakuna nchi duniani
itakayoweza kujiimarisha kiuchumi peke yake bila kushirikiana na nchi
nyingine. Ndio maana hata zile nchi zilizoendekea kama Marekani na nchi
za Ulaya wana umoja wao kwa madhumuni ya kuongeza nguvu na kasi ya
maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Waziri
Mahiga aliyasema hayo alipokuwa anafungua semina kuhusu elimu ya
Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na fursa zake kwa wananchi wa
Pemba ambayo itatolewa na wataalamu wa Wizara yake kwa siku nne kuanzia
leo kwenye Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Gombani.
Mhe.
Waziri alieleza kuwa kabla, wakati na baada ya ukoloni nchi za Afrika
Mashariki zilikuwa na aina moja au nyingine ya Ushirikiano kwa madhumuni
ya kuimarisha uchumi wa nchi zao, waliotutawala. Aina moja ya
Ushirikiano ni ule Umoja wa Huduma ambao ulianzishwa mwaka 1961. Umoja
huo ulianzisha mashirika mbalimbali kama vile bandari, ndege, hali ya
hewa, posta na reli ambayo yalikuwa yanaendeshwa kwa pamoja.
Alisema
Tanzania ipo katika eneo la kimkakati ndani ya Jumuiya ikiwa ni pamoja
na kuwa na eneo kubwa kuliko nchi zote, idadi kubwa ya watu, ukanda
mkubwa wa bahari na ardhi nzuri yenye rutuba na kihistoria Pemba ni eneo
lenye rutuba nzuri kuliko maeneo yote ya Afrika Mashariki. Hivyo,
kutokana na sifa hizo hakuna budi wananchi wa Pemba na Tanzania kwa
ujumla kujipanga vizuri ili kuchangamkia fursa hizo badala ya kubaki
kuwa watazamaji na walalamikaji.
Waziri
Mahiga aliongeza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina sifa nyingine
ya pekee ya kuwa Muungano wa nchi mbili na kutoa wito kwa washiriki wa
semina hiyo kutumia sifa ya umoja wao kuziendea na kuzichangamkia fursa
za kiuchumi zilizopo kwenye Mtangamano.
"Nchi
nyingi barani Afrika na duniani kwa ujumla zilijaribu kuungana lakini
zilishindwa, kwa mfano nchi za Ghana, Mali na Guinea, nchi za Afrika
zinazozungumza kifaransa, nchi za Misri na Syria, nchi za Afrika ya Kati
na nchi za Pembe ya Afrika". “Ni sisi peke yetu hadi leo tumedumisha
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo juzi tu tuliadhimisha miaka 53 ya
muungano huo”. Waziri Mahiga alisema.
Aliendelea
kuueleza kuwa ni jukumu la kila Mtanzania kudumisha Muungano huo ambapo
kwa maneno yake alisema kuwa unaonewa wivu Afrika na duniani kote.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri wa Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora wa
Serikali ya Zanzibar, Mhe. Khamisi Juma Mwalim aliwasihi washiriki wa
semina hiyo kuzingatia mafunzo yanayotolewa katika semina hiyo ili
waweze kunufaika katika shughuli zao ikiwemo ujasiriamali.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 15 Mei, 2017
Waziri
wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine
Mahiga (Mb.), akizungumza kwenye ufunguzi wa semina ya Mtangamano wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki Kisiwani Pemba. Semina hiyo inatolewa kwa
wajasiriamali wa Pemba ili waweze kuchangamkia fursa za mtangamano.
Semina hiyo inafanyika katika Ukumbi wa Mikutano uliopo katika Uwanja wa
mpira wa Gombani.
Sehemu
ya wajumbe waliohudhuria semina hiyo, wa kwanza kushoto ni Mbunge wa
Konde Mhe. Mbarouk Ali akiwa pamoja na washiriki wengine wakifuatilia
kwa makini ufunguzi huo
Sehemu nyingine ya wajumbe wakimsikiliza kwa makini Waziri Mahiga hayupo pichani.
Naibu
Waziri wa Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora wa Serikali ya
Zanzibar Mhe. Khamis Juma Maalim akisoma hotuba ya ukaribisho.
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi naye akielezea jambo kwenye ufunguzi
wa semina hiyo ya Mtangamano wa Afrika Mashariki.
Mwenyekiti
wa wafanyabiashara wa Sanday markert kutoka Pemba, Bw.Khamis Suleiman
Masoud akitoa neno la shukrani kwa Mhe. Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki (hayupo pichani).
Mkuu
wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga akitoa ufafanuzi
masuala mbali mbali kuhusiana na semina hiyo.
Ufunguzi wa Semina ukiendelea
Wakiwa katika picha ya pamoja.
SHARE
No comments:
Post a Comment