Nyota wa muziki wa
Pop kutoka Canada Justin Bieber amepigwa marufuku kutumbuiza nchini
China, kwa mujibu wa Wizara ya Utamaduni nchini humo.
"Justin Bieber ni mwimbaji mwenye kipaji, lakini pia ni mwanamuziki kijana mwenye kuzua utata," amesema.
Taarifa hiyo imetolewa kujibu swali lililokuwa limeulizwa na mmoja wa watu katika tovuti ya wizara hiyo.
"Twatumai kwamba Justin Bieber atakapokomaa, anaweza kuendelea kuimarisha maneno yake na matendo, na kuwa mwanamuziki anayependwa kwa dhati na umma," taarifa hiyo imesema.
Mwandishi wa BBC jijini Beijing John Sudworth anasema China inaonekana sasa kumuweka Bieber katika orodha sawa na Dalai Lama na watu wanaopigania kujitenga kwa Taiwan, japo labda chini yao.
Taarifa hizo zimetolewa baada ya wizara hiyo kujibu maswali kuhusu shabiki mmoja aliyeshangaa ni kwa nini hakuna ukumbi hata mmoja umetajwa kuwa utakuwa mwenyeji wa Bieber ilhali anatarajiwa kuanza ziara yake Asia karibuni.
- Justin Bieber aonekana akimpiga ngumi shabiki wake
- Matusi yamfanya Justin Bieber kufunga akaunti yake ya Instagram
Wengine ni bendi ya Uingereza kwa jina Oasis na kundi la Marekani kwa jina Maroon 5, ambao wamepigwa marufuku kwa sababu ya misimamo yao ya kisiasa badala ya tabia.
Mwaka 2014, Bieber, maarufu kwa wimbo wake Sorry alizua utata baada ya kupakia picha aliyopigwa akitembelea madhabahu ya Yasukuni jijini Tokyo.
Madhabahu hayo nchini Japan yalijengwa kwa heshima ya wanajeshi waliouawa vitani pamoja na wahalifu wa kivita lakini nchini China na Korea Kusini, hutazamwa kama ishara kwamba Japan haijajutia makosa yaliyotendwa na watawala wa nchi hiyo China na Japan miaka ya nyuma.
SHARE
No comments:
Post a Comment