Upinzani waonesha kuwa na matumaini machache katika
kufanikiwa mazungumzo ya Geneva ambayo ni duru ya saba tangu zilipoanza
juhudi za Umoja wa Mataifa miaka miwili iliyopita
Mjumbe wa Umoja wa mataifa kwa Syria Staffan De Mistura ameanzisha
duru mpya ya mazungumzo yasiyozihusisha moja kwa moja pande zinazovutana
katika mgogoro wa Syria,ikiwa ni duru ya saba ya mazungumzo kufikia
sasa kati ya wajumbe wa serikali ya Syria na viongozi wa upinazni.
Mchakato huo ni hatua ya juihudi za kujaribu kutafuta mwafaka wa mgogoro
huo ulioiharibu vibaya nchi hiyo.Mazungumzo yanayosimamiwa na Staffan De Mistura yanatarajiwa kuendelea kwa wiki nzima na tayari amekwishazungumza na ujumbe wa serikali ya Syria unaoongozwa na balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa Bashar al Jafaari,lakini De Mistura amekataa kuzungumzia chochote kuhusu matarajio yake ingawa anatazamiwa kuitisha mkutano na waandishi habari baadae leo.
Upinzani umeshasema kwamba matumaini yake ni machache mno katika kikao cha Geneva.Duru hii mpya ya mazungumzo ni ya saba katika msururu wa duru za mazungumzo ya kutafuta amani ya nchi hiyo ambazo zimekuwa zikifanyika nchini Uswisi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita ambapo hakuna hata duru moja iliyofanikiwa kupata mwafaka wa mgogoro huo na kwa sehemu kubwa duru hii ni kujaribu kuhakikisha inapatikana fursa ya kupelekwa msaada wa kibinadamu nchini Syria na kuandaa mikakati ya baada ya kumalizika vita.
Kuanza kwa mazungumzo hayo kumekuja wakati ambapo kumefikiwa makubaliano ya kusitisha vita upande wa kusini mwa Syria leo hii hatua ambayo ilisimamiwa na Marekani na Urusi pamoja na Jordan wiki iliyopita.Mwanaharakati wa upinzani Ahmad al-Masalmeh anasema hali ni ya utulivu katika mji wa Daraa karibu na mpaka wa Jordan,ingawan kundi linalofuatilia haki za binadamu kutokea nchini Uingereza limeripoti juu ya kutokea mashambulizi madogo katika mji huo usiku wa kuamkia leo. Utulivu huo unafuatiliwa kwa karibu ikiwemo na Israel ambapo waziri wake wa anayehusika na masuala ya ujasusi na usafiri Yisrael Katz ametowa mwito wa tahadhari kufuatia hatua hiyo akisema nchi yake haitokubali uwepo wa vikosi vya Iran wala Hezbollah katika eneo hilo la mpaka.
Makubaliano ya kusitisha vita yanahusisha mikoa mitatu ya Kusini mwa Syria na ni hatua ya matokeo thabiti yaliyofuatia mkakati wa miezi kadhaa na diplomasia kati ya serikali mpya ya Trump na rais wa Urusi Vladmir Putin.Kauli ya Israel imetolewa huku Umoja wa Mataifa kwa upande wake ukiendeleza juhudi za kusaka amani ambazo kwa sehemu zinataka kuhakikisha msaada wa kibinadamu unapata nafasi ya kupelekwa nchini Syria pamoja na kuweka misingi ya kujaribu kuumaliza mgogoro huu wa wenyewekwa wenyewe ulioingia mwaka wa saba.Zaidi ya watu 400,000 wanakadiriwa kuuwawa kufuatia vita hivyo na mazungumzo ya kujaribu kuzileta pande zote zinazovutana katika meza ya mazungumzo yanajikita katika masuala ya katiba serikali,magaidi na uchaguzi.
SHARE
No comments:
Post a Comment