Wakati
Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema akisema haogopi kusema
ukweli, Mkuu wa mkoa huo, Mrisho Gambo amemtahadharisha kuwa hataacha
kumchukulia hatua iwapo atamtukana Rais John Magufuli na Serikali yake.
Lema
ambaye ameanza kufanya mikutano ya hadhara katika jimbo lake jana
kwenye Soko Kuu la Arusha mjini alisema haogopi kusema ukweli hata kama
akipingwa na baba yake mzazi.
“Taifa lipo kwenye mgawanyiko mkubwa, wakuu wa wilaya na mikoa wanafanya maamuzi kwa maelekezo kutoka ngazi za juu,” alisema.
Aliongeza
kuwa hali ya demokrasia nchini ni mbaya kwa kuwa hakuna usawa na
kuwataka viongozi kuomba hekima wanapopata mamlaka ya uongozi.
Kadhalika
amezungumzia hatua ya kujiuzulu kwa Diwani wa Muriet, Credo Kifukwe
akisema kuwa Chadema haihitaji jeshi la watu wengi bali la wachache
wenye umoja.
“Nimeteswa
sana katika mji wa Arusha, lakini nawataka wafuasi wa Chadema msilipize
kisasi kwa wanaohama chama. Leo wapinzani hawaruhusiwi kufanya siasa,
lakini Rais anazunguka nchi nzima,” alisema.
Mbunge
huyo alisema Tanzania inahitaji demokrasia ya kweli na amani ya nchi
haiwezi kutunzwa na polisi isipokuwa kwa upendo wa Watanzania.
Pia, alimtaka Gambo kujipanga wakati wa uchaguzi mdogo wa madiwani kwa kuwa Chadema imejipanga kikamilifu.
Katika
mkutano huo, Lema aliwapandisha jukwaani madiwani wawili wa Chadema
jijini Arusha, Obeid Meng’roriki wa Kata ya Terat na Ruben Ngowi wa
Kimandolu huku akisema amesikia wanataka kujiuzulu nyadhifa zao.
Hata hivyo, madiwani hao waliposimama walisema wao hawana bei ya kuweza kununuliwa na mtu yeyote.
Wakati
Lema akiyasema hayo, Gambo alisema Serikali ya Awamu ya Tano
imejipambanua katika utendaji wake, hivyo mwanasiasa yeyote hataruhusiwa
kutoa matamshi yenye kumdhihaki Rais na Serikali.
Akizungumza katika mkutano na viongozi wa madhehebu ya dini uliofanyika jana kwenye ukumbi wa mikutano wa AICC alisema: “Tumempa
mbunge wa jimbo hili (Arusha Mjini) kibali cha kufanya mikutano na
wananchi wake kwa sababu ni kiongozi aliyechaguliwa na wananchi, hatuna
sababu ya kumzuia, ila hatutakubali kusikia kwenye mikutano yake
akimtukana Rais wetu na Serikali yake. Akifanya hivyo tutamshughulikia.”
“Mtu
yeyote anayetaka kuichezea Serikali na kutaka kukwamisha ajenda zake
tutawang’oa iwe kwa greda au kwa namna nyingine yoyote, Rais Magufuli
alipita nchi nzima akitoa ahadi zake na wamemchagua sasa wamwache
atekeleze alichowaahidi wananchi.”
SHARE
No comments:
Post a Comment