Na Eliphace Marwa – Maelezo
Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama
Barabarani Makao Makuu Jijini Dar es Salaam limetahadharisha, madereva
kuwa makini wakati wakiendesha vyombo vya moto ili kuepuka ajali
zinazosababishwa na ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani.
Hayo yamesemwa na Kaimu Kamanda wa
Kikosi cha Usalama barabarani SACP Fortunatus Muslimu wakati akitoa
taarifa ya hali ya usalama barabarani katika kipindi cha kuanzia mwezi
Januari mpaka Mei mwaka huu ukilinganisha na kipindi kama hicho kwa
mwaka jana.
Akisoma taarifa hiyo kwa waandishi
wa habari Kamanda Muslimu amesema kuwa ajali za barabarani zimepungua
ukilinganisha na mwaka jana kwani katika kipindi cha mwezi Januari mpaka
Mei jumla ya ajali za magari zilikuwa 4,177, vifo 1,286 na majeruhi
3,882 ukilinganisha na ajali 2,411, vifo 1,034 na majeruhi 2,291 katika
kipindi kama hicho mwaka huu.
Aidha kwa upande wa ajali za
pikipiki Kamanda Muslimu amesema kuwa katika kipindi cha Januari mpaka
Mei mwaka jana jumla ya ajali za pikipiki zilikuwa 1,110, vifo 347 na
majeruhi 950 ukilinganisha na ajali 607, vifo 302 na majeruhi 455 katika
kipindi kama hicho mwaka huu.
Pamoja na kupungua kwa ajali
nchini Kamanda Muslimu amesema kuwa ajali nyingi zimekuwa zikisababishwa
na makosa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja mwendokasi wa madereva, kupita
magari bila ya tahadhari, ulevi pamoja na kubeba abiria kupita kiasi kwa
njia zilizo hatarishi.
Kamanda Muslimu aliongeza kuwa kwa
sasa ukamataji wa makosa ya barabarani yatakuwa kipaumbele, hivyo
dereva atakeyekiuka sheria atachukuliwa hatua palepale ili kujenga utii
wa sheria bila ya shuruti.
“Ukamataji wa makosa utakuwa ni
moja ya kipimo cha utendaji wa askari barabarani ili waweze kukamata
makosa mengi mpaka pale madereva watakapoacha kukiuka sheria”, alisema
Kamanda Muslimu.
Aidha Kamanda Muslimu amesema kuwa
jeshi hilo halitomuonea mtu wala kumbambikia mtu makosa kwani ukamataji
huo wa makosa ya barabarani unalenga kuzuia ajali na sio kukusanya
mapato na hivyo kuwataka askari kuacha kufanya kazi kwa mazoea bali
wafanye kazi kwa nidhamu na maadili ya jeshi hilo.
Kamanda Muslimu amewataka
watumiaji wa barabara kutii sheria za usalama barabarani ili kuepuka
ajali zisizokuwa za lazima ambazo husababisha vifo na majeruhi na
kupelekea kuathiri uchumi wa jamii na nchi kwa ujumla kutokana na
kupoteza nguvu kazi ya Taifa.
SHARE
No comments:
Post a Comment