Waziri
wa Maji na Umwagiliaji, Inj. Gerson Lwenge akiwa kwenye mazungumzo na
Waziri wa Maji na Umwagiliaji wa Misri, Dkt. Mohamed Abdel Aty (wa
kwanza kushoto), akifuatiwa na Balozi wa Misri nchini Tanzania, Yasser
Ahmed Al Eldin Elshawaf (katikati) na Kansela wa Ubalozi wa Misri nchini
Tanzania, Moataz Kareem.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo akizungumza akiwa na
Mwenyekiti wa Sekta ya Maji ya Nile, Ahmed Bahaa Eldin Mohamed (kulia),
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Inj. Gerson Lwenge (kushoto) katika
kikao.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Inj. Gerson Lwenge akizungumza mbele ya ujumbe wa Misri na Tanzania katika kikao.
Waziri
wa Maji na Umwagiliaji, Inj. Gerson Lwenge akiwa na Waziri wa Maji na
Umwagiliaji wa Misri, Dkt. Mohamed Abdel Aty na ujumbe wake katika
sehemu ya mabanda katika Maonesho ya Sabasaba.
Waziri
wa Maji na Umwagiliaji, Inj. Gerson Lwenge akikabidhiwa zawadi na mmoja
wa wafanyabiashara kutoka Misri pamoja na Waziri wa Maji na Umwagiliaji
wa Misri, Dkt. Mohamed Abdel Aty katika banda kwenye Maonesho ya
Sabasaba.
…………………………………………………………………………………
Waziri wa Maji na Umwagiliaji,
Inj. Gerson Lwenge amekutana na Waziri wa Maji na Umwagiliaji wa Misri,
Dkt. Mohamed Abdel Aty kwa mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano baina ya
Serikali za Tanzania na Misri katika utekelezaji wa miradi ya Sekta za
Maji na Umwagiliaji.
Kikao hicho kilichofanyika katika
Ofisi za Wizara za Dar es Salaam kilihusisha mazungumzo ya utekelezaji
wa makubaliano ya ushirikiano wa mataifa ya Misri na Tanzania, hususani
katika utekelezaji wa miradi ya majisafi na kilimo cha umwagiliaji
nchini kwa serikali hizo mbili.
Katika kikao hicho Inj. Lwenge
alisema Tanzania na Misri ni mataifa yanayoshirikiana katika sekta
mbalimbali, na kupitia ushirikiano huo lengo kubwa ni kuinua Sekta za
Maji na Umwagiliaji.
“Kwa msaada wa Serikali ya Misri,
serikali imefanikiwa kutekeleza mradi wa maji wa visima 30 kwa ajili ya
uboreshaji wa huduma ya majisafi kwa wilaya kame za Same, Mwanga,
Kiteto, Bariadi na Itilima kwa awamu ya kwanza na bado wapo katika
mazungumzo ya kutekeleza miradi mingine mingi”, alisema Waziri Lwenge.
“Lakini pia tuna lengo la
kuendeleza kilimo cha umwagiliaji, kwa kutumia teknolojia ya kisasa
yenye kutumia maji kidogo na kuzalisha chakula kingi. Hivyo, kwa
kushirikiana na wenzetu wa Misri wenye utaalamu wa hali ya juu, tunataka
kufanikisha jambo hilo ili tuhakikishe usalama wa chakula na chakula
kutosha kwa ajili ya wananchi”.
Inj. Lwenge alisema ushirikiano
baina ya Serikali za Tanzania na Misri utaleta tija kwa Tanzania, hasa
ikizingatiwa taifa hilo limepiga hatua kubwa katika Sekta za Maji na
Umwagiliaji na kwa kubadilishana uzoefu, kutaisaidia Tanzania kupiga
hatua kubwa katika sekta hizi muhimu kwa taifa katika kutizima azma ya
Serikali ya Awamu ya Tano ya Tanzania kuwa Nchi ya Viwanda.
Naye, Waziri wa Maji na
Umwagiliaji wa Misri, Dkt. Mohamed Abdel Aty alisema wataendelea
kudumisha uhusiano wake na Tanzania kwa kuchangia maendeleo ya Tanzania
kupitia ushirikiano kwenye sekta za maji, umwagiliaji na hata
usafirishaji utakaoleta tija kubwa kwa ustawi wa mataifa haya.
Dkt. Abdel Aty aliambatana na
ujumbe uliojumuisha Balozi wa Misri nchini Tanzania Yasser Ahmed Al
Eldin Elshawaf, Mwenyekiti wa Sekta ya Maji ya Nile, Ahmed Bahaa Eldin
Mohamed na Kansela wa Ubalozi wa Misri nchini Tanzania, Moataz Kareem,
huku ujumbe wa Inj. Lwenge ukijumuisha Katibu Mkuu wa Wizara ya
Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo, Mkurugenzi Msaidizi wa Majishirikishi,
Sylivester Matemu, Mkurugenzi Msaidizi Mipango na Utafiti, Dkt. George
Lugomela na Mkuu wa Kitengo cha Sheria, Simon Nkanyemka.
Aidha, Waziri Lwenge alimpeleka
mgeni wake, Waziri Abdel Aty kutembelea Maonesho ya 38 ya Biashara ya
Kimataifa – Sabasaba, kwa nia ya kumuonyesha maendeleo ya Sekta ya
Biashara nchini, yaliyovutia kampuni 25 kutoka Misri na kushiriki katika
maonesho hayo.
SHARE
No comments:
Post a Comment