NA SHAMIMU
NYAKI WHUSM
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk
Harrison Mwakyembe, amesitisha uteuzi wa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo
la Taifa, (BMT), Deonis
Malinzi na wajumbe wote wa Baraza hilo
kuanzia leo Julai 10, 2017 kufuatia Baraza hilo kushindwa kutatua changamoto
mbalimbali zinazoikabili sekta ya Michezo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es
Salaam leo Dkt Mwakyembe ameeleza kuwa, amelivunja Baraza hilo kwa
mamlaka aliyopewa na Sheria ya BMT Na.12 ya mwaka 1967 iliyofanyiwa marekebisho
na Sheria Na.6 ya mwaka 1971 pamoja na kanuni zake za mwaka 1999.
Dionis Malinzi |
“Mhe. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliniagiza
nilifanyie mapitio na kulitathmini upya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ili
kujiridhisha na usimamizi wake wa shughuli za michezo nchini, na kwamba
ikidhihirika kwamba usimamizi wa BMT wa michezo nchini si imara basi ninaweza
kulivunja Baraza lililopo na kuunda upya.” Alisema Waziri Mwakyembe.
Aidha Waziri Mwakyembe ameeleza kuwa Baraza hilo
limeshindwa kutafuta njia bora za kuondoa changamoto ambazo zilikua zinahitaji
utashi na dhamira ya kujituma, ikiwemo Viongozi wa michezo kushika nafasi
zaidi ya moja, kushindwa kusimamia ushiriki wa wanamichezo wa Tanzania na wa
nje katika michezo mbalimbali.
Pia Waziri Mwakyembe alizitaja sababu nyingine za
kuvunjwa kwa BMT kuwa ni Uchaguzi wa vyama vya michezo nchini
kugubikwa na ubabe na rushwa, mapromota wa mchezo wa ngumi nchini kuendesha
shughuli zao bila kusajiliwa, pamoja na kanuni za vyama vya michezo kukosa
uhakiki wa kubaini upungufu kuhusu masuala ya fedha.
Hata hivyo Sektretarieti ya Baraza itaendelea
kufanya kazi katika kipindi hiki kwa kushirikiana kwaukaribu na Wizara ya
Habari Utamaduni Sanaa na Michezo wakati taratibu za kumpata mwenyekiti na
wajumbe wapya zikiendelea kufanyika kwa mujibu wa Sheria.
SHARE
No comments:
Post a Comment