TRA

TRA

Sunday, July 23, 2017

BALOZI MBELWA KAIRUKI ATAKA WATANZANIA KUCHANGAMKIA SOKO LA MIHOGO CHINA

Share On Facebook ! Tweet This ! Share On Google Plus ! Pin It ! Share On Tumblr ! Share On Reddit ! Share On Linkedin ! Share On StumbleUpon !




NA IDARA YA HABARI (MAELEZO)
BALOZI wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki, amewataka Watanzania kujikita katika kilimo cha muhogo baada ya zao hilo kupata soko la uhakika nchini China.
 
Balozi Kairuki alielezea fursa hiyo ya soko mwishoni mwa wiki alipofanya mahojiano na Idara ya Habari (MAELEZO) kuhusiana na fursa za biashara zinazopatikana China ambazo Tanzania inaweza kuzitumia ili kukuza uchumi.
 
Alieleza kuwa mwezi Mei mwaka huu, Serikali kupitia Ubalozi wake nchi China walisaini mkataba ambao unairuhusu Tanzania kuuza zao muhogo katika nchi hiyo, fursa ambayo Watanzania wanapaswa kuitumia kikamilifu kwa kufanya kilimo cha kisasa ili kuzalisha kwa wingi zao hilo kwa ajili ya kuuza nje.
 
“Tukichangamkia hii fursa ya muhogo tunaweza kusafirisha tani nyingi. Tunaweza hata kuanza kwa kusafirisha muhogo wenye thamani ya dola milioni 500 na baadae tukikua tunaweza kusafirisha muhogo wenye thamani ya bilioni mbili hadi tatu kwa mwaka”, alieleza Balozi Kairuki.
 
Alieleza kuwa kwa sasa Nigeria ndiyo nchi pekee kutoka Afrika ambayo inauza muhogo nchini China na inakusudia kuuza tani milioni 150 za muhogo na kwamba kijiografia Tanzania ina nafasi nzuri zaidi ya kuuza zao hilo kuliko Nigeria ambayo ni ya nne duniani kwa kuuza muhogo nchini China, ikitanguliwa na Thailand, Brazil na Indonesia.
 
Ili kulima kilimo chenya tija, Balozi Kairuki alishauri Watanzania kutumia teknolojia ya kisasa katika kuzalisha muhogo ikiwemo ile inayotumiwa na nchi ya Thailand ambayo hekta moja inazalisha mpaka tani 25 au teknolojia ya China ambayo hekta moja inazalisha tani 15 hadi 20 tofauti na Tanzania ambapo hekta moja huzalisha tatu hadi saba.
 
Alieleza kuwa ili kutatua changamoto katika kilimo cha muhogo, ofisi ya Ubalozi kwa kushirikiana na mamlaka za China na Watanzania wanaosoma China katika fani ya kilimo wamejaribu kuzishawishi taasisi za utafiti za China zishirikiane na taasisi za Tanzania ili kuwezesha kupata mbinu za kuongeza uzalishaji.
 
Aidha, Balozi Kairuki ametoa wito kwa wadau wote wa kilimo ikiwemo Wizara ya Kilimo, halmashauri pamoja na Kituo cha Utafiti cha Naliendele kuunganisha nguvu pamoja ili kutatua changamoto katika zao la muhogo na kuwawezesha wakulima kutumia vizuri fursa ya soko la muhogo nchini China.
 
Kwa mujibu wa takwimu, Tanzania ni nchi ya nne kwa uzalishaji muhogo barani Afrika ikitanguliwa na nchi za Nigeria, Ghana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Author:

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment

 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger